Hatua hiyo inatajwa kwamba huenda ikasaidia kuyafufua mazungumzo ya amani na wapalestina hasa kwakuwa kiongozi wa Labour Herzog ni mwanasiasa anayeunga mkono kuwepo dola huru la wapalestina
Imeripotiwa kwamba kiongozi huyo wa chama cha mrengo wa kulia cha Likud Benjamin Netanyahu amekuwa akatika majadiliano ya kina na marefu na kiongozi wa Labour Isaac Herzog katika kipindi cha wiki kadhaa za hivi karibuni katika jitihada za kujaribu kutafuta mwafaka wa kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Herzog ambaye chama chake kinaunda kile kinachoitwa muungano wa kizayuni kikiwa pamoja na chama cha mrengo wa kati cha Hatnuah huenda kikayawakilisha mapendekezo ya makubaliano ya kuunda serikali ya mseto mbele ya chama chake katika siku kadhaa zijazo zimeeleza ripoti. Inatajwa kwamba kuingia serikalini kwa chama hicho kutaifanya Jumuiya ya Kimataifa kufuatilia kwa karibu kitakachotokana na hatua hiyo ambayo inaweza kuwa chachu ya kufufuliwa kwa mazungumzo ya amani na wapalestina.
Hezrog anaonekana kuwa mtu anayeweza kupewa jukumu la wizara ya mambo nje ambalo kwa hivi sasa linabebwa na Netanyahu katika ngazi fulani fulani juu ya kuwa ni waziri mkuu wa nchi hiyo. Jana rais wa Misri Abdel Fatah al sisi aliwatolea mwito waisraeli na wapalestina kuchukua hatua ya kihistoria kufikia amani kauli hii imetasiriwa na wadadisi wa masuala ya mashariki ya kati kwamba ni jaribio la kutaka kuipa nguvu fikra ya Herzog kujiunga na serikali.
Tayari gazeti la Jerusalem Post ambalo limenukuu ripoti zilizotolewa na maafisa kutoka pande zote kwenye mazungumzo limeandika kwamba ikiwa serikali ya Umoja wa Kitaifa itaundwa Netanyahu na Herzog huenda wakasafiri kenda Misri kuanzisha juhudi mpya za mazungumzo ya kutafuta amani na wapalestina chini ya usimamizi wa rais Abdul Fatah al sisi.
Hata hivyo mpango huo wa kuundwa serikali kati ya Likud na Labour ni suala linalokabiliwa na upinzani mkali kutoka pande zote mbili na wadadisi wanasema suala la kufikia makubaliano bado liko mbali sana.Mpinzani mkubwa wa Herzog ndani ya chama chake cha Labour,Shelly Yatchimovich amesema muungano huo utakuwa ni sawa na ndoa ya damu.
Kadhalika wengi wa wanachama wa Likud wanahisi ni bora kuunda serikali ya mseto na chama cha kizalendo cha Yisrael Baiteinu kuliko Labour.Ikumbukwe kwamba Muungano wa kizayuni uliundwa kuelekea uchaguzi wa mwaka 2015 kwa lengo la kumuondoa madarakani waziri mkuu Netanyahu lakini ulishindwa na kumfanya waziri mkuu huyo baadae kuunda serikali yenye msimamo mkali zaidi ya mrengo wa kulia ambayo haijapata kutokea katika historia ya Israel. Hata hivyo serikali ya muungano ya Netayahu ina wingi wa kiti kimoja tu katika bunge na anaweza tu kuwa na mafanikio endapo atakuwa na uungwaji mkono mkubwa na hasa kwakuwa muungano wa sasa hivi una uwezo wa kumzuia.
No comments:
Post a Comment