Kumekuwepo na utulivu wa mashaka katika mji wa kaskazini wa Syria wa Aleppo Ijumaa, wiki moja baada ya mapigano kuuwa raia 123 wakiwemo watoto 18 pamoja na shambulio dhidi ya hospitali liloua watu 30.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelitaja shambulio hilo kuwa ni kisingizio kisichukubalika kinachokiuka sheria ya kimataifa. Mohamed al-Shami mwanaharakati aliyeko katika eneo linaloshikiliwa na waasi katika mji huo wa Aleppo amesema mazingira ya hofu yameugubika mji huo wakati watu wakitarajia mashambulizi zaidi ya anga kutoka kwa serikali na washirika wake.
Ameongeza kusema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Facebook kwamba sala ya Ijumaa imefutwa takriban katika misikiti yote kwa kuhofia mashambulizi zaidi.
Takriban watu 30 wakiwemo madaktari watatu wameuwawa hapo jana katika mashambulizi ya anga yanayoaminika kutekelezwa na serikali na mshirika wake Urusi katika hospitali ya al- Quds katika kitongoji kinachodhibitiwa na waasi cha al-Sukari katika mji huo wa Aleppo.
Miongoni mwa waliouwawa katika shambulio hilo la siku katika hospitali ya al-Quds ni pamoja na daktari pekee wa watoto aliebakia katika hospitali hiyo na watoto watatu.
Shambulio la hospitali halikubaliki
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani shambulio la hospitali ya Aleppo na kusema kwamba mashambilizi yanayowalenga raia ni kisingizio kisichokubalika kinachokiuka sheria ya kimataifa.
Ban amesema katika taarifa lazima kuwepo uwajibikaji kwa uhalifu huo dhidi ya hospitali inayosaidiwa na Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka MSF.
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametowa wito kwa pande zinazohasimiana kujitolea upya mara moja kwa usitishaji wa mapigano ambao umekuwa ukitekelezwa tokea mwishoni mwa mwezi wa Februari.
Pia ameyashajiisha mataifa yenye nguvu yanayounga mkono mchakato wa amani wa Syria hususan Marekani na Urusi kuhakikisha kunafanyika uchunguzi wa kuaminika kwa matukio kama shambulio hilo la hospitali ya al-Quds.
Ameongeza kusema kwamba badala ya kushambulia maeneo ya raia kwa mabomu, wahusika wote wa mzozo wa Syria lazima waelekeze upya nadhari yao kwa mchakato wa kisiasa.
Kufufuwa usitishaji wa mapigano
Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya misaada Stephen O'Brien naye ametowa wito kwa mataifa makubwa duniani kufufuwa usitishwaji wa mapigano na kukomesha mateso makubwa kabisa ya binaadamu nchini Syria.
Ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa mkutano juu ya hali ya kutisha ya kibinadamu kutokana na vita vya miaka mitano nchini Syria kwamba lazima wote waone aibu kwa kile kinachotokea mbele ya macho yao.
Nchi tano za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Misri, Japani, New Zealand, Uhispania na Uruguay zinarasimu azimio jipya lenye kulaani mashambulizi dhidi ya hospitali katika maeneo ya vita kama vile Syria, Yemen, Afghanistan na Sudan Kusini.
Rasimu ya azimio hilo inatarajiwa kupigiwa kura wiki ijayo katika hatua ambayo itatuma ujumbe mkali kabis kuhusu suala hilo.
No comments:
Post a Comment