Mkuu wa zamani wa Mkoa wa Kaskazini Pemba na mshauri wa Rais wa Zanzibar kisiwani humo, Dadi Faki Dadi amekamatwa akituhumiwa kufanya mapenzi na mtoto wake wa kambo.
Dadi alikamatwa juzi akidaiwa kukutwa na mtoto huyo wa mkewe wa ndoa mwenye umri wa miaka 21 katika nyumba ya kulala wageni inayoitwa Executive, jirani na makao makuu ya Uhamiaji Zanzibar katika eneo la Kilimani chini na Maisara, mjini Unguja.
Mwanasiasa huyo alijikuta akipigwa pingu na polisi akiwa kifua wazi mbele ya mkewe na wanafamilia na kisha kupelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Mwembemadema.
Picha za video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, zilimwonyesha Dadi akikabiliwa na mashambulizi makali ya maneno kutoka kwa watu waliomkamata, akiwamo mkewe.
“Mwacheni avae nguo kwanza, mpeleke bwana, twende bwana..." ni baadhi ya maneno yanayosikika katika video iliyorekodiwa wakati wa kumtia mbaroni.
Taarifa zilizopatikana miongoni mwa wanafamilia ya kiongozi huyo, zilidai kwamba alikamatwa baada ya kumtilia shaka binti huyo kutokana na mienendo yake ya hivi karibuni na kuamua kumfuatilia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam alithibitisha kumshikilia Dadi kwa muda kabla ya kumwachia kwa dhamana.
“Kijamii alitenda kosa, lakini sisi tunaendelea kufanya uchunguzi, iwapo tutabaini ametenda kosa la kisheria na anaweza kuwa mashtaka tutamkamata ili kumpeleka katika vyombo vya sheria,” alisema Mkadam.
Mmoja wa wanafamilia ambaye aliomba jina lake lisitajwe alisema:“Mwizi siku zake ni arobaini, tulimtega na hatimaye tumemnasa sasa tuone mwisho wake utakuwa nini na kipi kitajiri baadaye.”
No comments:
Post a Comment