Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Afya
Duniani (WHO) imeonya kuwa hali ya uchafuzi wa hewa inazidi kuwa mbaya
duniani kote huku zaidi ya asilimia 80 ya wakaazi wa miji mikubwa
wakivuta hewa chafu na kuongeza hatari ya kupatwa na saratani ya mapafu
na maradhi mengine hatari.
Ripoti hiyo ya WHO imebainisha kuwa wakaazi wa mijini katika
nchi masikini ndio wanaoathiriwa zaidi na kufafanua kwamba ni asilimia
mbili tu ya miji katika nchi za kipato cha chini na cha kati ambayo watu
wake wanavuta hewa inayokidhi viwango vya shirika hilo la kimataifa la
afya. Kiwango hicho ni asilimia 44 katika miji ya nchi tajiri.
Ripoti ya Shirika Afya Duniani imezingatia utafiti iliofanya katika miji 795 ya nchi 67 katika kipindi cha kati ya mwaka 2008 hadi 2015.
Kwa kuzingatia kiwango cha mada zenye madhara kama sulfeti na kaboni nyeusi, WHO imegundua kuwa hewa inachafuka zaidi katika maeneo ya nchi zinazoendelea hususan katika Mashariki ya Kati na Kusini Mashariki mwa Asia.
Utafiti huo wa shirika la Afya Duniani umeonesha kuwa India ina miji 15 kati ya 30 duniani yenye hewa chafu zaidi.
Mji wa Zabol ulioko mashariki mwa Iran ndio wenye hewa chafu zaidi ukifuatiwa na miji ya Gwalior na Allahabad ya India na Riyadh na Jubail ya Saudi Arabia.../
No comments:
Post a Comment