Rais mpya wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliapishwa rasmi jana katika sherehe zilizofanyika katika uwanja mkuu wa michezo mjini Bangui.
Katika sherehe hiyo iliyohudhuriwa na marais kadhaa wa nchi za magharibi mwa Afrika, Rais Faustin-Archange Touadera alikula kiapo cha kulinda katiba ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na kurejesha amani nchini humo. Vilevile ameahidi kutekeleza vyema majukumu yake bila ya kuathiriwa na mitazamo ya kikabila au kidini.
Faustin-Archange Touadera ambaye alikuwa mwalimu wa somo la hesabati aliwashangaza wengi baada ya kupata ushindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Februari 14 mwaka huu.
Hivi sasa baada ya karibu miaka mitatu ya mapigano na vita vya ndani, wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wana matarajio ya kushuhudia tena amani na usalama nchini humo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, wataalamu wa mambo wanasisitiza kuwa ukosefu wa usalama na amani ndiyo changamoto kubwa inayoikabili serikali mpya ya Bangui. Kwa msingi huo inaonekna kuwa, miongoni mwa majukumu muhimu zaidi ya rais mpya wa CAR ni kurejesha hali ya utulivu na mapatano ya kitaifa.
Japokuwa ni kwa muda sasa ambapo vita vimekomeshwa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati lakini mapigano ya hapa na pale yangali yanashuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Siku chache zilizopita Rais wa serikali ya mpito ya Jamhuri ya Afrika ya Kati Bi Catherine Samba-Panza alikiri kuwa hakufanikiwa kuyapokonya silaha makundi yote ya wanamgambo na kueleza kwamba, ana matumaini serikali mpya itapata ufumbuzi wa matatizo mawili makuu ambayo ni tatizo la ukosefu wa usalama na silaha zinazomilikiwa na makundi ya wanamgambo.
Mgogoro wa chakula, hali mbaya sana ya kibinadamu hususan watoto na wanawake, matatizo ya kiuchumi na umaskini ni changamoto nyingine zinazoikabili serikali mpya ya CAR.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon pia ameeleza kusikitishwa na mashaka yanayowasumbua watoto katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kutokana na ukati wa aina mbalimbali. Watoto wa nchi hiyo wamekuwa wahanga wa ukatili wa kingono uliofanywa na askari wa kulinda amani waliotumwa kuwalinda. Maelfu ya watoto wadogo pia wameuawa katika mapigano ya ndani na waliookoka wameshuhudia mauaji ya kutisha, suala ambalo yumkini likawasababishia wengi miongoni mwao matatizo ya kinafsi ya kisaikolojia.
Kwa msingi huo kuna haja ya kutiliwa maanani zaidi hali ya watoto wadogo na kuanzishwa vituo vya elimu vyenye suhula za kutosha kwa ajili ya kizazi kipya cha nchi hiyo iliyoathiriwa na vita. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Jamhuri ya Afrika ya Kati inasumbuliwa na hali mbaya sana ya uchumi licha ya kuwa na utajiri wa madini kama almasi na dhahabu. Idadi kubwa ya vijana wa nchi hiyo hawana kazi na nchi hiyo haina miundombinu mizuri ya uchumi na ustawi.
Tukiachia mbali hayo yote kwa sasa nchi hiyo inasumbuliwa na uhaba wa chakula. Mkurugenzi Mkuu wa shirika la WFP alisema kuwa Jamhuri ya Afrika ya Kati inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa chakula kwa kadiri kwamba, nusu ya watu wa nchi hiyo wanasumbuliwa na njaa.
Kwa vyovyote vile serikali mpya ya Jamhuri ya Afrika ya Kati itakuwa na kibarua kikubwa cha kushughulikia matatizo mengi ya nchi hiyo na kuhakikisha angalau inapunguza machungu na mashaka ya watu wa nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment