Showing posts with label MAKALA. Show all posts
Showing posts with label MAKALA. Show all posts

Tuesday, April 5, 2016

Mradi wa pamoja waleta nuru vita dhidi ya GBV-Kenya


UN Women/Video capture
Nchini Kenya wadau mbali mbali wanashirikiana katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia, GBV kupitia programu ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake Jowege.
Programu ya pamoja kati ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Kenya. Lengo la programu hiyo ni kuimarisha uwezo wa wahusika ili kuweza kukabiliana na kuzuia ukatili wa kijinsia.
Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu, UNFPA moja ya wadau wanaoendesha miradi mbali mbali nchini Kenya, ukatili wa kijinsia unaweza chukua mfumo wowote ikiwemo, ubakaji, ukatili wa kijinsia au wa kimwili na unaweza lenga mtu wa jinsia yeyote ikiwemo wanaume.
Kenya ni moja ya nchi ambazo zinakabiliwa na tatizo hili. Je ni mikakati ipi ambayo Umoja wa Mataifa na wadau ikiwemo Shirika la Uhamiaji duniani IOM kwa kushirikiana na serikali wamechukua? Basi ungana na Grace Kaneiya katika makala hii.

Sunday, March 27, 2016

Zanzibar kwanza, vyama baadaye


BAADA ya kuapishwa kuongoza tena Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, juzi alimwapisha Said Hassan Said kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Hatua hii inaonesha kwamba baada ya kumalizika kwa uchaguzi, Dk Shein ameanza kuunda timu yake itakayowaongoza Wazanzibari katika kipindi kingine cha miaka mitano ambacho kikatiba ni cha mwisho cha uongozi wake.
Matumaini ya wengi ni kwamba Dk Shein ataunda serikali ya Umoja wa Kitaifa, kwani hilo alilizungumza mara kadhaa wakati wa kampeni mwaka jana. Ingawa katika uchaguzi wa marudio hakuna chama cha upinzani kilichofikisha asilimia 10 au kupata angalau mwakilishi ili kukidhi matakwa ya kikatiba, bado Shein anaweza kutumia madaraka yake ya kuchagua wawakilishi kutoka upinzani na hivyo kuweza kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Katiba inamruhusu Rais Shein kuchagua wawakilishi 10. Hata hivyo, la muhimu zaidi ni Wazanzibari kumuunga mkono katika harakati zake za kuijenga Zanzibar ikiwa ni pamoja na kudumisha amani huku wakizingatia kwamba ni yeye Shein aliyeridhia na kutekeleza uundaji wa serikali ya umoja wa kitaifa, baada ya asilimia 66 ya Wazanzibari kutaka uwepo wa serikali hiyo.
Wazanzibari wakumbuke pia kwamba amani ya Taifa lolote lile ni nyenzo muhimu ya maendeleo na ni hatari kuruhusu amani iliyopo iharibike. Kwa vile chama chochote cha siasa kinaanzishwa lengo kuu likiwa ni kuwatumikia wananchi kwa kutatua changamoto za maisha yao, ni vyema vyama vya siasa vikiwemo vilivyosusia uchaguzi wa marudio vikajikita katika kusaidia utatuzi wa hali ngumu ya maisha ya Wazanzibari kwa kujenga hoja na kutoa njia mbadala na sio kuwagawa watu kwa kuwapandikiza chuki.
Baada ya Wazanzibari kuondoka katika siasa za chuki pale ilipoundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2010, bado sisi tunaamini kwamba mwanasiasa halisi ni yule anayewahurumia watu wake na si yule anayejinasibu kuivuruga amani na kupania kuifanya serikali iliyoko madarakani ishindwe kutekeleza majukumu yake.
Chama chochote makini cha siasa sharti kitambue kuwa amani hii iliyopo ndio kinafanya siasa na si vinginevyo. Zanzibar kwa muda mrefu imekuwa ikijulikana duniani kote kwa ukarimu, kuvumiliana na upendo wa watu wake. Tunu hii inapaswa kutunzwa na kila mwenye akili timamu.
Ni vyema sasa Wazanzibari wakasema yaliyopita si ndwele na hivyo wakaanza kuganga yaliyopo na yajayo kwa kuhakikisha hawarudi kwenye chuki za kisiasa. Ni kwa mantiki hiyo, tunaviasa vyama vilivyosusa uchaguzi sasa kuona namna vinavyoweza kushirikiana na Dk Shein katika kuijenga Zanzibar na siyo kuibomoa.
Ni vyema kila Mzanzibari akakataa kutumiwa, akaweka mbele maslahi mapana ya taifa lake, mintarafu suala zima la amani, upendo na utulivu. Iwe ni Zanzibar kwanza, siasa za vyama baadaye.

