Ofisa wa Mawasiliano wa WB Tanzania, Loy Nabeta
Dar es Salaam. Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia (WB), imeipiga jeki Serikali baada ya kupitisha Dola 70 milioni za Marekani (Sh152.6 bilioni) kwa ajli ya kusaidia ukuaji wa sekta ya kilimo ili kuchochea maendeleo nchini.
Uamuzi wa bodi hiyo uliofikiwa jana, umelenga kuimarisha na kuwaunganisha wakulima wadogo na mnyororo wa thamani wa sekta hiyo inayotegemewa na takriban asilimia 80 ya Watanzania kuongeza vipato vyao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisa wa Mawasiliano wa WB Tanzania, Loy Nabeta, fedha hizo zitasaidia utekelezaji wa mradi wa Ukuzaji Kilimo Ukanda wa Kusini (SAGCOT) uliopo chini ya mkakati wa Taifa wa maendeleo kwa ajili ya kuimarisha biashara ya kilimo kwa kukabiliana na kiwango kidogo cha uzalishaji na ukosefu wa masoko ya uhakika.
Fedha hizo zimetolewa na Benki ya Dunia kupitia uwekezaji wa Taasisi ya Maendeleo ya Kimataifa (IDA), zikilenga pia kuongeza fursa za kipato kwa kaya zaidi ya 100,000 za wakulima wadogo ambao watapatiwa teknolojia mpya na njia bora za masoko katika ukanda huo.
Bella Bird ambaye ni Mkurugenzi Mkazi wa WB Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, alisema wakulima wadogo ni nguzo muhimu ya ukuaji wa sekta ya kilimo inayochangia kwa kiasi kikubwa cha pato la Taifa.
Mradi huo unaojumuisha zaidi ya theruthi ya nchi, unawanufaisha zaidi ya watu 500,000 na kuwahusisha wafanyabiashara wakulima wakubwa 40, hususan wanawake, katika mnyororo wa thamani wa kilimo.
No comments:
Post a Comment