Vikosi vya upinzani nchini Syria vinavyoungwa mkono na ndege za kivita
za Marekani vimeuzingira mji wa Marea, kaskazini mwa Mkoa wa Allepo na
kuwafurusha wapiganaji wa kundi la IS karibu na mpaka na Uturuki.
Vikosi vya upinzani nchini Syria vinavyoungwa mkono na ndege za kivita
za Marekani vimeuzingira mji wa Marea, kaskazini mwa Mkoa wa Allepo na
kuwafurusha wapiganaji wa kundi la dola la kiislamu IS waliokuwa
wakidhibiti eneo hilo muhimu karibu na mpaka na Uturuki. Wakati huo huo
mawaziri wa ulinzi wa Syria,Iran na Urusi wanakutana mjini Tehran kwa
mazungumzo juu ya hatua zaidi za kupambana na makundi ya wapiganaji.Kwa mujibu wa kundi la uangalizi wa haki za binadamu la nchini Syria, mji wa Marea ulikuwa mikononi mwa wapiganaji wa IS kabla ya kufurushwa na vikosi vya upinzani.
Makundi ya wapiganaji yameuzingira mji huo baada ya kufanya shambulizi la kushutukiza dhidi ya IS baada ya kutoa taarifa kuwa wanaunganisha nguvu. Wamekitwaa kijiji cha Kafr Kalbin katika barabara inayounganisha Marea na Azaz, kilometa 20 kutoka kaskazini magharibi , taarifa hizo ni kwa mujibu wa kundi la uangalizi wa haki za binadamu.
Mkuu wa kundi la uangalizi wa haki za binadamu Rami Abdel Rahman ameliambia shirika la habari la DPA kuwa mji huo umezingirwa.
Mwezi Mei,IS iliuvamia mji huo wa Marea na kukata mawasiliano na mpaka wake na Uturuki.
Eneo la kaskazini mwa Allepo nalo lilikata mawasiliano na kusini mwa Allepo mwezi Februari na vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na majeshi ya angani ya Urusi. Mapigano hayo yamesababisha maelfu ya raia kukwama katika mji wa Marea.
Mazungumzo Tehran
Wakati huohuo Waziri wa ulinzi wa Syria Fahd Jassem al-Freji atakutana na mawaziri wenzake wa Iran na Urusi siku ya alhamis..
Mojawapo ya jengo lililoharibiwa mjini Marea,Allepo.
Urusi imetuma ndege za kivita na vikosi maalumu katika kuunga
mkono utawala wa rais Bashar al-Assad wakati ambapo Iran ikipeleka
washauri wa kijeshi na vifaa kwa wanamgambo wanaoiunga mkono serikali ya
nchi hiyo.Ziara ya waziri huyo wa ulinzi mjini Tehran , inakuja wakati ambao utawala wa Assad ukipiga hatua katika kampeni yake ya kupambana na IS na makundi mengine ya waasi mjini Allepo.
Waziri mwenzake wa Urusi, Sergei Shoigu atahudhuria mkutano huo baada ya nchi yake kuahidi hatua zaidi za kuongeza mashambulizi ya angani dhidi ya waasi nje na ndani ya mji wa Allepo,akishutumu upande wa waasi kwa kushindwa kutekeleza makubaliano ya mwezi februari ya kusitisha mapigano na kukata mafungamano na kundi la Al-Nusra lililo na mafungamano na Al-Qaeda.
Mazungumzo hayo ya mawaziri wa ulinzi yanakuja baada ya mwaliko wa mkuu wa majeshi wa Iran Hossein Dehghan.
Tehran imekuwa ikitoa msaada wa vifaa na fedha kwa serikali ya Syria tangu kuibuke uasi dhidi ya Bashar al-Assad miaka mitano iliyopita.
No comments:
Post a Comment