Showing posts with label MASUALA YA KIJAMII. Show all posts
Showing posts with label MASUALA YA KIJAMII. Show all posts

Friday, May 20, 2016

Unamjua mdudu mwenye uwezo wa kupaa kilomita 6000?

Utafiti uliofanywa na kituo kinachohusika na kufuatilia wadudu wanaohama sehemu moja kwenda nyingine kilichoko Marekani kimegundua kwamba Kurumbiza au Dragonfly anauwezo mkubwa wa kuruka kupitia baharini kilomita 6000
Dragonfly pia ni Kati ya wadudu walioko hatarini kutoweka duniani
Dragonfly pia ni Kati ya wadudu walioko hatarini kutoweka duniani
Sijui kama umeshapata kusikia mdudu anayeitwa kurumbiza au kereng'ende? Huyu ni aina ya mdudu ambaye ni maarufu sana aakiwa na uwezo wa kuruka au kupaa kilomita nyingi. Inatajwa kwamba kurumbiza katika kipindi cha uhai wao wanaweza kupaa kwa takriban kilomita 6,000 kwenda na kurudi. Utafiti uliofanywa na kituo kinachohusika na kufuatilia wadudu wanaohama sehemu moja kwenda nyingine kilichoko Marekani baada ya kuwachunguza wadudu hao kutoka nchi sita za mabara tafauti, umegundua kwamba vinasaba vya wadudu hawa licha ya kutokea umbali mkubwa havitofautiani kwa kiasi kikubwa.
Kurumbiza au Dragonfly
Kurumbiza au Dragonfly
Na kwa maana hii wadudu hawa kutokana na uwezo wao wa kuzunguka masafa marefu sana duniani wanakuwa na umoja na ukaribu sana kama familia, linasema shirika la Plos One katika utafiti huo. Inasemekana kurumbiza hutoka India kila mwaka na kufanya ziara hadi Afrika na katika safari hiyo hawatumii njia ya ardhi bali wanavuka Bahari ya Maldives na Bahari ya Hindi.

Friday, May 13, 2016

WHO: Asilimia 80 ya wakaazi wa mijini wanavuta hewa chafu


Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) imeonya kuwa hali ya uchafuzi wa hewa inazidi kuwa mbaya duniani kote huku zaidi ya asilimia 80 ya wakaazi wa miji mikubwa wakivuta hewa chafu na kuongeza hatari ya kupatwa na saratani ya mapafu na maradhi mengine hatari.
Ripoti hiyo ya WHO imebainisha kuwa wakaazi wa mijini katika nchi masikini ndio wanaoathiriwa zaidi na kufafanua kwamba ni asilimia mbili tu ya miji katika nchi za kipato cha chini na cha kati ambayo watu wake wanavuta hewa inayokidhi viwango vya shirika hilo la kimataifa la afya. Kiwango hicho ni asilimia 44 katika miji ya nchi tajiri.
Ripoti ya Shirika Afya Duniani imezingatia utafiti iliofanya katika miji 795 ya nchi 67 katika kipindi cha kati ya mwaka 2008 hadi 2015.
Kwa kuzingatia kiwango cha mada zenye madhara kama sulfeti na kaboni nyeusi, WHO imegundua kuwa hewa inachafuka zaidi katika maeneo ya nchi zinazoendelea hususan katika Mashariki ya Kati na Kusini Mashariki mwa Asia.
Utafiti huo wa shirika la Afya Duniani umeonesha kuwa India ina miji 15 kati ya 30 duniani yenye hewa chafu zaidi.
Mji wa Zabol ulioko mashariki mwa Iran ndio wenye hewa chafu zaidi ukifuatiwa na miji ya Gwalior na Allahabad ya India na Riyadh na Jubail ya Saudi Arabia.../

