Umoja wa Mataifa umesisitiza juu ya ushiriki zaidi wa wanawake barani Afrika katika masuala ya kijamii na kisiasa kwa shabaha ya kuleta amani na uthabiti barani humo.
Phumzile Mlambo-Ngcuka, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake amesema katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa cha umoja huo siku ya Jumatatu ya jana kwamba, jamii ya kimataifa hususan nchi za Kiafrika zinapaswa kuwaunga mkono zaidi wanawake na kuipa umuhimu nafasi yao chanya katika jamii. Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amebainisha kwamba, wanawake wana nafasi muhimu katika kuleta amani na uthabiti barani Afrika, licha ya kuwa nafasi yao imekuwa ikipuuzwa na kutozingatiwa kama inavyotakiwa. Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema kuwa, kuanzishwa vituo vya kukabiliana na migogoro kwa kushirikishwa wanawake lengo likiwa ni kusimamia chaguzi au kutabiri migogoro ya ndani katika nchi za Kiafrika ni jambo ambalo daima limekuwa na mafanikio. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake ameongeza kuwa, mazungumzo na viongozi wa vyama vya kisiasa au maafisa usalama katika nchi zenye migogoro, hadi sasa yamekuwa na mafanikio.
Mkurugenzi Mtendaji huyo anaeleza hayo katika hali ambayo, wanawake walioko katika maeneo mbalimbali barani Afrika wamekuwa wakipitia tajiriba tofauti. Nafasi ya wanawake katika baadhi ya nchi za Kiafrika ambazo zimepiga hatua kubwa katika uga wa ustawi wa kisiasa na kiuchumi, nayo imebadilika mno na akthari yao wameingia katika harakati za kiuchumi na kisiasa. Katika baadhi ya nchi za Kiafrika kiwango cha ushiriki wa wanawake katika masuala ya kisiasa kimeongezeka mno. Wengi wa wanawake hao ni mawaziri au washauri katika serikali na vyama vya kisiasa huku wengine wengi wakishiriki katika harakti mbalimbali kwenye asasi zisizo za kiserikali hususan katika kuwasaidia watoto, vitengo vya elimu na katika vituo vya afya. Kadhalika katika akthari ya nchi barani Afrika kutokana na mwenendo wa kiuchumi kupiga hatua, wanawake wengi wameingia katika uwanja huo kama nguvu kazi na kuwa na nafasi muhimu katika kudhamini mahitaji ya familia. Pamoja na hayo wanawake barani Afrika wangali wanakabiliwa na matatizo mengi. Kustawi utamaduni katika baadhi ya nchi barani Afrika, kumeshuhudia wanawake katika nchi hizo wakikabiliwa na dhulma na wengi wao wamekuwa wakinyimwa hata haki zao za kimsingi kabisa.
Filihali, kuna nchi nyingi barani Afrika ambazo zinakabiliwa na mapigano ya ndani ya kikabila na kidini. Machafuko yameyafanya mazingira ya maisha ya wakazi wake hususan wanawake na watoto kuwa mabaya mno. Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati ni baadhi tu ya nchi hizo. Katika nchi ambazo kuna vurugu na machafuko wanawake na watoto wamekuwa wakikabiliwa na hali mbaya ya kimwili na kiroho na kukosa huduma muhimu. Pamoja na matatizo yote hayo, lakini katika miongo ya hivi karibuni kuna wanawake ambao wamefanikiwa kubadilisha mazingira yanayowakabili na hivyo kuwa na nafasi muhimu katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi katika nchi husika. Hivi sasa wanaharakati wengi na asasi za kimataifa zina matumaini kwamba, katika miaka ijayo ushiriki amilifu wa wanawake katika nyuga za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni barani Afrika utakuwa na taathira chanya katika kupatiwa haki zao na kuondolewa dhulma na uonevu dhidi yao barani Afrika na kwa muktadha huo kuwaandalia mustakbali mzuri wanawake hao.
No comments:
Post a Comment