Huku kukiwa na uwezekano mkubwa wa kupata ushindi Donald Trump katika uteuzi wa mgombea wa chama cha Republican kuwania urais Marekani, kumeibuka wasi wasi kuhusu taathira hasi ya mwanasiasa huyo wa kutatanisha na bilionea katika sera za kigeni za Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry amekiri kuwepo utovu wa nidhamu katika kampeni za uchaguzi wa rais nchini humo na kusema jambo hilo limepelekea Marekani kuaibika kimataifa. Naye Leone Penetta waziri wa zamani wa ulinzi wa Marekani amesema, Trump ni mtu asiyewajibika na hadiriki ipasavyo usalama wa taifa la Marekani.
Katika siku za hivi karibuni, Trump ameanza kutoa matamshi kuhusu sera za kigeni za Marekani. Trump ametamka mara kadhaa kuwa, iwapo atachaguliwa kuwa rais wa Marekani mwaka huu, atasitisha ununuzi wa mafuta ya petroli kutoka Saudi Arabia hadi pale Riyadh itakapotuma wanajeshi kukabiliana na magaidi wa Daesh au ISIS. Aidha amesema atazipatia Japan na Korea Kusini silaha za nyuklia ili zikabiliane na kile alichodai kuwa ni tishio la Korea Kaskazini.
Kabla ya hapo pia, Trump aliwahi kutoa wito wa kujengwa ukuta wa kiusalama baina ya Marekani na Mexico kwa gharama ya serikali ya Mexico. Hali kadhalika Trump ametaka Waislamu wapigwe marufuku kuingia Marekani.
Katika kujaribu kuwavutia wapiga kura, Trump amekuwa akitoa nara ya 'Kuifanya Marekani iwe na Nguvu Tena' yaani Make America Great Again.
Mwanagenzi huyo wa siasa za Marekani ameitaja nchi hiyo kuwa "iliyodhoofika katika kipindi cha utawala wa Barack Obama hadi kufika kiwango cha adui kupata ujasiri wa kuhatarisha maslahi ya Washington na waitifaki wake."
Kwa mtazamo wa Trump, si maadui tu waliofaidika na udhaifu wa Markenia bali hata waitifaki wake kama vile Saudia na Mexico wamefaidika na udhaifu huo.
Trump anasema serikali ijayo ya Marekani inapaswa kutumia mkono wa chuma kukabiliana na mataifa mengine duniani. Watu kama Trump wanaamini kuwa, Marekani inapaswa kutumia uwezo wake wa kijeshi na kiuchumi kuazisha mfumo mpya wa kimataifa.
Weledi wa sera za kigeni na usalama Marekani na hata wanasiasa wa chama cha Republican wameonya kuhusu mitamzamo hiyo ya kufurutu ada ya Trump.
Wanasema matamshi ya Trump si tu kuwa yanahatarisha usalama wa Marekani pekee bali wa dunia nzima kwa ujumla. Kwa mtazamo wa weledi hao, dunia ya karne ya 21 haijaundika kwa namna inavyotaka Marekani.
Aidha kutoa matamshi kama vile kuzipa Japan na Korea Kusini silaha za atomiki, kuanzisha vita vya kibiashara na China, kujenga ukuta wa kiusalama na Mexico na kukabiliana na Waislamu ni mambo ambayo yataiweka Marekani katika mapambano na pande kadhaa duniani, mapambano ambayo yatadumu kwa muda mrefu na kuipelekea Washington kupata hasara kubwa.
Hakuna shaka kuwa iwapo Trump atachaguliwa kuwa rais wa Marekani, dunia nayo itachukua hatua za kukabiliana na sera hizo hatari na za kufurutu ada.
Kwa kuzingatia udhaifu wake wa kiuchumi, kisiasa, na kiutamaduni, Marekani bila shaka itadhoofika zaidi katika makabiliano na dunia.
Inaelekea kuwa Trump yuko tayari kutumia kila njia ili ateuliwe na chama cha Republican kuwania urais wa Marekani.
Pamoja na hayo, iwapo baadhi ya yale ambayo Trump amekuwa akiyasema yatatekelezwa, basi dunia itaondokewa na utulivu na amani.
No comments:
Post a Comment