Uhakiki wa silaha uwe nchi nzima


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda hivi karibuni alitoa siku 90 kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam wanaomiliki silaha kuzihakiki. Uhakiki huo unaofanywa na Jeshi la Polisi nchini umelenga kubaini wale wanaomiliki silaha hizo kihalali na pia kuona kama hazitumiwi katika matukio ya kihalifu licha ya kumilikiwa kihalali.
Katika kutilia mkazo agizo hilo, raia namba moja wa nchi hii, Rais John Magufuli, alijitokeza na kuhakiki silaha zake mbili; Bastola moja na Shot gun. Rais Magufuli alifanya hivyo akiwa nyumbani kwake na alifanya uhakiki huo mbele ya Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro.
Rais alikuwa mtu wa kwanza kuitikia agizo la kuhakiki silaha lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa wakazi wote wa jiji hilo. Makonda aliwataka wamiliki wa silaha kwenda kwa Wakuu wa Polisi Wilaya kuhakiki taarifa za silaha zote wanazomiliki kihalali au kusalimisha zile zilizopatikana kwa njia zisizotambulika.
Mbali na Rais Magufuli kuhakiki silaha zake anazomiliki, pia alitoa mwito kwa wananchi wote kuhakiki silaha zao. Ni wazi sasa zoezi hili la kuhakiki silaha siyo tu kwa jiji la Dar es Salaam bali sasa ni la nchi nzima maana tayari Rais ameshiriki na kuagiza watu wote wafanye hivyo.
Ingawaje sijasikia viongozi wengine waliofuata nyayo hizo za Rais hata Mkuu mwenyewe wa Mkoa wa Dar es Salaam labda hana silaha anayomiliki, lakini ni ngumu kuamini kuwa katika baraza zima la mawaziri hakuna anayemiliki silaha.
Hivi kweli hata wabunge wetu nao hakuna anayemiliki silaha, au wao hawapendi kufanya hivyo kupitia vyombo vya habari kama alivyofanya Rais ili kuhamasisha wengine. Hofu yangu ni kwamba kama zoezi hili halitafanyika nchi nzima, wenye nia ovu ya kuficha silaha zao wanaweza kujisogeza mikoa jirani na kujificha huko hadi hali itakapokuwa shwari baada ya vuguvugu la agizo hilo kupoa.
Wakuu wa mikoa na makamanda wa Polisi mikoa na wilaya ni vyema sasa wakawahimiza wananchi kufanya uhakiki huo nchi nzima ili kutokomeza kabisa uhalifu wa kutumia silaha kama si kupunguza.
Aidha uhakiki huu ukifanyika kwa umakini na utaalamu wa kutosha utaweza kabisa kulisaidia Jeshi la Polisi kuondokana na aibu ambayo Rais amekuwa akiisema mara kwa mara juu ya askari kuporwa silaha.
Natoa rai kwa wananchi nchi nzima kufanya uhakiki huo wa silaha ili kujiondoa katika usumbufu wowote ambao unaweza kujitokeza pindi ikijulikana kuwa unamiliki silaha ya moto lakini hujaihakiki.
Ni wazi baada ya hizo siku 90 kumalizika patakuwa na msako mkali wa kuwapata wamiliki wa silaha ambao hawajazihakiki. Hakuna maana ya kupotezewa wakati kwa kushurutishwa utekelezaji wa amri hiyo halali ya viongozi wetu akiwamo Rais ambaye anatamani siku moja nchi hii iwe na amani na utulivu kwa maana ya kutokuwa kabisa na matukio ya ujambazi wa kutumia silaha.
Na pia ni muhimu sana kwa wananchi kuwafichua wanaomiliki silaha isivyo halali kwa kuwa tunaishi nao mitaani. Lakini hili la kuhakiki silaha ni vyema pia likaendana na kampeni ya kutokomeza vikundi vya wizi na uporaji kama panya road ambavyo vinaelezwa kuwepo katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam na kutishia amani ya wananchi. Kimsingi, usalama utarejea nchini mwetu kama kila mwananchi atatoa ushirikiano wa kufichua waovu katika jamii kwa kuwa tunaishi nao mitaani.

