Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim,Majaliwa akipokea tuzo ya filamu kutoka kwa msanii Single Mtambalike aliyoshinda katika Tuzo za Filamu Afrika kwa mwaka 2016 zilizofanyika chini Nigeria hivi karibuni kulia ni msanii Elizabeth Michael.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim,Majaliwa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa Tuzo za Filamu Afrika kwa mwaka 2016 pamoja na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia Wambura(wa pili kulia), Katibu Mkuu wa Wizara wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Prof Elisante Ole Grabriel(wa pili kushoto), kulia ni Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Joyce Fisso na kushoto ni Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) Simon Mwakifamba.
Picha na Raymond Mushumbusi MAELEZO
………………………………………………………………………………………………………………………………….
Na: Immaculate Makilika MAELEZO
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imefarijaka kwa ushindi wa wasanii wa filamu nchini walioshinda tuzo za filamu Afrika za mwaka 2016(African Magic Viewers Choice Award) ziliyofanyika jijini Lagos nchini Nigeria mwishoni wa wiki iliyopita.
Waziri Mkuu Majaliwa, amesema hayo leo katika ukumbi wa mikutano ulipo katika Ofisi yake Jijini Dares Salaam, alipokutana na washindi wa tuzo za filamu Afrika za mwaka 2016 (AMVCA) ambao ni Elizabeth Michael ‘Lulu’ aliyeshinda tuzo ya Filamu Bora ya Afrika Mashariki na Single Mtambalike ‘Richie’ aliyeshinda tuzo ya Filamu Bora ya Kiswahili pamoja Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Mhe. Annastazia Wambura,Katibu Mkuu wa wizara Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bi Joyce Fisso na wasanii wa filamu.
“Serikali imefarijika sana kwa nyie kwenda Nigeria na kushinda na mmetumia lugha ya Kiswahili, lazima tutumie nafasi hii kuwatangaza pia mmuendelee na fani hii ili kuvutia wengi zaidi” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu amewapongeza wasanii hao na kusema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wasanii wakati wowote na amewataka kujipanga vizuri kutumia vyama vyao vya sanaa na kusisitiza kuwa Mhe. Rais John Pombe Magufuli ametoa matamko kadhaa kuhusu sanaa na wasanii na ameendelea kushughulikia malalamiko yao ikiwemo suala la COSOTA, na kusema kuwa baada ya taratibu zote kukamilika suala hilo litasimamiwa na Wizara inayohusika na kazi za Sanaa.
Waziri Mkuu Majaliwa, pia amewataka watanzania kuacha tabia ya kutojiamini na kujidharau, na kuwataka watu waige mfano kwa wasanii hao, na kuwashauri wasanii wote kwa ujumla kutumia vyombo vya habari kujiimarisha na kujitangaza.
Kwa upande wao, wasanii waliopata tuzo hizo kwa filamu ya “mapenzi ya Mungu” ya Elizabeth Michael na filamu ya “Kitendawili” ya Single Mtambalike, wameishukuru Serikali kwa kuwathamini na kuonesha ushirikiano katika kazi zao za sanaa, na wameahidi kuendelea kutengeneza kazi nzuri za sanaa ili ziweze kuitangaza Tanzania kimataifa.
Naye, Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania(TAFF) Saimon Mwakifamba ameishukuru Serikali kwa jitihada mbalimbali inazofanya katika kusaidia tasnia ya sanaa kwa ujumla na ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza tasnia hiyo kimataifa.
No comments:
Post a Comment