Yanga itakutana na Al Ahly baada ya kuvuka raundi ya kwanza kwa kuitoa APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ambapo mchezo wa kwanza Yanga ilishinda Rwanda mabao 2-1 na ule wa marudiano uliochezwa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki zilitoka sare ya bao 1-1.
Akizungumza na gazeti hili, Pluijm alisema Al Ahly ni timu nzuri, lakini haifanyi wao kuogopa kwani kama watajipanga vizuri na kurekebisha upungufu wao ni wazi wanaweza kufanya vizuri.
“Ninaijua Al Ahly sio mara ya kwanza kukutana. Tuliwahi kukutana mwaka juzi katika Kombe la Shirikisho, walituzidi kidogo kwa penalti, ambapo ndipo sehemu muhimu walikotuangusha,” alisema na kuongeza kuwa mechi hiyo ijayo itakuwa ni ngumu kwa kuwa ni timu zinazofahamiana.
Alisema siri ya kuwatoa Al Ahly ni wachezaji kuzingatia kile wanachoelekezwa kwa kucheza kwa kujiamini na kuonesha ushirikiano.
Kocha huyo wakati mwingine amekuwa akiwalalamikia washambuliaji wake kushindwa kuonesha kiwango bora na kupoteza mawasiliano wenyewe, hali ambayo imekuwa ikisababisha kushindwa kutumia nafasi wanazozitengeza kufunga.
Kocha huyo alisema ana kazi ya kuendelea kuzungumza na wachezaji wake wasirudie makosa ya aina hiyo, kwani yanaweza kuwagharimu.
Awali, uongozi wa Yanga ulisema ili kufanya vizuri katika mchezo huo watafanya maandalizi mazuri, ikiwa ni pamoja na kutafuta kambi yenye utulivu ikiwezekana nje ya nchi.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alisema lengo la kwanza la timu hiyo ni kufikia katika hatua ya makundi, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha maandalizi ya timu yanakuwa mazuri.
No comments:
Post a Comment