Gwiji wa soka ya Brazil Pele ameishataki kampuni ya kutengeza bidhaa za kielektroniki ya Samsung kwa kutumia mfano wake katika matangazo ya kibiashara bila idhini.
Pele anataka kampuni hiyo ya Korea Kusini imlipe dola milioni $30 pesa za Marekani.
Pele anadai kuwa Samsung imekuwa ikitumia mfano wake katika tangazo la runinga aina ya ultra high-definition katika jarida la New York Times bila idhini yake.
Mbrazil huyo mwenye umri wa mia 75 ambaye majina yake halisi ni Edson Arantes do Nascimento, aliwasilisha kesi hiyo katika mahakama ya Chicago Marekani
Pele anatambulika kama baba wa kizazi kipya cha wasakataji kabumbu anafahamika kote duniani kwa ustadi wake wa kucheza mpira.
Aliongoza timu ya Brazil iliyotwaa kombe la dunia la mwaka wa 1958 na 1970.
Aidha Pele alichezea timu iliyotawala kombe la dunia mwaka wa 1962.
Umaarufu wake haukuishia tu katika ushindi wa kombe la dunia, la, Pele anakumbukwa kwa kuisaidia klabu yake ya Santos kutwaa ubingwa wa Copa Libertadores mara mbili mbali na kunyakua kombe la Intercontinental .
Baada ya kustaafu soka ya kimataifa Pele alihamia Marekani ambapo alijenga jina kama nembo ya mpira wa kandanda ligi ya taifa NASL ilipokuwa ikijaribu kupata umaarufu katika miaka ya 1970.
Yamkini Samsung walitumia mfano wake hata baada ya kuvunja majadiliano naye mwaka wa 2013 walipokuwa wamemtaka awape ruhusa ya kutumia mfano wake kuuza runinga zao.
Nyota huyo sasa anatumia sura yake kunadi bidhaa mbali mbali na pia kushiriki maonesho kadha kujichumia mkate wake wa kila siku.
No comments:
Post a Comment