Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetoa ripoti inayoonesha kuwa, kundi la kigaidi la Boko Haram liliwateka mamia ya wanawake na watoto katika mji wa Damasak kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Shirika hilo limewanukuu wakazi wa mji wa Damasak na kufichua kwamba, Novemba mwaka 2014, kundi la kigaidi la Boko Haram liliwateka nyara takribani wanawake na watoto 500 katika mji huo ulioko kaskazini mashariki mwa Nigeria. Ripoti hiyo inaeleza kuwa, wakazi wa mji wa Damasak wanafahamu kuhusiana na utekaji nyara huo lakini wameamua kunyamaza kimya wakihofia hasira za serikali ambayo haitaki kufichuliwa habari za utekaji nyara huo. Serikali ya wakati huo ya Nigeria chini ya uongozi wa Rais Goodluck Jonathan, Machi mwaka jana sio tu kwamba, haikutangaza habari ya kutokea operesheni kubwa ya Boko Haram huko Damasak iliyopelekea kutekwa nyara takribani wanawake na watoto 500, bali ilikanusha habari za kuweko tukio kama hilo.
Human Rights Watch inafichua habari hiyo katika hali ambayo, Aprili mwaka 2014, kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram lilivamia shule moja ya bweni ya wasichana iliyoko eneo la Chibok mkoani Borno kaskazini mwa Nigeria na kuwateka nyara wanafunzi wapatao 276, ambapo licha ya baadhi yao kukombolewa, makumi ya wasichana hao hadi leo bado wanashikiliwa na wanamgambo hao.
No comments:
Post a Comment