Friday, March 11, 2016

Dk Shein, Maalim Seif wakutana kwa robo saa




By Edwin Mjwahuzi, Mwananchi emjwahuzi@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein juzi usiku alifanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kwa takriban dakika 15 alipokwenda kumjulia hali kwenye Hoteli ya Serena jijini hapa.
Lakini, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa Ladhu amedai kuwa Dk Shein amefanya ziara hiyo kwa sababu alipata taarifa kuwa Rais John Magufuli alifika hapo kumjulia hali Maalim Seif baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali.
Maalim Seif yuko hotelini hapo kwa mapumziko baada ya kuruhusiwa kutoka Hospitali ya Hindu Mandal alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
“Dk Shein amekutana na Maalim Seif si kwa mazungumzo mengine yoyote, alikuja kumjulia hali tu na mazungumzo yao yalichukua takriban dakika 10,” alisema Jussa
Dk Shein alifika hotelini hapo saa 2.25 usiku na kwenda moja kwa moja kwenye chumba alichokuwa amefikia Maalim Seif na kufanya naye mazungumzo kwa muda usiozidi dakika 15.
Maelezo ya picha zilizotumwa na Ikulu ya Zanzibar yalieleza kuwa Dk Shein alikwenda kumjulia hali Maalim Seif baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali alikokuwa amelazwa Jumatatu na kuruhusiwa kutoka siku iliyofuata na hakuna maelezo ya ziada kuhusu mazungumzo hayo.
Wawili hao wamekutana siku kumi na moja kabla ya uchaguzi wa marudio kufanyika Zanzibar, baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana.
Jecha alifuta uchaguzi huo Oktoba 28, mwaka jana kwa madai ya kuwapo kasoro kitendo ambacho kilipingwa na Maalim Seif aliyekuwa mgombea urais na baadaye yeye na chama chake cha CUF walitangaza kutoshiriki katika uchaguzi huo wa marudio.     

Unknown Web Developer

Morbi aliquam fringilla nisl. Pellentesque eleifend condimentum tellus, vel vulputate tortor malesuada sit amet. Aliquam vel vestibulum metus. Aenean ut mi aucto.

No comments:

Post a Comment