Papa aruhusu mjadala wa wanawake mashemasi

Papa aliahidi kubuni tume kutafiti na kujadili uwezekano huo wa kuwezesha wanawake kuhudumu katika ngazi hiyo ambayo ni daraja moja tu chini ya makasisi. Wanahistoria wanasema zamani wanawake walihudumu kama mashemasi.
Papa Francis akiwa Vatican. Papa Francis akiwa Vatican.
Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, amesema ataunda tume itakayochunguza na kujadili uwezekano wa wanawake kuteuliwa kuwa mashemasi katika Kanisa hilo katika pendekezo linaloashiria uwazi wa kuruhusu wanawake kuteuliwa kuhudumu katika nafasi ambazo zimekuwa za wanaume pekee. Wazo hilo tayari limeanza kuibua hisia mbalimbali.
Ni katika mkutano wake maalum na waumini wanawake 900 waliojumuika Vatican ambapo katika awamu ya maswali, suala hilo likaibuka. Papa aliulizwa ikiwa atakuwa radhi kuruhusu utafiti kufanywa kuhusu uwezekano wa wanawake kuwa mashemasi, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za sheria za kanisa hilo. Papa aliahidi kubuni tume kutafiti na kujadili uwezekano huo wa kuwezesha wanawake kuhudumu katika ngazi hiyo ambayo ni daraja moja tu chini ya makasisi. Wanahistoria wanasema zamani wanawake walihudumu kama mashemasi.
Robert Gahl ambaye pia ni kasisi na pia profesa wa maadili katika chuo kikuu cha kikatoliki Pontifical University of the Holy Cross anasema "Kile ambacho Papa anatafakari ni uchunguzi wa kihistoria kuhusu majukumu ambayo mashemasi wanawake walikuwa wakifanya, na kufikiria kuyazingatia ili kuwezesha wanawake katika njia moja ya ushemasi. Hata hivyo tutarajie kuwa papa hatahimiza kitu kama hicho kwa sababu tayari ameshasema hataki wanawake kuwa makasisi. Analotaka ni kuwezesha wanawake katika jamii".
Wanawake waunga mkono
Wanawake kanisani maarufu Sisters. Wanawake kanisani maarufu Sisters.
Kauli ya Papa ilipokelewa vema na baraza la kutawaza wanawake WOC, shirika la Marekani linalohimiza kanisa katoliki kuanza kutea na kutawaza wanawake katika ngazi zote za huduma kanisani ikiwemo ukasisi. Papa Francis ameonekana mara kwa mara akihimiza usawa wa kijinsia. Kate Mc Elwee ambaye ni mkurugenzi wa baraza la uteuzi wa wanawake, ni kati ya wale ambao wamesifia kauli ya Papa kwa kukubali mjadala huo ufanywe. Amesema "Ninafikiria kuwa Papa kweli anataka swali hilo lijadiliwe. Maandiko yetu wenyewe na wahubiri wametuambia kuwa wanawake sawa na wanaume wamekuwa mashemasi tangu zamani, kwa hivyo ninafikiria tume itaunga mkono historian a itakuwa bora ikiwa Vatican itakubaliana na hilo"
Mashemasi hutawazwa kuwa wahudumu tu wa kanisa lakini si makasisi. Japo wanaweza kutekeleza majukumu mengineyo yanayofanywa na makasisi, kama vile kuongoza sherehe za harusi, ubatizo na hata kuhubiri, hawawezi kuongoza misa ya Pasaka.
Kadhalika amerudia mara kwa mara kuwa hataki kuwakilisha mafunzo yote ya kanisa kana kwamba yameandikwa kwenye jiwe. Amejaribu kufanya kanisa kuwa na uelawa na kutofanya maamuzi dhidi ya waliotalikiana, wanaowekeana kimada na waumini ambao ni wapenzi wa jinsia moja

Friday, April 29, 2016

WAKATAZWA KUTUMIA MITANDAO YA KIJAMII NDIVYO SIVYO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sihaba Nkinga alisema hayo wakati akifungua mkutano wa tatu wa Kamati Kuu ya Baraza la Watoto Tanzania.

Aidha Nkinga aliwataka watoto kuhakikisha wanatimiza wajibu wao na kuacha kulalamikia haki bila kutimiza wajibu.

