Rais José Mário Vaz wa Guinea-Bissau amempiga kalamu Carlos Correia, Waziri Mkuu wa nchi hiyo na kutangaza kuivunja serikali.
Akilihutubia taifa jana Alkhamisi, Rais Vaz alisema serikali ya
Correia imeshindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa uliopo na
kubuni taasisi zinazoendana na matakwa ya utawala wake.
Rais José Mário Vaz wa Guinea-Bissau amevitaka vyama vya siasa kushauriana na kumteua Waziri Mkuu mpya.
Correia alipewa jukumu la kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika mwezi Oktoba mwaka jana, akiwa ni kiongozi wa tatu kushikilia wadhifa huo ndani ya muda wa miezi mitatu. Correia kama wenzake wawili waliomtangulia, alitazamiwa na utawala wa Rais Vaz kuupatia ufumbuzi mzozo wa kisiasa unaotokota nchini humo unaodaiwa kuripuka kuanzia ndani ya chama tawala cha PAIGC.
Mapema mwezi Machi mwaka huu, Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ulioitembelea nchi hiyo kwa ajili ya kuchunguza hali ya mambo, umeyasema hayo wakati wa mazungumzo na Rais wa Guinea-Bissau, José Mário Vaz, Spika wa Bunge na viongozi wa vyama vya kisiasa.
Mgogoro wa kisiasa nchini Guinea-Bissau umekuwa mkubwa kiasi cha kufanya upatanishi wa Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) na Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Lugha ya Kireno (CPLP) kushindwa kumaliza mivutano hiyo ya kisiasa.
No comments:
Post a Comment