Sunday, March 27, 2016

Ongezeko la baa Mbeya na biashara ya ngono




BIASHARA ya vileo inazidi kushamiri siku hadi siku mkoani Mbeya kama ilivyo kwa maeneo mengine nchini. Kushamiri kwa biashara hiyo kunaenda sambamba na ubunifu wa wamiliki wa maeneo hayo ya burudani ili kuvutia wateja.
Maeneo ya Mwanjelwa, Kabwe, Soweto, Ilomba na Sae yaliyopo pembezoni mwa barabara kuu ni miongoni mwa sehemu zenye baa nyingi. Ingawa mkoa wa Mbeya una makanisa mengi wingi wa nyumba hizo za ibada haujawa kikwazo cha ongezeko la baa mkoani humo. Inadaiwa kwamba uwepo wa maeneo mengi ya kuuza mvinyo ni matokeo ya jiji la Mbeya kupata wageni wengi na kipato kizuri cha wakazi wake.
Kuna watu wengi wanaokwenda Mbeya wakitoka mikoa mbalimbali nchini, nchi jirani za Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Wageni wengi wanaokuja Mbeya ni wafanyabiashara wanaopeleka bidhaa kutoka makwao au kwenda kuchukua zinazozalishwa mkoani humo yakiwemo mazao ya chakula na biashara.
Mazao hayo ni pamoja na ndizi, mahindi, kokoa, mpunga na kahawa. Kuna wanaoamini kwamba, uwepo wa maeneo mengi ya starehe ni dalili za kukua kwa uchumi wa eneo husika. Wingi wa maeneo hayo umesababisha kukua kwa ushindani hivyo wamiliki wa huduma mbalimbali vikiwemo vileo wanajitahidi kuwa wabunifu kupata wateja.
Kuwa na wahudumu warembo katika mabaa ni moja kati ya ubunifu huo. Wafanyabiashara wa vileo wanasema, wahudumu warembo wanashawishi wateja kwenda walipo hivyo mauzo yanaongezeka. “Usione watu wanajaa namna hii ukajiuliza maswali mengi.
Ni kweli wengine wanaweza kusema umetumia kizizi na wengine wakasema umeboresha mazingira yako vizuri. Lakini ukweli ni kwamba siku mabinti hawa wakipungua na mauzo yanapungua pia,” anasema mmoja wa wafanyabiashara ya vileo katika maeneo ya Mwanjelwa. Inadaiwa kuwa wahudumu wengi wanafuatwa mbali na maeneo wanapofanya kazi ili kuepuka usumbufu zikiwemo ruhusa za mara kwa mara na kurubuniwa.
Kuna taarifa zinazodai kuwa, wateja kwenye maeneo hayo hawavutiwi na namna tu wanavyohudumiwa na warembo ila pia kuna cha ziada wanachokipata kwa wanawake hao, ikiwemo huduma ya ngono. Kuna madai kwamba, wahudumu wengi wa baa wanafanya biashara ya ngono na kwamba, wateja wao wakubwa ni wanaokwenda kunywa kwenye maeneo hayo.
Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Community Media Organization (Tacomo), linasema limefanya uchunguzi na kubaini hali mbaya kwa kuwa wahudumu wa kike wanafanya pia biashara ya ngono na wakati mwingi katika mazingira hatarishi. Mkurugenzi wa Tacomo, Gordon Kalulunga, anasema kuna tatizo la wasichana wanaofanya kazi kwenye baa kufanyiwa ukatili wa kingono na kwamba, chanzo cha ukatili huo na waajiri wao.
Kwa mujibu wa shirika hilo, wanawake hao wapo hatarini lakini hawatoi taarifa kwa hofu ya kufukuzwa kazi na usalama wa maisha yao. “Waajiri wakiwemo wamiliki wa baa na mameneja wamekuwa wakiwalazimisha wahudumu kufanya nao ngono kabla ya kuwapa ajira hizo. Lakini hata mara baada ya kuwaajiri huwalazimisha kufanya ngono na wateja wa baa hizo kwa makubaliano ya wateja hao kulipia kati ya shilingi elfu tano hadi elfu kumi kwa siku, fedha iliyopewa jina maarufu la malipo ya kaunta.
