SERIKALI imesema itaanza kutumia mbinu mpya kuwadhibiti madaktari na wauguzi wanaoiba dawa za serikali na kisha kuziuza kwenye maduka ya watu binafsi.
Tamko hilo lilitolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John Kijazi alipoenda kukabidhi magodoro 50 katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dar es Salaam Mwananyala yaliyotolewa na umoja wa makanisa ya Kipentekoste nchini.
Kijazi alisema mbinu hiyo itasaidia kuwabaini kiurahisi watumishi hao kwani itaendeshwa kwa siri ambapo kila kitengo katika wizara ya afya kutakuwa na mwakilishi atakayesaidia kutoa taarifa pindi atakapoona jambo hilo.
“Mimi niwatake wenye tamaa waache mara moja haiwezekani dawa serikali inunue kwaajili ya kuwapatia wananchi bure mtu mmoja kwa manufaa yake azipeleke kwa wafanyabiasha kuuza wananchi wakose dawa na kuanza kuhangaika”alisema Kijazi.
Pia amewataka wauguzi kuhakikisha kwamba malalamiko yanayotolewa na wananchi yanafanyiwa kazi mara moja na kuongeza serikali haitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kumnyanyasa mgonjwa.
Alisema wagonjwa wamekuwa wakitoa malalamiko mengi juu ya huduma zinazotolewa katika hospitali ya Mwananyamala hivyo amewataka watendaji kubadilika ili kuepuka malalamiko yasiyo ya msingi.
Alisema ni lazima watoa huduma za afya wakazingatia nidhamu na weledi katika utendaji wa kazi kwani hawakulazimishwa kusomea taaluma hiyo na kuongeza kuwa fani zipo nyingi hivyo ambaye anaona hawezi kufanya yanayotakiwa aachie wengine.
Pamoja na hayo amezitaka hospitali zote kuanzisha dawati la malalamiko ili wanaohudumiwa wapate pakusemea pindi wanapofanyiwa vitendo vya unyanyasaji ikiwa ni pamoja na kucheleweshewa huduma au kuombwa fedha ili kuwahishiwa huduma ili hali ikiwa ni haki yao.
Hata hivyo ametaka madawati hayo kuwa wazi masaa 24 ili wananchi wapate muda mwingi wakujieleza na sio kusubiri kuelezea hisia zao pale wanapoona viongozi wakitembelea vituo hivyo.
Kijazi alitembelea wodi mbalimbali hospitalini hapo ikiwamo wodi ya wazazi, Wanaume, Watoto, Wanawake na watoto njiti ambapo alipata kujionea baadhi ya wagonjwa wakilala zaidi ya mmoja kwenye kitanda kimoja kutokana na kukosekana kwa vitanda.
Naye Mganga mkuu msaidizi katika hospitali hiyo Delila Moshi alieleza matatizo yanayoikabili hospitali hiyo kuwa ni pamoja na madeni ambapo inadaiwa stahiki za watumishi Sh. milioni 500 ambazo ni fedha za likizo kwa wafanyakazi, Sare za kazi, Nyumba na posho za masaa ya ziada.
Moshi alisema hospitali hiyo pia ina ukosefu wa vifaa vya kisasa kama CT Scan hali inayosababisha wagonjwa kupewa rufaa ya kwenda muhimbili kwaajili ya vipimo zaidi, Ukosefu wa chumba cha uangalizi wa wagonjwa mahututi (ICU) na Daktari bingwa wa mifupa na wagonjwa wa dharura.
Tatizo lingine ni wingi wa wagonjwa wa msamaha ambapo kwa kuanzia januari hadi desemba mwaka jana zaidi ya bilioni 2 zilitumika huku kwa mwezi wakitoa matibabu ya zaidi ya milioni 100 bure.
No comments:
Post a Comment