Moshi. Imeelezwa kuwa watu tisa kati ya 10 wenye ulemavu wa ngozi (albino) hufariki dunia kabla ya kufikisha umri wa miaka 30 kutokana na saratani ya ngozi inayosababishwa na ukiukwaji wa ushauri wanaopewa na madaktari wa ngozi.
Hayo yamebainishwa leo na mwakilishi wa Taasisi ya Kilimanjaro Suncare, Maflda Soto kwenye warsha ya kujadili changamoto zinazowakabili albino, iliyozikutanisha taasisi 10 zinazotoa huduma kwa walemavu hao nchini na uongozi wa juu wa chama cha watu wenye ualbino Tanzania (TAS).
Maflida amesema kutokana na baadhi yao kutofuata masharti ikiwamo kuhudhuria kliniki na kutopaka mafuta yao kunasababisha wengi wao kufa kutokana na kuugua saratani ya ngozi.
“Ikumbukwe kuwa watu wenye ualbino wanaathirika zaidi na jua kwasababu ya upungufu wa rangi kwenye ngozi, wanaungua kirahisi na wengi wao hufa kwa saratani ya ngozi kabla ya kufikisha miaka 30,” amesema Maflida.
Amesisitiza kuwa elimu ya vifaa vya kinga ya ngozi ni njia moja wapo ya kumsaidia mtu mwenye ualbino kuweza kuishi kwa muda mrefu kama ilivyo kawaida.
Daktari wa taasisi ya ngozi katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Alfred Naruri alisema walemavu wengi wa ngozi hupuuza ushauri wanaopatiwa na madaktari na kuugua magonjwa hayo kisha kufa.
No comments:
Post a Comment