Umoja wa Ulaya unalenga kusitisha wimbi la wakimbizi wanaoingia Ulaya
wakitokea Afrika. Kwa sababu hiyo, Umoja huo unataka kushirikiana na
mataifa ya Afrika ili yafunge mipaka kuzuia wakimbizi kutoka.
Mkuu wa sera za kigeni katika Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini ni
mmoja wa wanasiasa wanaotaka hatua zozote zile zichukuliwe kupunguza
idadi ya Waafrika wanaokimbilia Ulaya. Yeye anasisitiza kwamba njia
pekee ni kufanya kazi bega kwa bega na Waafrika wenyewe.Katika waraka uliochapishwa na Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, inaelezwa kwamba maelfu ya Waafrika wamekwama nchini Libya wakitafuta njia ya kusafiri mpaka Ulaya. Hata hivyo, mataifa mwanachama wa Umoja wa Ulaya hayana msimamo wa pamoja kuhusu idadi ya wakimbizi wanaoweza kupokelewa na nchi gani zinazotakiwa kubeba jukumu la kuwapokea. Idadi ya Waafrika wanaojaribu kuingia Ulaya inapanda, na wengi wao wanahatarisha maisha yao kwa kuvukua Bahari ya Mediterania wakitaka kuwasili nchini Italia. Nchi za Kiarabu pia zinashirikishwa katika mpango huo.
Wakimbizi waliokamatwa Libya wakitaka kuelekea Ulaya
Umoja wa Ulaya unataka kusaini makubaliano na Jordan, Lebanon,
Tunisia, Nigeria, Senegal, Mali, Ethiopia na Libya. "Tutapendekeza
kutumia mchanganyiko wa njia hasi na chanya kuzipatia msaada nchi ambazo
ziko tayari kushirikiana nasi na kuhakikisha kwamba kutakuwa na athari
kwa wale ambao hawatashirikiana nasi," anaeleza Frans Timmermans, naibu
mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya. "Miongoni mwa mambo
mengine tutatumia sera zetu za maendeleo na biashara kama shinikizo."Wabunge wasema mpango una mapungufu
Nchi zitakazokuwa tayari kuimarisha ulinzi katika mipaka yake na vile vile kuwa tayari kuwapokea wakimbizi watakaonyimwa hifadhi Ulaya na pia kufungua vituo vya kupokea wakimbizi zitaungwa mkono na Umoja wa Ulaya na zimeahidiwa misaada ya kimaendeleo na mikataba bora zaidi ya biashara.
Pamoja na hayo, mpango huu unazitaka nchi za Kiafrika na Kiarabu ziimarishe miundombinu na zikuze uchumi ili raia wasiwe na sababu ya kukimbilia nchi nyingine.
Hata hivyo wapo wabunge wa Umoja wa Ulaya wanaoukosoa mkakati huu. Guy Verhofstadt ni kiongozi wa kundi la wanasiasa wa vyama vya kiliberali katika bunge la Umoja wa Ulaya. Kwa mtazamo wake, si sahihi kuziahidi nchi za Kiafrika na Kiarabu kwamba zitapatiwa pesa iwapo zitakuwa tayari kuwapokea watu waliokataliwa hifadhi ya ukimbizi Ulaya. Badala yake anataka lengo kuu liwe kuboresha maendeleo ya kibiashara na demokrasia. Wanaoupinga mpango huu wanasema hauna tofauti na ule uliofikiwa kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki, ambapo Uturuki inapatiwa fedha kupokea wakimbizi ili wasiingie Ulaya.
No comments:
Post a Comment