Rais mpya wa mpito nchini Brazil Michel Temer ametoa wito wa umoja
nchini humo, wakati kiongozi aliyesitishiwa madaraka yake na baraza la
Seneti ameapa kupambana na kile alichokiita mapinduzi.
Mvutano huo wa madaraka nchini Brazil umeweka wazi mpasuko mkubwa wa
kisiasa katika taifa hilo la Amerika ya kusini lenye wakaazi wengi.Mitazamo hiyo inayokinzana imekuja saa chache tu katika jengo la makao ya rais baada ya baraza la seneti nchini Brazil kupiga kura 55 dhidi ya 22 jana Alhamis kumshitaki rais Dilma Rousseff, na kumuweka makamu wake wa rais Michel Temer madarakani.
Rousseff ambaye umaarufu wake umeporomoka huku kukiwa na mdororo mkubwa kabisa wa uchumi tangu miaka ya 1930, anashutumiwa kwa kutumia mbinu chafu za kimahesabu kuficha nakisi kubwa katika bajeti ya taifa ya Brazil.
Wapinzani wanadai kwamba hali hiyo imeiathiri nchi hiyo, lakini rais huyo mwanamke wa kwanza nchini Brazil ameiita kesi hiyo isiyo na msingi , iliyotengenezwa na wale wanaofahamika kama watu wenye nafasi za juu katika jamii ambao wana wasi wasi kwamba huenda chama chake cha mrengo wa kushoto cha wafanyakazi kinaweza kunyakua tena madaraka.
Baraza la mawaziri
Temer amechukua hatua za haraka kwa kutangaza baraza jipya la mawaziri na kusema umuhimu wa kwanza wa serikali yake ni kuufufua uchumi wa Brazil. Temer amesema.
"Neno langu la kwanza kwa Wabrazil ni neno uaminifu. Uaminifu katika maadili ambayo yanajenga hadhi ya mtu. Katika uimara wa demokrasia. Uaminifu katika kuufufua uchumi wa nchi yetu."
Pia ameahidi kuunga mkono uchunguzi mpana zaidi kuhusiana na rushwa na ufisadi katika kampuni la taifa la mafuta ambao tayari unawagusa wanasiasa maarufu kutoka vyama mbali mbali na hata kumgusa Temer binafsi.
Mamia ya waandamanaji waliingia mitaani katika mji wa Sao Paulo baada ya kura ya Seneti ya kumvua kwa muda madaraka yake rais Dilma Rousseff hatua inayosafisha njia rais huyo kushitakiwa kwa kuvunja sheria za bajeti.
Baadhi ya watu waliokuwa wakishangiria mjini Sao Paulo na miji mingine walijifunika bendera ya Brazil ya rangi ya kijani, njano na buluu, wakati baadhi ya wafuasia wa Rousseff wakiandamana pia.
Rais Dilma Rousseff , aliondoka Ikulu ya Planalto katika mji mkuu Brasilia huku maelfu ya wanaomuunga mkono wakijikusanya kumuaga.
Waungaji wake mkono wakiimba kauli mbiu kama "Ruosseff shikilia" na "waliopanga mapinduzi wataondoka" wakieleza mshikamano wao na Rousseff.
Wengine wameeleza kwamba serikali imewatoa mamilioni ya watu kutoka katika umasikini . Ni mara ya kwanza serikali kupiga hatua kama hiyo ya maendeleo katika historia. Usawa wa kijamii umeimarika tangu chama cha Wafanyakazi kuingia madarakani miaka 13 iliyopita.
Viongozi wa mrengo wa kushoto
Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesema "Sina shaka yoyote kwamba mswada huu wa mapinduzi umetengenezwa Marekani. Sina shaka na hilo. Hii inatengeneza sehemu ya kile rais Obama anachokiacha nyuma katika mataifa ya America ya kusini, akiwatenga wana mageuzi, demokrasia na vuguvugu la wananchi.
Serikali ya Cuba imesema inashutumu vikali mapinduzi ya kisheria bungeni, yaliyovikwa uhalali ambao umekuwa ukiendelea nchini Brazil kwa miezi kadhaa. Wengi wa maseneta wa Brazil wameamua kuendelea na hatua za kumshitaki kisiasa rais wa Brazil aliyechaguliwa kihalali na wananchi , Dilma Rousseff.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / ape
No comments:
Post a Comment