Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumatano ya kesho tarehe 30 Machi anatarajiwa kuelea Vienna Austria kujibu mwaliko wa Rais wa nchi hiyo Heinz Fischer.
Katika safari hiyo ambapo Rais Rouhani anauongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi, pande mbili zinatarajiwa kufikia makubaliano ya mwisho kuhusiana na hati ya Ramani ya Njia ya ushirikiano wa kiuchumi. Kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Austria, Kansela wa nchi hiyo na kushiriki katika kongamano la wanaharakati wa masuala ya kiuchumi wawakilishi wa sekta binafsi za Iran na Austria ni sehemu ya ratiba ya Rais Hassan Rouhani akiwa katika mji mkuu wa Austria Vienna. Aidha katika safari hiyo, pande mbili zinatarajiwa kutiliana saini hati za ushirikiano wa kiuchumi katika nyuga mbalimbali. Akizungumza wakati wa kukaribia safari ya Rais Hassan Rouhani, Rais wa Austria amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na Shirika la Habari la Radio na Televisheni la Iran kwamba, historia ya ushirikiano kati ya Iran na Austria inarejea nyuma miaka mingi. Rais Fischer amebainisha kuwa, Iran ni nchi kubwa katika eneo lenye mivutano mingi la Mashariki ya Kati na ulimwengu kwa ujumla ambayo ikishirikishwa inaweza kuwa na nafasi muhimu katika kupunguza migogoro iliyopo. Rais wa Austria ameashiria mgogoro wa Syria na kusisitiza kuwa, hadi sasa mgogoro wa nchi hiyo umepelekea watu wengi kuuawa huku bara Ulaya likikabiliwa na wimbi la wahajiri. Amesema, Ulaya inaweza kuisaidia Iran ikiwa dola kubwa katika Mashariki ya Kati na hivyo kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria. Rais wa Austria ameashiria kufikiwa makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na madola sita makubwa duniani yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kubainisha kwamba, makubaliano hayo yamefungua ukurasa mpya katika uhusiano na Iran na Austria. Rais Fischer ameashiria pia safari yake ya hivi karibu hapa mjini Tehran na mazungumzo yake na Kiongozi Muadhamu, Rais Hassan Rouhani, Spika wa Bunge la Iran na viongozi wengine wa ngazi za juu hapa nchini na kubainisha kwamba, safari hiyo ilikuwa na mafanikio makubwa.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kufikiwa makubaliano ya nyuklia ya Iran na madola sita makubwa duniani kumefungua ukurasa mpya wa uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu na madola ya Ulaya. Kuondolewa vikwazo Iran na kuandaliwa mazingira mazuri ya kiuchumi kunaweza kuifanya Iran kuwa mshirika bora kabisa wa kiuchumi na nchi za Ulaya.
Kwa sasa kuna mazingira mazuri nchini Iran ya kukua uchumi na nchi za Ulaya zinaweza kuwekeza nguvu kazi amilifu kwa ajili ya kunufaika na fursa hii. Iran ni nchi kubwa zaidi inayotengeza magari Mashariki ya Kati na Austria inaweza kuwa na ushirikiano mzuri na Iran katika uwanja wa utengenezaji magari. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana safari ya Rais Hassan Rouhani nchini Australi ikatathminiwa kuwa na umuhimu wa aina yake.
No comments:
Post a Comment