KAMPUNI ya Vodacom nchini, imezindua mauzo ya simu za kisasa zisizoingiza maji aina ya Galaxy S7 na S7 Edge kwa kushirikiana na Samsung. Uzinduzi huo ulifanyika jana Dar es Salaam na tayari zimeanza kuuzwa katika maduka yote ya Vodacom na Samsung nchini.
“Samsung Galaxy S7 na Galaxy S7 Edge zitakuwa zikitolewa kupitia maduka yetu yote huku zikiambatanishwa na Power-Bank ya bure; pia wateja 50 wa kwanza watajipatia Bluetooth Earphones za Galaxy za bure pia,” alisema Samson Mwongela, Mkuu wa Kitengo cha Huduma na Bidhaa cha Vodacom Tanzania.
Mwongela alibainisha kuwa simu hizo zimekuja zikiwa na maboresho yanayolenga kukidhi mahitaji ya vijana wa kisasa hususan katika msimu huu wa sikukuu ya Pasaka, ambapo watumiaji watafurahia na intaneti ya kasi na haraka zaidi nchini kutoka Vodacom.
Akielezea sifa za simu hizo, Meneja Mwendeshaji wa Samsung nchini, Suleiman Mohammed alisema zina uwezo wa kutoingiza maji, hata pale zinapokuwa katika kina cha mita moja na nusu kwa dakika zisizozidi 30.
“Hakika kwa sasa hakuna tena kikomo kwa vijana hapa nchini kuweza kuwasiliana na ndugu, jamaa na rafiki zao popote walipo ulimwenguni, hasa ukizingatia tunaelekea kufikia tamati ya matumizi ya simu zisizokuwa halisi na zenye ubora hapa nchini kabla ya kuisha Juni mwaka huu,” alisema Mohammed.
No comments:
Post a Comment