Rais wa Ujerumani Joachim Gauck amesema hatawania urais kwa mara nyingine, akikiri kuwa uamuzi huo si mrahisi kwake. Haijafahamika nani atachukua nafasi ya mwanasiasa huyo mashuhuri.
Gauck mwenye umri wa miaka 76 ambaye ni maarufu ameshikilia wadhifa huo ambao si wa kiutendaji tangu mwaka 2012. Ameamua kutokuendelea na wadhifa wake kutokana na afya yake na umri wake mkubwa.
Mwanasiasa huyo ameeleza kuwa ana wasiwasi kuhusu uwezo wa kuendelea kufanya kazi ya urais kwa nguvu inayotakiwa iwapo ataendelea nayo hata baada ya kufikisha miaka 80. “Uamuzi huu haukuwa rahisi kwangu,” alisema katika makao yake kwenye Kasri la Bellevue mjini Berlin. “Sitaki kujitolea kwa miaka mingine mitano bila kuwa na uhakika kwamba nitakuwa na nguvu na afya ya kutosha.”
Hata hivyo amesisitiza kwamba amelitumikia taifa la Ujerumani kwa furaha na heshima kwa miaka minne na kwamba anatazamia kipindi kilichobaki.
Nani atamrithi rais?
Gauck, mchungaji wa kanisa la Protestant, alipata umaarufu kutokana na kuwa mwanaharakati wa haki za binadamu katika iliyokuwa Ujerumani mashariki ya kikomunisti na alitoa mchango muhimu katika vuguvugu ambalo lilisaidia kuanguka kwa ukuta wa Berlin mwaka 1989.
Haijafahamika nani atakayechukua madaraka hayo baada ya Gauck. Baadhi ya watu wanaotajwa kuwa na nafasi nzuri ni Waziri wa Fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble, Waziri wa Mambo ya Nje Frank-Walter Steinmeier, spika wa bunge Norbert Lammert na mwanasiasa wa CSU Gerda Hasselfeldt.
No comments:
Post a Comment