Ongezeko la baa Mbeya na biashara ya ngono



BIASHARA ya vileo inazidi kushamiri siku hadi siku mkoani Mbeya kama ilivyo kwa maeneo mengine nchini. Kushamiri kwa biashara hiyo kunaenda sambamba na ubunifu wa wamiliki wa maeneo hayo ya burudani ili kuvutia wateja.
Maeneo ya Mwanjelwa, Kabwe, Soweto, Ilomba na Sae yaliyopo pembezoni mwa barabara kuu ni miongoni mwa sehemu zenye baa nyingi. Ingawa mkoa wa Mbeya una makanisa mengi wingi wa nyumba hizo za ibada haujawa kikwazo cha ongezeko la baa mkoani humo. Inadaiwa kwamba uwepo wa maeneo mengi ya kuuza mvinyo ni matokeo ya jiji la Mbeya kupata wageni wengi na kipato kizuri cha wakazi wake.
Kuna watu wengi wanaokwenda Mbeya wakitoka mikoa mbalimbali nchini, nchi jirani za Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Wageni wengi wanaokuja Mbeya ni wafanyabiashara wanaopeleka bidhaa kutoka makwao au kwenda kuchukua zinazozalishwa mkoani humo yakiwemo mazao ya chakula na biashara.
Mazao hayo ni pamoja na ndizi, mahindi, kokoa, mpunga na kahawa. Kuna wanaoamini kwamba, uwepo wa maeneo mengi ya starehe ni dalili za kukua kwa uchumi wa eneo husika. Wingi wa maeneo hayo umesababisha kukua kwa ushindani hivyo wamiliki wa huduma mbalimbali vikiwemo vileo wanajitahidi kuwa wabunifu kupata wateja.
Kuwa na wahudumu warembo katika mabaa ni moja kati ya ubunifu huo. Wafanyabiashara wa vileo wanasema, wahudumu warembo wanashawishi wateja kwenda walipo hivyo mauzo yanaongezeka. “Usione watu wanajaa namna hii ukajiuliza maswali mengi.
Ni kweli wengine wanaweza kusema umetumia kizizi na wengine wakasema umeboresha mazingira yako vizuri. Lakini ukweli ni kwamba siku mabinti hawa wakipungua na mauzo yanapungua pia,” anasema mmoja wa wafanyabiashara ya vileo katika maeneo ya Mwanjelwa. Inadaiwa kuwa wahudumu wengi wanafuatwa mbali na maeneo wanapofanya kazi ili kuepuka usumbufu zikiwemo ruhusa za mara kwa mara na kurubuniwa.
Kuna taarifa zinazodai kuwa, wateja kwenye maeneo hayo hawavutiwi na namna tu wanavyohudumiwa na warembo ila pia kuna cha ziada wanachokipata kwa wanawake hao, ikiwemo huduma ya ngono. Kuna madai kwamba, wahudumu wengi wa baa wanafanya biashara ya ngono na kwamba, wateja wao wakubwa ni wanaokwenda kunywa kwenye maeneo hayo.
Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Community Media Organization (Tacomo), linasema limefanya uchunguzi na kubaini hali mbaya kwa kuwa wahudumu wa kike wanafanya pia biashara ya ngono na wakati mwingi katika mazingira hatarishi. Mkurugenzi wa Tacomo, Gordon Kalulunga, anasema kuna tatizo la wasichana wanaofanya kazi kwenye baa kufanyiwa ukatili wa kingono na kwamba, chanzo cha ukatili huo na waajiri wao.
Kwa mujibu wa shirika hilo, wanawake hao wapo hatarini lakini hawatoi taarifa kwa hofu ya kufukuzwa kazi na usalama wa maisha yao. “Waajiri wakiwemo wamiliki wa baa na mameneja wamekuwa wakiwalazimisha wahudumu kufanya nao ngono kabla ya kuwapa ajira hizo. Lakini hata mara baada ya kuwaajiri huwalazimisha kufanya ngono na wateja wa baa hizo kwa makubaliano ya wateja hao kulipia kati ya shilingi elfu tano hadi elfu kumi kwa siku, fedha iliyopewa jina maarufu la malipo ya kaunta.
