Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anayemaliza muda wake, Dk Richard Sezibera
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anayemaliza muda wake, Dk Richard Sezibera amesema sera ya jumuiya ya uanzishaji wa viwanda itatengeneza ajira milioni 2.3 kwa wananchi wa Afrika Mashariki.
Dk Sezibera aliyasema hayo jana wakati akitoa hotuba yake ya kuaga Bunge la Afrika Mashariki (Eala), linaloendelea na vikao vyake jijini Dar es Salaam. Alisema mpango wa viwanda utakuwa na manufaa makubwa na kupunguza uingizaji wa bidhaa kutoka nje.
Alisema sekretarieti ya EAC imeandaa Dira ya 2050 kwa ajili ya kusimamia mipango ya maendeleo, lengo kuu ni kuhakikisha ifikapo mwaka huo pato la mwananchi wa chini linakuwa Dola 10 za Marekani.
“Ninaliomba Bunge hili lifuatilie dira hii kuhakikisha inatekelezwa kama ilivyopangwa, ni kitu kizuri ambacho kitaipeleka mbele jumuiya yetu,” alisema.
Sezibera alisema anajivunia mafanikio yaliyopatikana wakati wa uongozi wake, huku akitaja baadhi kuwa ni uhuru wa watu kutembea ndani ya jumuiya.
Alitolea mfano nchini za Kenya, Uganda na Rwanda ambazo tayari wanatumia kitambulisho cha taifa kusafiria kutoka nchi moja kwenda nyingine. Alisema bado wanaendelea kufanyia kazi suala la kuunganisha elimu ya juu.
ili wanafunzi waweze kusoma katika chuo chochote ndani ya Afrika Mashariki kwa viwango vya ubora vile vile vinavyotolewa katika vyuo vingine.
“Mkutano wa 17 wa wakuu wan chi ulijadili umuhimu wa kuwa na pasi ya kusafiria moja ndani ya Afrika Mashariki. Ninaimani kwamba siku moja suala hilo litakamilika na kuwa na passport moja kwa nchi zote,” alisema.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa mchakato wa kuwa na sarafu moja nao bado unaendelea. Alisema itifaki ya sarafu ya pamoja ni muhimu licha ya kwamba ina changamoto zake. Alisema hatua zinaendelea vizuri kukamilisha itifaki hiyo.
Katibu huyo alisema “Tunajua jinsi Umoja wa Ulaya (EU) unavyopata shida katika suala hili, lakini tutafanikiwa tu. Suala la kuunganisha taasisi za fedha pia linaendelea vizuri,” alisema Sezibera ambaye anamaliza muda wake rasmi Mei, mwaka huu.
Kuhusu kuongeza muingiliano wa watu wa Afrika Mashariki, Sezibera alisema mpaka sasa kuna miradi ya miundombinu itakayogharimu Dola za Marekani bilioni 100. Alitolea mfano mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa itakayopita katika nchi zote za Afrika Mashariki.
Alisema mradi mwingine ni uwekezaji kwenye nishati ambao nao umefikia hatua nzuri. Alisema watu wa Afrika Mashariki wanashirikishwa kikamilifu kupitia majukwaa mbalimbali kama vile umoja wa vijana, serikali za mitaa, mabunge, viongozi wa dini na vyama vya wakulima.
“Tumepitia upya pia taasisi za EAC ili kuangalia ufanisi wake na kufanya mabadiliko. Mambo mengi yamefanyika lakini bado tuna mengi yanatakiwa kufanyika. Tuziti kushirikiana ili kufikia malengo yetu,” alisema.
No comments:
Post a Comment