Wednesday, June 22, 2016

Ugomvi wa Wabunge wa CCM na UKAWA Wafikia Pabaya........UKAWA Wakataa Kusalimiwa, Wenye Wapenzi CCM watakiwa Kuwaacha

Sakata la wabunge wa Ukawa kususa vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson limefika pabaya baada ya baadhi ya wawakilishi hao kuanza kutowasalimia baadhi ya wabunge wa CCM.

Hatua hiyo ilikuwa dhahiri jana baada ya Ukawa kutangaza kuwa hawatashirikiana na wabunge wenzao wa chama tawala katika shughuli za kawaida za kijamii, kama vile michezo na kutumia kantini ya Bunge, wakisema wenzao wameanza kuwabagua.

Mbali na kitendo hicho, wabunge hao pia walitoka kimyakimya bungeni baada ya Dk Tulia kuingia, lakini safari hii hawakufanya mbwembwe za kujiziba midomo kama walivyofanya juzi.

Jana asubuhi, mbunge wa CCM  Kangi  Lugola alisema  kuwa alisikitishwa  baada ya kudai kuwa Mbunge wa Chadema (Viti Maalumu), Lucy Magereli hakumjibu salamu yake wakati akiingia bungeni licha ya kumsalimia mara tatu na kuwa katika umbali mfupi wa kusikika.

“Kusalimia ni jambo la utamaduni wetu. Nilikuwa namsalimia mbunge wa kike wa Ukawa, lakini hakujibu. Lakini, nikajua ni sababu ya wao kufunga mdomo na plasta, nikamtania au kwa sababu ya plasta hujibu ili isije kudondoka hakuitikia,” alisema Lugola.

Alisema ameshtushwa na hali ilipofikia na hajui sababu za msingi za wabunge wa Ukawa kufanya vitendo hivyo, kinyume na udugu na utamaduni wa Watanzania.

Mbunge huyo machachari, alisema Kubenea alimziba mdomo Msigwa kwa mkono ili asizungumze chochote.

Naye mbunge wa  Sumve (CCM ) Richard Ndassa  alisema jambo wanalolifanya wabunge wa Ukawa siyo jema na halina tija kufanywa na wawakilishi hao wa wananchi.

“Sisi ni wabunge, hivi inapofikia kususa kuongea na wabunge wenzako, hatima yake nini?” alisema.

“Mimi nilienda kuwasalimia kama kawaida ambavyo huwa tunafanya kwa wabunge awe CUF, CCM au Chadema, sasa unavyosusa una maanisha nini,” alilalamika Ndassa.

Alisema kitendo cha kutosalimia ni cha juu sana na kwamba iwapo Ukawa wanashauriwa na mtu basi inawapasa kuchuja mambo mengine, likiwamo hilo la kuwasusa wabunge wenzao.

Juzi Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia wakati anawaongoza wabunge wa Ukawa kutoka bungeni aliwatuhumu wabunge wenzao wa CCM kuwa wanawabagua
Naye Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea   alisema;   “Leo  tumekubaliana hatutashiriki katika michezo na wabunge wa CCM, hilo tumeanza leo asubuhi kwenye mazoezi katika viwanja mbalimbali, hivi sasa tunatafakari hata kutafuta uwanja wetu.

“Tukikutana katika uwanja mmoja, sisi tutatumia upande mmoja na wao watatumia upande mwingine, hatuchanganyani, hata salamu leo kuna mmoja kanisalimia nimekwepesha mkono wangu,”
 
Kubenea alisema hata katika mechi zinazoandaliwa kwa ajili ya timu ya wabunge UKAWA hawatashiriki katika kipindi hiki cha wiki mbili zilizobakia za bajeti.
 
“Si katika michezo tu, hata katika mahusiano, tumekubaliana kama kuna wabunge wana mahusiano ya kimapenzi na wabunge wa CCM yasitishwe kwa muda wa wiki mbili mpaka tutakavyoamua vinginevyo,” alisema Kubenea.

