Tuesday, March 29, 2016

Mwelekeo mpya wa Uchumi wa China, msisitizo kwenye ubora wa uchumi







Mkutano wa mwaka wa bunge la umma la China unaowakutanisha wabunge elfu tatu kutoka nchi nzima, umemalizika hivi karibuni jijini Beijing China. Mbali na kujadili mambo mbalimbali yanayohusu nchi, mkutano huo pia ulipitia na kujadili ripoti ya kazi za serikali inayoeleza mipango ya utekelezaji wa kazi za serikali kwa mwaka huu, na kuandaa rasimu ya utekelezaji wa mpango wa 13 wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Jambo kubwa zaidi lililofuatiliwa zaidi katika mkutano wa bunge la umma kwa mwaka huu, lilikuwa ni mwelekeo wa uchumi wa China. Kwanza ni kutokana na umuhimu wa mchango wa China kwenye uchumi wa dunia, hasa katika wakati huu ambapo China inatajwa kutoa mchango chanya katika kufufua uchumi wa dunia, kwa kuwa soko kubwa la bidhaa na kivutio cha uwekezaji kwa nchi nyingi duniani. Na pili ni kuwa China imekuwa ni mwekezaji muhimu katika nchi za nje kwenye miradi ya viwanda na ujenzi. Mabadiliko yoyote ya kisera na hata kiutendaji yanayoweza kuamuliwa na bunge, yanaweza kuwa na athari za moja kwa moja kwa wanaotaka kuwekeza China, na wanategemea kupata uwekezaji kutoka China.
Kama ilivyo desturi, kwenye ufunguzi wa mkutano wa Bunge Waziri Mkuu wa China aliwasilisha ripoti kuhusu kazi zinazotarajiwa kufanywa na serikali kwa mwaka huu. Moja ya mambo yaliyotajwa kwenye ripoti hiyo ni kuwa, serikali imeweka lengo la makadirio ya ongezeko la uchumi kuwa kati ya asilimia 6.5 na asilimia 7. Makadirio haya ni ya chini kabisa katika kipindi cha miaka 30 ya utekelezaji wa sera ya mageuzi na ufunguaji mlango, na yamefanya watu kuwa na maoni mbalimbali kuhusu mwelekeo wa uchumi wa China.
Makadirio ya asilimia 6.5 yanaweza kuonekana ni ya chini kwa nchi ambayo kwa kipindi kirefu ongezeko lake limekuwa karibu asilimia 10. Lakini tukifuatilia kwa undani yaliyotajwa na waziri mkuu wa China kwenye ripoti ya kazi ya serikali, inaonekana kuwa msisitizo kwenye ongezeko la uchumi wa China kwa sasa, hautakuwa tena kwenye tarakimu kubwa za ongezeko la pato la taifa GDP, bali kwenye ubora wa uchumi wenyewe.
Kwa sasa lugha inayotumiwa zaidi hapa China kuhusu mabadiliko ya muundo wa uchumi ni "hali mpya ya kawaida" (new normal). Hii ina maana kuwa zama ya ongezeko la kasi kubwa ya uchumi, ambayo ilikuwepo kwa miongo miwili iliyopita sasa haipo tena, na badala yake msisitizo kwenye maendeleo ya uchumi umehama kutoka kutegemea zaidi biashara ya nje na uwekezaji kuwa chanzo kikuu cha ongezeko la uchumi, na kuwa kuongeza mchango wa matumizi ya ndani kuwa injini muhimu ya ongezeko la uchumi.
Kulingana na badiliko hilo, mfumo wa kutathmini utendaji wa serikali za ngazi mbalimbali pia umefanyiwa marekebisho, kwamba utendaji wa viongozi wa serikali za mitaa sio tu utapimwa kwa kuangalia kazi wanazofanya katika kuhimiza ongezeko la uchumi, bali vigezo vingine kama vile vinavyohusu mazingira na kuinua viwango vya maisha ya watu pia vitafuatiliwa. Kwa ujumla vigezo hivyo vinatumiwa kupima kama maendeleo yanapatikana katika hali nzuri, na kwa njia endelevu.
Baadhi ya vyombo vya habari vya nchi za magharibi vimekuwa vikionesha wasiwasi kuhusu kupungua kwa kasi ya ongezeko la uchumi wa China, na hata kufikia hatua ya kusema kupungua huko kunaweza kuathiri maendeleo ya nchi za Afrika zenye ushirikiano wa karibu na China, ikiwa ni pamoja na nchi zinazouza malighafi kwa wingi nchini China hasa mafuta na madini. Baadhi ya vyombo hivyo vimedhiriki kusema China itapunguza uwekezaji wake kwa nchi za Afrika.
Tukiangalia kwa undani tunaweza kuona kuwa hofu hii haina msingi, na haiendani na hali halisi iliyopo kwenye uhusiano wa kiuchumi kati ya China na nchi za Afrika. Kwanza ni kuwa ni nchi chache tu za Afrika zinazouza nishati kwa wingi kwa China, na nchi hizo hazitegemei bidhaa moja tu. Lakini pia hali ya kupungua kwa uchumi wa China haijaanza mwaka huu, na katika kipindi chote ambacho ongezeko la uchumi wa China limekuwa likipungua thamani ya biashara kati ya China na nchi za Afrika imekuwa ikiongezeka, na sasa imefikia dola bilioni 222. Mbali na hizo ni uwekezaji wa moja kwa moja wa China barani Afrika pia umeongezeka na kufikia dola za kimarekani bilioni 2.5
Kuna mifano wazi inayoonekana kwenye uwekezaji kwenye miradi mikubwa kama vile reli kati ya Mombasa na Nairobi na reli nyepesi ya mjini Addis Ababa. Miradi hii imewekezwa wakati kasi ya ongezeko la uchumi wa China imepungua. Mwelekeo huu pia unaendelea, ni hivi karibuni tu Rais Xi Jinping wa China alitangaza kwenye mkutano wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mjini Johannesburg, mipango kumi ya ushirikiano yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 60.
Tunatakiwa kukumbuka pia kuwa, kwa sasa mchango wa matumizi ya ndani kwa uchumi wa China umeongezeka na kufikia karibu asilimia 50. Hali hii imechangiwa na hatua za serikali kuhumiza matumizi ya ndani na kuongezeka kwa mapato ya watu wa tabaka la kati. Kati ya bidhaa zinazotumiwa ni pamoja na zile zinazozalishwa kwa wingi barani Afrika kama vile mvinyo na kahawa, hii pia ni fursa nyingine sawa na ile ya orodha ndefu ya bidhaa za kilimo za nchi za Afrika zinazoruhusiwa kuingia kwenye soko la China bila ushuru.
Kwa hiyo wakati China ikiendelea na juhudi za kubadilisha muundo wa uchumi wake, tunachotakiwa kufanya ni kuangalia ni vipi mabadiliko hayo na utekelezaji wa mpango wake wa 13 maendeleo, utakuwa fursa kwa maendeleo ya nchi zetu.
Unknown Web Developer

Morbi aliquam fringilla nisl. Pellentesque eleifend condimentum tellus, vel vulputate tortor malesuada sit amet. Aliquam vel vestibulum metus. Aenean ut mi aucto.

No comments:

Post a Comment