Rais wa Ujerumani Joachim Gauck, hatagombea awamu ya pili ya miaka mitano madarakani, ikizingatiwa umri wake na sababu za kiafya. Hayo yameripotiwa na gazeti la Bild Ijumaa (03.06.2016)
Gauck, mwenye umri wa miaka 76, anatarajiwa kutoa maelezo juu ya uamuzi wake wa kutowania muhula wa pili kama mkuu wa dola katika mkutano na kansela wa Ujerumani Angela Merkel siku ya Jumatatu, gazeti hilo liliripoti.
Gauck anatarajiwa kutoa tangazo rasmi kwa umma siku ya Jumanne mjini Berlin. Muhula wa Gauck, unakamilika Machi 2017. Msemaji wa rais huyo amekataa kutoa kauli kuhusu suala hilo. Rais Gauck aliidhinishwa kuwa rais Machi 2012, kuchukua nafasi iliyoachwa na Christian Wulff, ambaye baada ya miezi 20 tu alilazimika kujiuzulu kutokana na kashfa iliyohusisha mkopo wa nyumba.
Mwaka 2010 Gauck alishindwa na rais wa zamani Wulff wakati alipokuwa mgombea wa muungano wa vyama vya Kijani na Social Democratic, SPD. Mwaka 2012 kansela Merkel na muungano wa vyama ndugu vya Christian Democratic Union, CDU na Christian Social Union, CSU, ulimuunga mkono Gauck baada ya mabishano kadhaa.
Mwezi uliopita viongozi wa vyama vinavyounda serikali viliahidi kuunga mkono muhula wa pili wa rais Gauck. Gazeti la Frankfurter Rundschau liliripoti kwamba chama cha Christian Democratic Union, CDU cha kansela Merkel pamoja na mshirika wake serikalini, chama cha Social Democratic SPD, vilihofia athari za Gauck kukataa kugombea awamu ya pili.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, uamuzi huo ungekwamisha kampeni zao za uchaguzi wa shirikisho mwaka 2017, iwapo vyama havitoweza kukubaliana kuhusu mgombea mmoja. Baraza maalumu linalomchagua rais litakutana Februari 12 mwaka ujao 2017.
Wajerumani wataka Gauck aendelee
Matokeo ya kura ya maoni ya hivi karibuni, yanaonyesha asilimia 70 ya Wajerumani wangependelea Gauck aendelee kuwa rais. Kiongozi huyo kwa muda mrefu alikuwa ameliacha wazi suala la ikiwa atagombea awamu ya pili ama la. Wakati alipofanya ziara nchini China mwezi Machi mwaka huu rais Gauck alisema ni hisia nzuri kwamba watu wengi wangependelea kuendelea kufanya kazi yao kwa weledi. "Lakini katika hilo mtu anatakiwa kujifikiria hali yake ya mwili na uwezo wake kisaikolojia," alisema.
Rais wa Ujerumani ni mkuu wa dola na kwa kiwango kikubwa hushikilia wadhifa wa heshima, kuiwakilisha nchi katika masuala ya sheria za kimataifa na mikutano rasmi. Rais hachaguliwi moja kwa moja na umma, bali huchaguliwa na kamati maalumu inayowajumuisha wabunge wa bunge la Ujerumani, Bundestag, na idadi sawa na hiyo ya wajumbe kutoka kwa mabunge ya mikoa.
Rais wa Ujerumani huwa na muhula wa miaka mitano na anaweza kuchaguliwa tena mara moja tu. Raia yeyote wa Ujerumani mwenye umri wa zaidi ya miaka 40, anaweza kugombea urais
No comments:
Post a Comment