Sarakasi
za kisiasa zinaendelea kutawala ndani ya chama cha CUF baada ya Katibu
Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, kudai kuwa Profesa Ibrahim Lipumba
anatumiwa kukihujumu chama hicho.
Maalim
Seif alimtuhumu Profesa Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa CUF,
anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuwa
anakihujumu chama ili kishindwe kudai haki waliyoipata katika Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba 25 mwaka juzi.
Aliyasema
hayo jana katika kijiji cha Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja
alipozungumza na wanachama wa chama hicho, ikiwa ni ziara maalumu ya
uimarishaji wa chama katika mikoa yote ya Kisiwa cha Unguja.
Maalim
Seif alisema pamoja na Profesa Lipumba kupata nguvu kutoka vyombo vya
dola na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika kukihujumu chama
hicho, lakini hawataweza kufikia malengo hayo.
Alisema
taasisi hizo kwa pamoja zimekuwa zikimuunga mkono Lipumba kwa kumpa
kila nguvu anayohitaji ili kuona anafanikisha malengo ya CCM ya
kuitawala nchi bila ya kuwepo kwa chama kikuu pinzani, ila nguvu zao
hizo zitagonga mwamba.
“Nashangaa
sana kuona Lipumba amekubali kutumika na CCM kwa kukihujumu chama kwa
masilahi binafsi, lakini nataka muelewe wananchi kuwa pamoja na nguvu
zao zote hizo katu hawataweza kuwakatisha tamaa Wazanzibari ya kudai
haki yao waliyoipata katika uchaguzi uliopita,” alisema.
Alishangazwa
kuona Ofisi ya Msajili kwa kushirikiana na vyombo vya dola badala ya
kufuata Katiba na sheria za nchi, wao wamekuwa wakikihujumu chama hicho.
“Pamoja
na hujuma hizi zinazofanywa na Lipumba katika chama chetu, lakini
nashangaa Rais (John) Magufuli anatumbua watendaji wabovu, lakini humu
mrajisi (Msajili) wa Vyama vya Siasa anamuachia,” alisema.
Kuhusu
kuondolewa kwenye nafasi yake, Maalim Seif alisema kwa mujibu wa katiba
ya CUF, Lipumba hana uwezo wa kumvua nyadhifa hiyo hata kama angekuwa
ni mwenyekiti halali.
Alisema
kwa mujibu wa katiba yao ili Katibu avuliwe wadhifa wake lazima mkutano
mkuu uhudhuriwe na zaidi ya nusu ya idadi wajumbe.
Alisema
kikao kilichofanyika chini ya Profesa Lipumba kilihudhuriwa na wajumbe
wasiokuwa na ujumbe kihalali, ambao walipandikizwa kuonesha kama kikao
hicho kilikuwa halali.
“Ikiwa
mimi nimefukuzwa chama kutokana na madai kuwa sihudhurii vikao
vinavyofanywa na ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam, mbona yeye
Lipumba tangu mwaka 2015 hawajawahi kuja ofisi kuu ya chama ambayo ni
mtendeni hadi leo, kwa hiyo naye alitakiwa kufukuzwa,” alihoji.
Maalim
Seif alisema kuwa kinachosikitisha ni kuona Ofisi ya Msajili wa Vyama
vya Siasa nayo kuidhinisha kuwa wamekubaliana na mageuzi hayo
yaliyofanywa na Lipumba kwa kushirikiana na wajumbe wake.
“Ninachokifahamu
mimi ndani ya katiba yetu inasema kuwa ili uamuzi wa kuvuliwa nafasi ya
uongozi ni lazima anayedaiwa kufanya kosa aitwe na uongozi kujieleza,
lakini mimi sijaitwa kujieleza,” alihoji Maalim Seif.
Akizungumzia
madai ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliopita, Maalim Seif alisema
waliwataka wananchi wa Zanzibar kutokata tamaa na haki yao, huku akidai
hivi karibuni dola ya Zanzibar itakuwa chini ya CUF.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema uongozi wa CUF unasikitika kuona vyombo vya dola vikiingilia mamlaka ya chama hicho na kusahau wajibu wao.
Alisema
kuwa wajibu wa vyombo hivyo ni kusimamia amani ya wanachama na viongozi
wake, lakini ni jambo la kushangaza kwa viongozi wa vyombo hivyo kuwa
ni miongoni mwa wanaongoza kuonesha chuki dhidi ya CUF.
Alisema
pamoja na hujuma hizo, lakini viongozi wakuu wa chama hicho chini ya
Maalim Seif, hawatosita kudai haki yao hadi kieleweke.
Akijibu
tuhuma hizo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho bara na anayemuunga mkono
Profesa Lipumba, Magdalena Sakaya alimtuhumu Maalim Seif kuwa ndiye
anakula njama za kukidhoofisha chama.
Alisema
Seif amekataza ruzuku zisifike kwenye wilaya, hakuna mikutano na hakuna
hata pikipiki huku wenzao Chadema waliokuja juzi wamekuwa chama kikuu
cha upinzani kutokana na kuwa wamoja.
“Malalamiko anayotoa ajikite kwenye katiba, aichambue kifungu kwa kifungu atabaini anakosea wapi.
“Hii
ni taasisi ya chama, siyo kampuni ya mtu, lazima tufuate katiba
tuliyojiwekea ambayo ipo wazi inatoa maelekezo ya kila kitu,
anayekengeuka anafanya makusudi na sisi hatuwezi kukaa kimya bila
kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuteua watakaofanya kazi alizotakiwa
kufanya yeye,” alisema Sakaya.
Alieleza
kuwa badala ya kujenga chama, ameamua kukidhoofisha na anatumiwa
kufanya hivyo akijificha kwenye mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa).
“Amekuwa
bwana kesi, kila kukicha anafungua mpya, mimi nina kesi, Lipumba ana
kesi, Msajili wa Vyama ana kesi, mwanasheria ana kesi, akae kimya
asubiri ziishe, ”alisema Naibu katibu mkuu huyo.
No comments:
Post a Comment