Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
anatazamiwa kukutana na ujumbe wa upinzani kusaka njia za kuukwamua
mkwamo wa kisiasa unaotishia kuyavunja makubaliano ya Disemba 31.
Hata hivyo, hakuna uhakika endapo upinzani utashiriki kwenye
mazungumzo hayo yaliyoitishwa wakati upinzani nao ukipanga mgomo wa nchi
nzima kumshinikiza Kabila kutekeleza kwa vitendo makubaliano hayo
yaliyosimamiwa na Kanisa Katoliki nchini Kongo.
Wakati huo huo,
mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, ametoa wito wa kupatikana
kwa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akitaka umwagaji
damu ukomeshwe mkoani Kasai.
"Taarifa za mapigano zinaendelea
kuwasili kutoka Kasai, ambayo yanapelekea wahanga wengi zaidi na
kuwakosesha watu makaazi yao," mkuu huyo wa Kanisa aliwaambia waumini
wapatao 2,000 katika mji wa Carpi ulio kaskazini mwa Italia, ambao
wenyewe ulikumbwa na matetemeko mawili makubwa ya ardhi mwaka 2012.
"Kila mmoja aombe ipatikane amani na kwamba nyoyo za wanaohusika na uhalifu huu zisibakie watumwa wa chuki na ghasia," alisema.
Watu
wapatao 400 wamekufa ndani ya kipindi cha miezi sita ya machafuko
ambayo yamesambaa kwenze majimbo ya Kasai-Central, Kasai, Kasai-West na
Lomami.
Papa Francis ataka kusitishwa kwa mauaji ya Kasanga, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mkoa
huu unakabiliwa na mapigano tangu vikosi vya serikali kumuuwa kiongozi
wa kimila na mkuu wa kundi moja la wanamgambo, Kamwina Nsapu, katikati
ya mwezi Agosti 2016. Nsapu anaripotiwa kuanzisha uasi dhidi ya serikali
kuu ya Rais Joseph Kabila mjini Kinshasa.
Siku ya Alhamis (30
Machi), viongozi wa kanisa na mwakilishi wa Papa Francis nchini Kongo
walivitaka vyombo vya usalama, ambavyo vinatuhumiwa kwa kuwatesa
wapinzani, kujizuia kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa operesheni zao.
Mwezi
uliopita, polisi iliwatuhumu waasi kwa kuwauwa maafisa 39 jimboni
Kasai, na wiki iliyopita miilki ya wahandisi wawili wa Umoja wa Mataifa
ilipatikana baada ya kutekwa nyara huko Kasai-Central.
Raia
wawili wa kigeni walitekwa na watu wasiojuilikana tarehe 12 Machi
sambamba na raia wengine wanne wa Kikongo waliokuwa wanawasindikiza.
Bensouda asema uhalifu wa kivita umetendeka DRC
Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda, anaamini kuna uhalifu dhidi ya ubinaadamu unatendeka nchini DRC.
Katika
hatua nyengine, mwendesha mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu
(ICC), Fatou Bensouda, amesema kuuawa kinyama kwa timu ya wataalamu ya
Umoja wa Mataifa na ghasia nyengine nchini Kongo kunaweza kuwa sawa na
uhalifu unaoweza kushitakiwa na mahakama yake.
Katika taarifa
yake ya Ijumaa, Bensouda alisema amesikitishwa sana ghasia kwenye jimbo
la Kasai. Miili ya raia wa Marekani, Michael Sharp, Msweden Zaida
Catalan, na mkalimani raia wa Kongo, Betu Tshintela, ilipatikana mapema
wiki hii.
Wataalamu hao walikuwa wakichunguza tuhuma za uvunjaji
wa haki za binaadamu uliofanywa na jeshi la Kongo na makundi ya
wanamgambo kwenye eneo hilo.
Watu wengine watatu kwenye timu
yao, bado hawajuilikani walipo, lakini Bensouda ameitaka serikali ya
Kinshasa kufanya uchunguzi wa kina na "wa hakika".
Kawaida, ICC
inaweza kutoa waraka wa kukamatwa kwa washukiwa, lakini ni juu ya taifa
mwanachama kuwakamata na kuwafikisha mahakamani kujibu mashitaka.