Friday, March 25, 2016

Stars waahidi raha zaidi





KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ‘Taifa Stars’, Charles Mkwasa amewashukuru na kuwapongeza wachezaji wake kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Chad juzi na kuahidi wataendelea kuwapa furaha Watanzania katika michezo ijayo.
Katika mechi hiyo ya kuwania kufuzu fainali za michuano ya Kombe la Mataifa Afrika 2017 iliyochezwa mjini N’Djamena, Chad bao la Stars lilifungwa na nahodha wake Mbwana Samatta na kufufua matumaini ya timu hiyo.
Akizungumza kwa simu kutoka N’Djamena jana, kocha Mkwasa alisema anawashukuru wachezaji wake kwa ushindi huo kwani Watanzania walikuwa wanyonge na kwamba sasa wamepata furaha, ambayo itazidi kuongezeka kama wakishinda mchezo ujao.
“Kwanza nawashukuru wachezaji wangu sana maana ushindi huu umerudisha imani ya Watanzania, lakini pia niwapongeze sana kwa sababu huku hali ya hewa ni joto zaidi ya huko nyumbani, iliwapa tabu sana wachezaji wangu, lakini wakapambana kuibuka na ushindi… walisikiliza na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi kama tulivyowaelekeza,” alisema.
Matokeo hayo yameifanya Stars kufikisha pointi nne katika Kundi G ambalo pia lina timu za Misri na Nigeria.
Misri inaongoza ikiwa na pointi sita na Nigeria inafuata ikiwa na pointi nne kama Stars ila yenyewe ina uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa. Hiyo ilikuwa mechi ya kwanza kwa Stars tangu ilipofungwa mabao 7-0 ugenini dhidi ya Algeria katika mechi ya kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwishoni mwa mwaka jana.
Mkwasa alisema kilicho mbele yake baada ya matokeo hayo ni kukiandaa kikosi chake kwa mechi ya marudiano dhidi ya Chad itakayochezwa Jumatatu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Niwashukuru tena Watanzania jamani sapoti yao tumeiona, wanatuunga sana mkono nasi hatutaki kuwaangusha, tutafanya tunavyoweza kushinda Jumatatu, nawaomba tena waje kwa wingi uwanjani kutuunga mkono, tushirikiane kupata ushindi mechi hii,” alisema.
Baada ya mechi hiyo ya marudiano, Stars itacheza tena na Misri Juni 4 Dar es Salaam kabla ya kufunga safari ya kuifuata Nigeria Septemba mwaka huu. Mechi ya kwanza dhidi ya Misri iliyochezwa mwaka jana mjini Cairo, Stars ikiwa chini ya kocha Mholanzi Mart Nooij ililala kwa mabao 3-0.
Akizungumzia mechi hizo, Mkwasa alisema hakuna kinachoshindikana kwenye mpira hivyo ana imani timu yake itaendelea kupata matokeo mazuri.
“Timu yangu iko vizuri nashukuru, makosa madogomadogo tunaendelea kuyarekebisha kadri siku zinavyokwenda, naomba tuungwe mkono tu,” alisema.
Fainali za Kombe la mataifa Afrika mwaka 2017 zimepangwa kufanyika Gabon. Tanzania ilishiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza na ya mwisho mwaka 1980 huko Lagos, Nigeria.

Unknown Web Developer

Morbi aliquam fringilla nisl. Pellentesque eleifend condimentum tellus, vel vulputate tortor malesuada sit amet. Aliquam vel vestibulum metus. Aenean ut mi aucto.

No comments:

Post a Comment