Waogeleaji wakichuana katika mashindano mbalimbali yaliyopita.
Na Mwandishi wetu
Jumla ya waogeleaji 15 wa Tanzania (Tanzania Swim Squad) watashiriki katika mashindano ya kimataifa ya Afrika Kusini yaliyopangwa kuanza Machi 28 mpaka Aprili 3 mjini Johannesburg.
Wachezaji hao wametoka katika klabu tatu ambazo ni Dar Swim Club, Taliss na Arusha ambao wataogelea kwa kutumia jina la Tanzania Swim Squad (TSS) katika mashindano hayo ambayo yatafanyika kwa awamu mbili, yale ya ‘South Africa level 2’ na South Africa Level 1.
Mashindano ya South Africa Level 2 yamepangwa kuanza Machi 28 mpaka Machi 31 kwenye bwawa la kuogelea la Ellis Park na yale ya South Africa level 1’ yaliyopangwa kuanza Machi 31 mpaka Aprili 3 kwenye bwawa la kuogelea la Germiston.
Afisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Benson Chacha aliwataja waogeaji watakaoiwakilisha nchi katika mashindano ya South Africa level 2 kwa upande wa wanawake kuwa ni Marin de Villard, Celina Itatiro (Dar Swim Club), Amani Doggart (Taliss), Josephine Oosterhuis, Jacqueline Kortland na Isabella Kortland wote kutoka Arusha.
Kwa upande wa wanaume ni Adil Bharmal na Pieter de Raadt kutoka Arusha. Waogeleaji wa South Africa Level 1 kwa upande wa wanawake ni Ursula Khimji, Anjani Taylor (DSC) na Slyvia Caloiaro (Taliss) na Kayleen Van Rensburg wa Taliss wakati wanaume ni Dhashrrad Magesvaran, Harry Mcintosh na Oliver Mcintosh wote kutoka Taliss.
Kwa upande wa viongozi ambao wataambatana na wachezaji hao ni Inviolata Itatiro, Thauriya Bharmal ambao ni wakuu wa msafara na makocha ni Michael Livinstone, Alex Mwaipasi na Emma Mcintosh.
“BMT imetoa kibali kwa waogeleaji hao kwa ajili ya kuiwakilisha nchi katika mashidano hayo muhimu, waogeleaji hao wanatarajia kuondoka Jumamosi na Jumapili, mchezo wa kuoegelea kwa sasa unakuja juu sana na lengo letu ni kuona tunapata mfanikio kupitia mchezo huu, mashindano kama haya ya kimataifa ni muhimu sana kwa waogeleaji wetu,” alisema Chacha.
Chacha pia alisema kuwa pia wameiruhusu waogeaji wa shule ya Braeburn ambao nao watashiriki katika mashindano hayo.
Katibu Mkuu wa Dar Swim Club, Inviolata Itatiro alisema kuwa wanashiriki mashindano hayo kwa mara ya pili na lengo lao ni kupata uzoefu wa mashindano ya kimataifa.
“Haya ni mashindano makubwa ambayo yatawashirikisha waogeaji kutoka nchi mbalimbali Afrika, naamini Watanzania watajifunza na kupata uzoefu na baadaye kutuletea medali katika mashindano mengine kama ya Olimpiki, Jumuiya ya Madola na mashindano ya Dunia ya kuogelea,” alisema Inviolata.
No comments:
Post a Comment