Malipo haya hayamhusishi binti anayekwenda kutumikishwa katika ngono bali itategemeana huruma ya mtu aliyekwenda naye akiamua kumlipa sawa na asipotaka pia haya,” anasema Kalulunga. “Kibaya zaidi ni kwamba tumebaini uwepo wa biashara ya binadamu ambapo kuna wahudumu wamekuwa mawakala wa kuwanunua wenzao mikoani kwa kuwalaghai kuwa waje Mbeya kufanya kazi za hoteli na kulipwa fedha nyingi, ahadi ambayo haitimii kwani wakifika hapa wanaishia kutumikishwa kingono kwenye baa wanazoajiriwa,” anasema.
Anaitaja mikoa ambako wasichana wengi wanatoka na kwenda Mbeya kutumikishwa kingono kuwa ni pamoja Singida, Iringa, Njombe na Ruvuma. “Mkoa wa Singida unaongoza katika jambo hili. Tulichobaini ni kuwa wengi wanadanganywa kwa kuahidiwa mambo makubwa wakiwa makwao. Ndiyo sababu utakutana na mabinti wadogo wanaotoka kwenye mkoa huo wakifanya kazi za uhudumu katika baa za hapa mjini. Wapo pia wanaokuja hapa baada ya kutoroka mashuleni.
“Ukweli wanapofika hawakutani na yale walioahidiwa wakiwa nyumbani. Hujikuta wametumbukia kwenye hatari ya ulevi na ukahaba kwa kulazimishwa na waajiri wao,” anasema Kalulunga. “Wanajikuta kuhiari utumwa wa kuuzwa kwa kuwa wanapofika hupewa chumba kimoja kwa ajili ya kulala na kuhifadhi vitu vyao kama nguo. Haijalishi wako wengi kiasi gani. Wengine hupewa godoro na kitanda kimoja ili walale hapo.
Wao huviita vyumba hivi gheto. Siku pekee ambayo binti anaona analala vizuri ni pale anapobebwa na mwanaume kwenda kufanya naye ngono kwa kuwa watalala wawili tofauti na gheto anajiona mwenye bahati. Huenda pia akala chakula kizuri zaidi ya wanachokula wenzie ghetoni,” anasema Kalulunga. Anasema Tacomo wameandaa mafunzo kwa wahudumu waweze kujitambua ili wasiwe waoga wa kutoa taarifa.
Anawaomba wadau kuona umuhimu wa kushiriki katika mpango huo na anavitaja vyombo vya habari kuwa ni mhimili muhimu utakaowezesha kuikomboa jamii ya wahudumu wa baa. Anatoa mwito kwa wahudumu wa kike kwenye baa mkoani Mbeya wajitokeze kwenye vyombo vya habari na vya sheria watoe malalamiko ya ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa, hasa kulazimishwa kutoa rushwa za ngono ili kuajiriwa.
Kuhusu hatari ya kuambukizana maradhi, Kalulunga anasema mara nyingi wawili hao, mwanaume na mhudumu wa baa huwa wamelewa na hivyo wanapofikia uamuzi wa kwenda kufanya ngono uhakika wa kutumia kinga inavyostahili huwa mdogo. Katika mahojiano wakati wa kuandika makala haya, mhudumu mmoja wa baa aliyejitambulisha kwa jina moja la Jasmini alisema: “Kama tunajikuta tumebeba mimba kutokana na wanaume haohao tunaolewa nao, si rahisi kukwepa magonjwa ya zinaa.
Upo uwezekano mkubwa wa kupata pia maambukizi kwa kuwa wakati mwingine tunakosa namna ya kujitetea hasa pale mwanaume anapokuwa amekulipia kaunta na umekunywa bia zake.” “Inafikia wakati yule anayepata wanaume wengi anaonekana mwenye bahati zaidi ya wengine. Atakula vizuri, atavaa vizuri, atasuka vizuri na atapendeza zaidi hata tunapokuwa tumeingia kazini.
Anakuwa amejitengenezea mtaji mzuri wa kupata mwanaume mwingine aliye na fedha nyingi. Hivyo unapoanza shughuli hii kwa kumpata mwanaume mwenye nazo pesa unakuwa umejipatia mtaji mzuri sana,” anasema msichana huyo.
Unknown Web Developer

Morbi aliquam fringilla nisl. Pellentesque eleifend condimentum tellus, vel vulputate tortor malesuada sit amet. Aliquam vel vestibulum metus. Aenean ut mi aucto.

No comments:

Post a Comment