Jeshi la Somalia limefanikiwa kuwaua magaidi zaidi ya 115 wa kundi la kitakfiri la Al Shabab katika jimbo la Galmudug nchini humo.
Gavana wa jimbo hilo Abdikarim Hussein Guled amesema mapigano makali yalitokea siku ya Jumapili kati ya vikosi vya usalama na magaidi wa al Shabab na kwamba baada ya kumalizika mapigano hayo, magaidi 115 waliuawa na wengine 110 kutiwa nguvuni.
Guled amesema serikali ya jimbo hilo itawaangamiza magaidi kote Galmudug na kusaidia maeneo mengine ya Somalia katika kuwatimua magaidi.
Ameongeza kuwa mapigano hayo yaliendelea kwa muda wa siku nne na kusisitiza kuwa kuna haja kushirikiana ili kuhakikisha magaidi hawarudi tena eneo hilo baada ya kupata pigo.
Jeshi la Somalia linapambana na magaidi wa al Shabab kwa kushirikiana na Kikosi cha Kulinda Amani vya Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM chenye askari 22,000 katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
No comments:
Post a Comment