Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amelitaka Jeshi la Polisi nchini na Ofisi ya Mwendesha Mashitaka kujirekebisha kwa kutekeleza wajibu wao huku wakitanguliza maslahi ya taifa.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo jana tarehe 29 Aprili, 2016 wakati akifungua kikao cha kazi cha Makamanda wa polisi wa mikoa, Mawakili wafawidhi wa serikali wa Mikoa na Wakuu wa upelelezi wa Mikoa na Vikosi, kinachofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Mikutano wa Dodoma uliopo katika eneo la Tambukareli Mjini Dodoma.
Awali kabla ya kutoa hotuba yake Rais Magufuli aliwapa nafasi Makamanda na Mawakili Wafawidhi hao kutoa maoni yao juu ya changamoto zinazowakabili katika kutekeleza wajibu wa kufanya upepelezi na kuendesha mashitaka, hususani kujua sababu za kuchelewesha kesi za makosa ya jinai, ambapo wamedai ufinyu wa bajeti ndio sababu kubwa ya kucheleweshwa kwa kesi za hizo.
Kufuatia kutajwa kwa changamoto hiyo Rais Magufuli ameahidi kuhakikisha anawatafutia fedha kwa ajili ya kukabiliana nazo, lakini ametaka fedha zitakazotafutwa zitumike vizuri kwa kuwa taarifa zinaonesha Jeshi la Polisi limekuwa likihusishwa na matumizi mabaya ya fedha hali inayoongeza ukubwa wa matatizo yanayokwamisha utendaji wake wa kazi.
Ametolea mfano wa taarifa za matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya kununulia vifaa na sare za askari, ama mikataba yenye mashaka inayotiwa saini kati ya Polisi na wawekezaji kuwa ni baadhi ya mambo yanayoongeza hali ngumu ya utendaji kazi kwa jeshi hilo.
"Oysterbay pale ni eneo ambalo ni very prime, kila mmoja anajua, mmeingia kwenye mikataba mnayoijua nyinyi, akapewa mtu anawajengea pale, sifahamu kama majengo hayo yanafaa. Palikuwa na ubaya gani eneo la Oysterbay likawa na hati, mkaitumia hiyo hati kwenda kukopa benki na kujenga nyumba hata za ghorofa 20 pale, mkaweka investment na Polisi wenu wakakaa pale. Nimesema lazima nizungumze kwa uwazi, nisiposema kwa uwazi nitajisikia vibaya nikimaliza mkutano huu, nataka muelewe na muelewe ukweli direction ninayoitaka mimi" Amesema Rais Magufuli
Aidha, Rais Magufuli ameitaka Ofisi ya Mwendesha Mashitaka kujipanga kufanya kazi kwa ufanisi na ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya serikali kushindwa katika kesi nyingi mahakamani licha ya kuwa na wanasheria mahiri.
"Niwaombe mawakili na polisi wanaohusika na upelelezi mtangulize maslai ya nchi mbele, kwa sababu kumekuwa na usemi kwa baadhi ya wapelelezi na mawakili wachache, nasema wachache, panapokuwa na kesi inayohusiana na pesa pesa, wana misemo yao wanasema dili limepatikana, na saa nyingine kesi inapopelekwa mahakamani wana-collude Mawakili wa serikali na mawakili wanaomtetea mhalifu, na wanapo-collude siku zote serikali inashindwa. Unapoona hali hiyo ya kila siku serikali inashindwa, halafu siku hiyo unataka serikali ikuwezeshe, kwa vyovyote serikali inapata kigugumizi" amesisitiza Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli pia amelitaka Jeshi la Polisi kujiepusha na kashfa ambazo zimekuwa zikisemwa dhidi yake, ikiwemo maafisa wa Polisi kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kuazimisha silaha kwa wahalifu wa ujambazi.
Hata hivyo Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kwa kazi kubwa wanayoifanya na ametaka apelekewe mpango wa mahitaji yao ili atafute namna ya kuimarisha vyombo hivyo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
No comments:
Post a Comment