KUELEKEA Sikukuu ya Pasaka, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limepiga marufuku disko la mchana ambalo mara nyingi linahusisha watoto kwenye kumbi mbalimbali za burudani.
Disko la aina hiyo nyakati za sikukuu mbalimbali, limepata umaarufu zaidi kwa kuitwa Disko Toto.
Kwa mujibu wa taarifa kwa Basata iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Godfrey Mngereza, kamwe hawatafumbia macho wamiliki wa kumbi za burudani wanaokiuka taratibu.
“Basata linawakumbusha wamiliki wote wa kumbi za sherehe na burudani kwamba ni marufuku kukusanya watoto katika kumbi zao kupitia kile kinachoitwa ‘Disko Toto’ katika msimu huu wa Sikukuu ya Pasaka ili kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.
“Uzoefu unaonesha kwamba, nyakati za sikukuu kama hizi wamiliki wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kuendekeza faida katika biashara zao kiasi cha kuandaa madisko ya watoto hali mbayo imekuwa ikisababisha maafa ambayo yangeepukika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu. “
Aidha, baadhi ya wamiliki na waendeshaji wa kumbi kwa msingi huohuo wa kuendekeza faida pasi na kujali maelekezo ya vibali vyao wamekuwa wakijaza watu kupita viwango vya madaraja waliyopangiwa na Basata,” ilisema taarifa hiyo.
Aliwakumbusha wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani kufuata sheria, kanuni na taratibu walizopewa kwenye vibali vyao vya uendeshaji wa kumbi.
“Wanaelekezwa kuhakikisha wanakuwa na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia muda wa utumizi wa kumbi, kuepuka kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalumu hasa makazi ya watu na kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu na mali zao,” alisema Katibu huyo.
No comments:
Post a Comment