Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha ijumaa hii kwa kauli moja azimio linalomwomba Katibu Mkuu Ban Ki-moon kujadiliana na serikali ya Burundi, Muungano wa Afrika na wadau wa kikanda ili kutuma vikosi vya polisi vya Umoja wa Mataifa nchini humo.
Kwa mujibu wa azimio hilo lililotayarishwa na Ufaransa, lengo ni kuimarisha usalama, utawala wa sheria na kulinda haki za binadamu nchini Burundi.
Wakisisitizia hali ya vurugu, mkwamo wa kisiasa na mzozo wa kibinadamu nchini Burundi, wanachama wa Baraza la Usalama wamempa Katibu Mkuu siku kumi na tano kabla awasilishe mapendekezo yake ili kuimarisha timu ya mshauri wake maalum nchini humo, Jamal Benomar.
Halikadhalika, wamekaribisha uamuzi wa Burundi wa kuruhusu ujumbe wa wataalam wa haki za binadamu na masuala ya kijeshi wa Muungano wa Afrika kufanya uchunguzi nchini humo, wakizisihi serikali ya Burundi na wadau wengine kuharakisha usambazaji wao.
Hatimaye wanachama wa Baraza hilo wamelezea nia yao ya kutazamia harakati zozote zitakazoweza kuchukuliwa dhidi ya watu waliopo ndani na nje ya Burundi ambao wanachangia katika kuendeleza vurugu nchini humo.
No comments:
Post a Comment