Jinai za muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia zimeendelea nchini Yemen kufuatia ndege za kivita za Saudia kushambulia maeneo ya makazi ya raia kusini mwa nchi hiyo.
Kwa upande wao jeshi na vikosi vya wananchi w Yemen vimeendelea kupambana na wavamizi pamoja na magenge ya kigaidi kwa kushambulia maeneo ya magaidi wa al Qaida katika mji wa Zinjibar, makao makuu ya mkoa wa Abyan wa kusini mwa Yemen na kuwalazimisha magaidi wanaoungwa mkono na Saudia kukimbia katika baadhi ya maeneo muhimu na majengo ya serikali. Makundi mawili ya kigaidi na kitakfiri ya al Qaida na Daesh (ISIS) yamefanya jinai nyingi nchini Yemen katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wa tangu Saudia kuivamia nchi hiyo ya Kiarabu. Aidha yamesababisha hasara kubwa za roho na mali za watu nchini humo. Tangu mwaka 2014, vikosi vya wananchi wa Yemen vinadhibiti mji mkuu wa Yemen, Sana'a na maeneo mengi ya nchi hiyo. Hali hiyo inashuhudiwa katika hali ambayo tangu mwanzoni mwa mwaka jana vikosi vya Abdu Rabuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu na kukimbia nchi vinadhibiti mikoa mitano ya kusini mwa Yemen kwa msaada wa Saudia na Marekani. Wakati huo huo duru za kijeshi za Yemen zimetangaza kuwa, makumi ya wanajeshi wa Abdu Rabuh Mansour Hadi wameuawa katika maeneo ya kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Maafisa hao wa Yemen wamesema, raia 45 wa nchi hiyo wameuawa kwa umati katika shambulio la vikosi vya Mansour Hadi kwenye bandari ya Midi ya Bahari Nyekundu. Huku hayo ya kiripotiwa, vikosi vya wananchi wa Yemen vinaendelea kusonga mbele kuelekea kwenye Bahari Nyekundu na kuwazingira mamluki wa Saudi Arabia nchini humo. Naye Muhammad Ali al Houthi, Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen ametaka kukomeshwa mzingiro wa kiuchumi dhidi ya nchi hiyo kwani wananchi wasio na hatia wanaendelea kuteseka. Amesema hayo wakati alipoonana na Jamie McGoldrick, mratibu wa masuala ya misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen na kusisitizia udharura wa kupelekewa chakula na madawa wananchi wa Yemen waliozingirwa kinyume cha sheria na kinyume na ubinadamu. Tangu mwaka mmoja nyuma Saudi Arabia kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu, Marekani na utawala wa Kizayuni, imekuwa ikifanya mashambulizi makubwa nchini Yemen kwa madai ya kumrudisha madaraka Abdu Rabuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Saudia. Hata hivyo hadi leo hii Saudia na wenzake wameshindwa kufanikisha chochote zaidi ya jinai, ukatili, chuki na uharibifu wa kuchupa mipaka nchini Yemen. Saudia ilimlazimisha Mansour Hadi aunde serikali nje ya Yemen, serikali ambayo makao yake ni Riyadh, Saudi Arabia. Serikali hiyo imeshindwa na kufeli vibaya kiasi kwamba habari zinasema kuwa, mawaziri kadhaa wa serikali hiyo wameomba hifadhi ya ukimbizi katika nchi za Ulaya. Wachambuzi wa mambo kama vile Abdel Bari Atwan mhariri mkuu wa gazeti maarufu la Rai al Youm la mjini London Uingereza ameandika katika makala yake moja kuwa, baada ya kushindwa kupata njia za kurejea madarakani nchini Yemen, mawaziri wa serikali ya Mansour Hadi wameamua kutafuta ukimbizi katika nchi za Ulaya. Aidha katika makala hiyo amegusia uvamizi wa Saudi Arabia nchini Yemen ambao Saudia imeupa jina la "Tufani Ngangari" na kusema kuwa matunda pekee ya "Tufani Ngangari" hiyo ni kuongezeka chuki na hasira za wananchi wa Yemen dhidi ya Saudia. Maelfu ya wananchi wa Yemen wameuawa na kujeruhiwa pamoja na kupoteza makazi yao katika kipindi cha mwaka mmoja wa mashambulizi ya kivamizi ya Saudia na wenzake huko Yemen.
No comments:
Post a Comment