Twiga Stars imeaga michuano ya awali kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa wanawake baadae mwaka huu baada ya kufungwa jumla ya mabao 3-2 na Zimbabwe.
Timu hiyo ilipoteza mchezo wa kwanza nyumbani kwa kufungwa mabao 2-1 kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 mjini Harare mwishoni mwa wiki iliyopita.
Twiga Stars ilirejea nchini alfajiri ya juzi. Akizungumza na gazeti hili jana, Nasra alisema yeye na wachezaji wake wamesikitishwa na matokeo hayo, lakini huo sio mwisho wa mapambano. “Tumetolewa mapema kwenye mashindano, lakini sio mwisho kwetu tutaendelea kupambana kwenye michuano mingine, Watanzania watuunge mkono wasituache maana bila wao hatuwezi,” alisema.
Nasra alisema bado soka ya wanawake inayo nafasi ya kufanya vizuri endapo wadau watawekeza na kuamua kuisaidia.
Twiga Stars iliwahi kufuzu fainali za michuano hiyo zilizofanyika Afrika Kusini mwaka 2010 na kuishia hatua ya makundi.
Timu hiyo pia ilicheza fainali za michezo ya Afrika mwaka jana zilizofanyika Congo Brazzavile, ambapo pia iliishia hatua ya makundi.
No comments:
Post a Comment