Alisema ushiriki wa watoto ni moja ya haki tano za msingi kwa watoto wote, bila kujali tofauti zao na serikali inalipa suala la ushiriki wa watoto umuhimu wa kipekee katika mipango ya maendeleo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya watoto kutoka Wizara hiyo, Magret Mussai alisema, mkutano huo wa Baraza la Watoto ni muhimu na utawasaidia watoto kuangalia mambo yao ikiwemo kuangalia mikakati wa taifa ya ushirikishwaji wa watoto katika mambo mbalimbali.

Monday, April 4, 2016

Wafanyakazi wa majumbani wana haki ya kupumzika- ILO




Wafanyakazi wa ndani bado hawana haki ya kupumzika. (Picha:© UN Women/Pornvit Visitoran)
Shirika la kazi duniani, ILO limesema zaidi ya nusu ya wafanyakazi wa majumbani kote ulimwenguni bado wanakosa haki ya msingi ya binadamu ya kupumzika kutokana na kukosa ukomo wa saa za kazi siyo tu kwa siku bali kwa wiki. Flora Nducha na ripoti kamili.
(Taarifa ya Flora)
Katika kichapisho chake, ILO imesema , ukosefu wa haki hiyo ya kisheria unaweka katika kiza cha mazingira magumu ya kazi hususan wale wanaoishi na waajiri wao wakifanya kazi kwa zaidi ya saa 60 kwa wiki wengine wakiamshwa hata nyakati za usiku.
ILO inasema madhara ya kufanya kazi bila kupumzika ni pamoja na magonjwa kama vile kisukari aina ya Pili, moyo na msongo wa mawazo ambapo imesema wafanyakazi wa majumbani wanatakiwa kupumzika saa 11 kwa siku.
Philippe Marcadent mkuu wa kitengo cha mazingira ya kazi ILO amesema bado kuna mkwamo kuzingatia haki hiyo kwa kuwa kazi inafanyika majumbani licha ya kwamba mkataba wa kimataifa wa  wafanyakazi wa majumbani ibara ya 189 umetaja kupumzika kama haki ya msingi.
Hata hivyo nchi kama Chile zimepongezwa kwa kuzingatia mkataba huo ikiwemo wafanyakazi wa ndani kupumzika saa 11 kwa siku huku jumamosi na jumapili wakiwa mapumziko.

Thursday, March 31, 2016

Nchini Madagascar, utumwa bado huwakumba watoto

Nchini Madagascar. Picha kutoka akaunti ya Twitter ya ILO.
Bado zaidi ya asilimia 25 ya watoto wenye umri wa kati ya miaka mitano na 17 wanatumikishwa nchini Madagascar, hasa kwenye kazi za nyumbani, limesema Shirika la Kazi duniani ILO.
Tatizo hilo linakumba zaidi maeneo ya vijijini ambapo kwa mujibu wa ILO, asilimia 44 ya watoto wanaotumikishwa hivyo wameajiriwa wakiwa na umri wa kati ya miaka 10 na 12.
ILO imeongeza kwamba mshahara wao wastan ni dola 12 kwa mwezi, ukiwa chini sana ikilinganishwa na mshahara wa chini wa kitaifa ambao ni dola 66 kwa mwezi, wengi wao wakitumikishwa kwa saa zaidi ya 12 kila siku, kinyume na sheria ya kazi ya kitaifa, na wakikosa huduma za msingi za elimu.
Kwa ushirikiano na serikali ya Madagascar ambayo imeunda mpango kazi wa kitaifa mwaka 2004, ILO inafadhili miradi ya kusaidia watoto hawa kuokolewa, kupewa fursa mpya ya kusoma na kuwezesha familia zao kujiendeleza kiuchumi.

