Serikali ya Brazil imepata pigo baada ya chama mshirika cha PMDB, kujiondoa katika serikali ya muungano, kikisema kimeacha kuiunga mkono serikali ya Rais Dilma Rousseff.
Chama cha Democratic Movement-PMDB ambacho ni chama kikubwa cha kisiasa nchini Brazil, kimetangaza kujiondoa kwenye serikali ya muungano ya Rousseff kwa kuwataka mawaziri wake sita wajiuzulu mara moja au wachunguzwe na kamati ya maadili ya chama hicho. Makamu rais wa chama hicho, Seneta Romero Juca, mwenye ushawishi mkubwa, amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya wabunge 100 kuidhinisha uamuzi huo.
''Kuanzia leo na kuendelea katika mkutano huu wa kihistoria wa PMDB, chama chetu kinajiondoa kwenye serikali ya Rais Dilma Rousseff na hakuna hata mtu mmoja anayeruhusiwa kushika wadhifa wowote wa shirikisho chini ya jina la chama chetu,'' alisema Juca.
Kujiondoa kwa chama hicho sasa kunamuweka mahali pabaya Rais Rousseff katika hatari ya kuondolewa madarakani na bunge. Hali hiyo inaondoa nafasi ya kiongozi huyo kupata theluthi moja ya kura za bunge ambazo anazihitaji kujitetea asiondolewe madarakani katika kura ya kutokuwa na imani naye, inayotarajiwa kupigwa mwezi ujao wa Aprili.
Mkutano wa chama hicho ulimalizika huku ukikitaka chama cha Wafanyakazi cha kiongozi huyo kuondoka madarakani na Makamu wa Rais wa Brazil, Michel Temer, ambaye ni wa chama cha PMDB, awe rais mpya.
Temer anaendelea kuwa makamu wa rais
Temer mwenye umri wa miaka 75, ambaye anaendelea kuwa makamu wa rais chini ya serikali ya sasa ya Brazil licha ya kuvunjika kwa serikali ya muungano, atakuwa rais wa mpito iwapo Rais Rousseff ataondolewa madarakani na bunge.
Aidha, hatua hiyo imemfanya kiongozi huyo kuahirisha ziara yake nchini Marekani kuhudhuria mkutano wa kilele wa usalama wa nyuklia utakaofanyika siku ya Alhamisi na Ijumaa, ili aweze kukabiliana na mzozo unaoendelea nchini kwake ambao unatishia kumuondoa katika nafasi yake.
Utafiti wa maoni uliofanywa hivi karibuni umeonyesha kuwa asilimia 68 ya watu wanawataka wabunge wapige kura ya kutokuwa na imani na Rais Rousseff, huku asilimia 11 tu wakiamini kwamba watakuwa na serikali bora chini ya Temer.
Wananchi wa Brazil wamekuwa katika maandamano makubwa wakimshinikiza Rais Rousseff ajiuzulu kutokana na kashfa kubwa ya rushwa dhidi ya kampuni ya mafuta ya Petrobras. Wafuasi wa rais huyo wamesema maandamano ya kumtaka ajiuzulu ni sehemu ya jaribio la mapinduzi na wameapa kuandamana pia kuutetea utawala wake.
Hivi karibuni jaji mkuu wa Brazil, alipitisha uamuzi kumzuia rais wa zamani wa nchi hiyo, Luiz Inacio Lula da Silva kuchukua wadhifa wake kama mnadhimu mkuu wa baraza la mawaziri. Wakosoaji wanasema hatua ya Rousseff kumteua Lula, ni jaribio la kumkinga dhidi ya kashfa ya rushwa inayomkabili.
No comments:
Post a Comment