Serikali
imelegeza msimamo wake kuhusu kuondoa misamaha ya kodi kwenye Taasisi
za dini badala yake itaongeza udhibiti ili kuzuia mianya ya matumizi
mabaya ya misamaha hiyo.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ametoa ufafanuzi huo mjini
Dodoma wakati akiongea na vyombo vya habari ili kutoa ufafanuzi wa
baadhi ya hoja zilizotolewa na wabunge wakati wa kujadili bajeti Kuu ya
Serikali iliyopitishwa Juzi na Bunge.
Amesema
kuwa uamuzi huo wa serikali umefuatia maombi na mapendekezo mbalimbali
ya wadau yaliyoitaka serikali iendelee kutoa misamaha ya kodi kwa
Taasisi hizo kutokana na umuhimu wake wa kuisaidia jamii kupitia miradi
mbalimbali inayotekelezwa na taasisi hizo.
“Kwa
kutambua mchango mkubwa wa taasisi mbalimbali za kidini katika utoaji
wa huduma za elimu, afya, maji; nimeamua kufuta utaratibu nilioutangaza
katika hotuba ya bajeti, badala yake serikali itaimarisha zaidi udhibiti
wa misamaha hiyo”Alisema Dkt. Mpango
Alizitaja
baadhi ya hatua zitakazochukuliwa kuzuia mianya ya matumizi mabaya ya
misamaha hiyo kuwa ni kuzitaka Taasisi za dini kuwasilisha orodha ya
vifaa vinavyotarajiwa kununuliwa kutoka nje ya nchi kila mwanzo wa mwaka
wa kalenda, pamoja na kuthibitisha kama vifaa vilivyosamehewa kodi
mwaka uliotangulia vilitumika kwa mujibu wa sheria
Aidha,
utaratibu mpya utazitaka Taasisi hizo za dini kuwasilisha majina ya
watu waliowaidhinisha kuandika barua za maombi ya msamaha wa kodi
zikiainisha cheo, saini, picha, anuani na namba za simu za wahusika.
“Taarifa
hizo ni muhimu katika kuiwezesha TRA kufuatilia bidhaa zilizoombewa na
kupewa misamaha kama zimepata kibali cha Taasisi husika zimetumika na
zimetekeleza miradi iliyokusudiwa” Aliongeza Dkt. Mpango
Dkt.
Mpango alisema katika utaratibu huo mpya, wameweka masharti ya
kuzilazimisha Taasisi hizo za dini kuiandikia serikali barua ya
kumuidhinisha wakala wa forodha waliyemteua kutoa bandarini mizigo
itakayokuwa ikiagizwa kutoka nje
Alizitaja
hatua nyingine kuwa ni wakati wa kuomba msamaha wa kodi katika bidhaa
zinazoingizwa nchini, Taasisi za dini zitalazimika kupata barua ya
uthibitisho kutoka kwa Afisa Mtendaji wa serikali ya Mtaa ama kijiji na
mkuu wa wilaya mahali Taasisi au Mradi ulipo ili kuthibitisha uwepo wa
Taasisi au mradi na mahitaji ya vifaa vinavyoombewa msamaha
Dkt.
Mpango alifafanua kuwa magari yatakayoingizwa kwa msamaha wa kodi
yatalazimika kuwa na rangi pamoja na namba maalumu za utambuzi mfano TEV
222 AXZ kama njia ya kudhibiti matumizi yake.
No comments:
Post a Comment