Malipo haya hayamhusishi binti anayekwenda kutumikishwa katika ngono bali itategemeana huruma ya mtu aliyekwenda naye akiamua kumlipa sawa na asipotaka pia haya,” anasema Kalulunga. “Kibaya zaidi ni kwamba tumebaini uwepo wa biashara ya binadamu ambapo kuna wahudumu wamekuwa mawakala wa kuwanunua wenzao mikoani kwa kuwalaghai kuwa waje Mbeya kufanya kazi za hoteli na kulipwa fedha nyingi, ahadi ambayo haitimii kwani wakifika hapa wanaishia kutumikishwa kingono kwenye baa wanazoajiriwa,” anasema.
Anaitaja mikoa ambako wasichana wengi wanatoka na kwenda Mbeya kutumikishwa kingono kuwa ni pamoja Singida, Iringa, Njombe na Ruvuma. “Mkoa wa Singida unaongoza katika jambo hili. Tulichobaini ni kuwa wengi wanadanganywa kwa kuahidiwa mambo makubwa wakiwa makwao. Ndiyo sababu utakutana na mabinti wadogo wanaotoka kwenye mkoa huo wakifanya kazi za uhudumu katika baa za hapa mjini. Wapo pia wanaokuja hapa baada ya kutoroka mashuleni.
“Ukweli wanapofika hawakutani na yale walioahidiwa wakiwa nyumbani. Hujikuta wametumbukia kwenye hatari ya ulevi na ukahaba kwa kulazimishwa na waajiri wao,” anasema Kalulunga. “Wanajikuta kuhiari utumwa wa kuuzwa kwa kuwa wanapofika hupewa chumba kimoja kwa ajili ya kulala na kuhifadhi vitu vyao kama nguo. Haijalishi wako wengi kiasi gani. Wengine hupewa godoro na kitanda kimoja ili walale hapo.
Wao huviita vyumba hivi gheto. Siku pekee ambayo binti anaona analala vizuri ni pale anapobebwa na mwanaume kwenda kufanya naye ngono kwa kuwa watalala wawili tofauti na gheto anajiona mwenye bahati. Huenda pia akala chakula kizuri zaidi ya wanachokula wenzie ghetoni,” anasema Kalulunga. Anasema Tacomo wameandaa mafunzo kwa wahudumu waweze kujitambua ili wasiwe waoga wa kutoa taarifa.
Anawaomba wadau kuona umuhimu wa kushiriki katika mpango huo na anavitaja vyombo vya habari kuwa ni mhimili muhimu utakaowezesha kuikomboa jamii ya wahudumu wa baa. Anatoa mwito kwa wahudumu wa kike kwenye baa mkoani Mbeya wajitokeze kwenye vyombo vya habari na vya sheria watoe malalamiko ya ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa, hasa kulazimishwa kutoa rushwa za ngono ili kuajiriwa.
Kuhusu hatari ya kuambukizana maradhi, Kalulunga anasema mara nyingi wawili hao, mwanaume na mhudumu wa baa huwa wamelewa na hivyo wanapofikia uamuzi wa kwenda kufanya ngono uhakika wa kutumia kinga inavyostahili huwa mdogo. Katika mahojiano wakati wa kuandika makala haya, mhudumu mmoja wa baa aliyejitambulisha kwa jina moja la Jasmini alisema: “Kama tunajikuta tumebeba mimba kutokana na wanaume haohao tunaolewa nao, si rahisi kukwepa magonjwa ya zinaa.
Upo uwezekano mkubwa wa kupata pia maambukizi kwa kuwa wakati mwingine tunakosa namna ya kujitetea hasa pale mwanaume anapokuwa amekulipia kaunta na umekunywa bia zake.” “Inafikia wakati yule anayepata wanaume wengi anaonekana mwenye bahati zaidi ya wengine. Atakula vizuri, atavaa vizuri, atasuka vizuri na atapendeza zaidi hata tunapokuwa tumeingia kazini.
Anakuwa amejitengenezea mtaji mzuri wa kupata mwanaume mwingine aliye na fedha nyingi. Hivyo unapoanza shughuli hii kwa kumpata mwanaume mwenye nazo pesa unakuwa umejipatia mtaji mzuri sana,” anasema msichana huyo.