Mume amkata mke mikono na masikio Uganda


Kisa cha mwanamume mmoja nchini Uganda kumkata mkewe mikono na masikio kimezusha hisia mseto za hasira na huzuni kuhusu visa vya ukatili majumbani hasa dhidi ya wanawake.
Ninsiima akiuguza najeraha katika hospitali kuu ya Mulago baada ya kukatwa na muwe wake.
Ninsiima akiuguza najeraha katika hospitali kuu ya Mulago baada ya kukatwa na muwe wake.
Kitendo hicho kilitokana na hatua ya mwanamke huyo Ninsiima Kabonesa ambaye kwa sasa ni mjamzito kupinga jaribio la mume wake kuuza mavuno yake ya mahindi akihisi kwamba atampunja ili hali hakuchangia chochote katika uzalishaji wake.
Chanzo cha ugomvi huo kilikuwa ni gunia 100 za mahindi aliyovuna Kabonesa kwa jasho lake mwenyewe bila mume wake kuchangia chochote. "Mwanamke huyo hukodi ardhi na kupanda zao atakalo," alisema jirani ya muathirika huyo Fatuma Nalwanga, ambaye ndiye anamhudumia kwa sasa hospitalini.
Nalwanga aliiambia DW kuwa msimu huu Kabonesa alipanda mahindi na kuvuna gunia 100. "Mume wake alijaribu kumshawishi wauze mahindi hayo Ninsiima akakataa akihisi kwamba atampunja pesa zake zote na mabishano yao yaliishia kupigana."
Ramani ya Uganda.
Ramani ya Uganda.
Vyanzo vya ukatili
Mara nyingi visa vya ukatili majumbani hutokea pale mume na mke wanapofanikiwa kuingiza mapato. Mazingira haya haya ndiyo yamempelekea Kabonesa kujikuta katika hali ya ulemavu wa milele na hali ngumu ya unyanyapaa atakamoishi akiwa mtegemezi.
Yamkini mume huyo alilenga kumuua mama watoto wake kwani alielekeza upanga aliotumia kumkata kwenye shingo. Ni katika kingakinga za Ninsiima kunusuru maisha yake ndipo alikatwa mikono na masikio.
"Mwanamke alifanya kila aliloweza kujikinga ndipo akakatwa mikono yote miwili, masikio pamoja na mgongo," alifafanua Nalwanga. Kisa hicho kimezusha hisia za hasira miongoni mwa wanaharakati wa haki za wanawake.
Polisi wanyooshewa kidole
Wakati polisi ikisema kuwa inamtafuta mume huyo, baadhi ya wanaharakati wa haki za wanawake wanahisi chombo hicho cha kisheria hakijadhihirisha jitihada hizo kwani wakati kisa hicho kilipotokea mume huyo alibaki huru hadi pale majirani wa familia hiyo walipolalamika.
"Nadhani polisi wanahitaji kufanya jitihada zaidi wamtie mbaroni mwanamume aliyemkata mikoni Niinsima. Mara nyingi washukiwa wa aina hii hawakamatwi na ndiyo maana visa hivyo vinaongezeka," alisema Tina Msuya, mkurugenzi wa kituo cha ushughulikiaji wa visa vya ukatili majumbani CEDOVIP.
Msemaji wa polisi Fred Enanga amesema jeshi hilo linamsaka bwana huyo lakini itakuwa vigumu kumpata kwani amezima simu zake zote.
Visa vya ukatili dhidi ya wanawake hutoteka mara nyingi kutokana na kipato.
Visa vya ukatili dhidi ya wanawake hutoteka mara nyingi kutokana na kipato.
Kujifungua akiwa mlemavu wa kudumu
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba katika muda wa miezi miwili hivi ijayo mama huyo mjamzito Ninsiima anataraji kujifungua na atakabiliwa na wakati mgumu kumlea mtoto wake. Hi ina maana kwamba maisha ya mtoto huyo yameathirika kabla ya kuzaliwa kwake.
"Katika muda wa miezi miwili Ninsiima hatakuwa amepona ili kumlea mtoto wake ipasavyo kisha atahitaji zaidi ya miaka miwili kujifunza jinsi ya kutumia sehemu zilizobaki za viungo vyake pamoja na kuishi katika hali hiyo ya ulemavu," alifafanua mkurugenzi wa CEDOVIP Tina Msuya.
Visa na ugomvi wa aina hii hutokea mara nyingi majumbani hasa msimu wa mavuno na wanajamii wana mtazamo kuwa pana haja kwa serikali na wadau wengine kuendesha elimu nasaha kuviepusha.