Wednesday, April 13, 2016

Wapinzani wa Congo DR waunga mkono azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa


Wapinzani wa Congo DR waunga mkono azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Wapinzani wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamesema kuwa, wanaunga mkono azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kufanyike uchaguzi wa nchi hiyo katika muda uliopangwa.
Olivier Kamitatu, mmoja wa wajumbe wa kundi la G7 linaloundwa na vyama sabata vya siasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na ambaye hapo kabla alikuwa muitifaki wa Rais Joseph Kabila amesema kuwa, serikali ya Kinshasa inapaswa kuheshimu azimio hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka uchaguzi mkuu wa nchi hiyo ufanyike katika muda uliopangwa.
Msimamo huo wa wapinzani wa serikali ya Kinshasa unakuja kufuatia matamshi ya Raymond Tshibanda, Waziri wa Mashauri ya Kigeni na Lambert Mende Omalanga ambaye ni Waziri wa Mawasiliano ambao wamelilaani azimio nambari 2277 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalosisitiza juu ya udharura wa kufanyika uchaguzi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo katika tarehe iliyopangwa yaani Novemba mwaka huu. Raymond Tshibanda amesema kuwa, azimio hilo linaloitaka serikali ya Kinshasa kuitisha uchaguzi katika muda ulioainishwa sio la kuwajibika.
Wiki iliyopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitaka serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufanya uchaguzi ujao katika muda uliopangwa. Pamoja na hayo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa, azimio hilo la Baraza la Usalama litapelekea kushadidi machafuko na mivutano katika nchi hiyo.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, endapo uchaguzi wa DRC utafanyika kwa mafanikio, basi jambo hilo litakuwa ni hatua moja mbele katika mchakato wa kukabidhi madaraka kwa njia ya amani na utulivu.
Rais Joseph Kabila mwenye umri wa miaka 44 na ambaye yuko madarakani kwa miaka kumi na tano sasa, haruhusiwi na katiba kugombea tena kiti hicho katika uchaguzi ujao. Muhula wa uongozi wa Rais Kabila unafikia tamati Novemba 19 mwaka huu. Hata hivyo harakati za kiongozi huyo zinaonesha kuwa, anataka kutafuta njia ya kugombea tena uchaguzi ujao ili aendelee kubakia madarakani. Baada ya kambi ya upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kujitokeza na kupinga hatua yoyote ya Rais Kabila kubakia madarakani, chama tawala kimeanza kutoa visingizio hivi na vile likiwemo suala la ukosefu wa bajeti ya kuendeshea zoezi la uchaguzi huo. Mwezi uliopita Kamisheni ya Uchaguzi ya Congo Kinshasa iliitaka Mahakama ya Katiba isogeze mbele tarehe kufanyika uchaguzi huo ambayo ni Novemba 27 mwaka huu.
Wapinzani wanaamini kuwa, serikali inatoa visingizio hivyo ili kukwamisha kufanyika uchaguzi mkuu katika wakati uliopangwa na kutoa mwanya kwa Rais Joseph Kabila wa kusalia madarakani. Suala hilo limekuwa likizidisha mashinikizo na wimbi la upinzani dhidi ya Rais Kabila; kiasi kwamba hivi karibuni kiongozi huyo alitoa wito wa kufanyika mazungumzo kati ya serikali na wapinzani. Hata hivyo vyama vya upinzani vimekataa kuketi kwenye meza ya mazungumzo.
Wiki iliyopita, Umoja wa Afrika AU ulimteua Edem Kodjo, Waziri Mkuu wa zamani Togo kuwa mpatanishi katika mazungumzo ya kitaifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Weledi wa mambo wanaamini kwamba, kupelekwa silaha nyingi na suhula za kijeshi katika maeneo ambayo hayana mapigano kumekuwa na taathira hasi kwa hali ya usalama wa nchi. Hali hiyo inatia wasiwasi mno hasa kutokana na kuweko upinzani mkali dhidi ya kuendelea kubakia madarakani Rais Joseph Kabila kwa upande mmoja na kukaribia kufanyika uchaguzi katika nchi hiyo kwa upande wa pili.
Unknown Web Developer

Morbi aliquam fringilla nisl. Pellentesque eleifend condimentum tellus, vel vulputate tortor malesuada sit amet. Aliquam vel vestibulum metus. Aenean ut mi aucto.

No comments:

Post a Comment