Serikali Yarejesha Misamaha Ya Kodi Kwa Taasisi Za Dini, Yatoa Masharti Mazito

Serikali imelegeza msimamo wake kuhusu kuondoa misamaha ya kodi kwenye Taasisi za dini badala yake itaongeza udhibiti ili kuzuia mianya ya matumizi mabaya ya misamaha hiyo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ametoa ufafanuzi huo mjini Dodoma wakati akiongea na vyombo vya habari ili kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizotolewa na wabunge wakati wa kujadili bajeti Kuu ya Serikali iliyopitishwa Juzi na Bunge.

Amesema kuwa uamuzi huo wa serikali umefuatia maombi na mapendekezo mbalimbali ya wadau yaliyoitaka serikali iendelee kutoa misamaha ya kodi kwa Taasisi hizo kutokana na umuhimu wake wa kuisaidia jamii kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na taasisi hizo.

“Kwa kutambua mchango mkubwa wa taasisi mbalimbali za kidini katika utoaji wa huduma za elimu, afya, maji; nimeamua kufuta utaratibu nilioutangaza katika hotuba ya bajeti, badala yake serikali itaimarisha zaidi udhibiti wa misamaha hiyo”Alisema Dkt. Mpango

Alizitaja baadhi ya hatua zitakazochukuliwa kuzuia mianya ya matumizi mabaya ya misamaha hiyo kuwa ni kuzitaka Taasisi za dini kuwasilisha orodha ya vifaa vinavyotarajiwa kununuliwa kutoka nje ya nchi kila mwanzo wa mwaka wa kalenda, pamoja na kuthibitisha kama vifaa vilivyosamehewa kodi mwaka uliotangulia vilitumika kwa mujibu wa sheria

Aidha, utaratibu mpya utazitaka Taasisi hizo za dini kuwasilisha majina ya watu waliowaidhinisha kuandika barua za maombi ya msamaha wa kodi zikiainisha cheo, saini, picha, anuani na namba za simu za wahusika.

“Taarifa hizo ni muhimu katika kuiwezesha TRA kufuatilia bidhaa zilizoombewa na kupewa misamaha kama zimepata kibali cha Taasisi husika zimetumika na zimetekeleza miradi iliyokusudiwa” Aliongeza Dkt. Mpango

Dkt. Mpango alisema katika utaratibu huo mpya, wameweka masharti ya kuzilazimisha Taasisi hizo za dini kuiandikia serikali barua ya kumuidhinisha wakala wa forodha waliyemteua kutoa bandarini mizigo itakayokuwa ikiagizwa kutoka nje

Alizitaja hatua nyingine kuwa ni wakati wa kuomba msamaha wa kodi katika bidhaa zinazoingizwa nchini, Taasisi za dini zitalazimika kupata barua ya uthibitisho kutoka kwa Afisa Mtendaji wa serikali ya Mtaa ama kijiji na mkuu wa wilaya mahali Taasisi au Mradi ulipo ili kuthibitisha uwepo wa Taasisi au mradi na mahitaji ya vifaa vinavyoombewa msamaha

Dkt. Mpango alifafanua kuwa magari yatakayoingizwa kwa msamaha wa kodi yatalazimika kuwa na rangi pamoja na namba maalumu za utambuzi mfano TEV 222 AXZ kama njia ya kudhibiti matumizi yake.

Alionya kuwa Taasisi ya dini itakayothibitika kutumia vibaya msamaha wa kodi itafutiwa usajili wake

Mtanzania Mwingine Akamatwa kwa Kumtukana Rais Kupitia "WhatsApp"

Mkazi wa Dar es Salaam, Leornad Kyaruzi amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka la kutoa lugha ya kumdhalilisha Rais John Magufuli.

Kyaruzi alifikishwa katika Mahakama hiyo na kusomewa shtaka linalomkabili mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Magreth Bankika.

Akisoma hati ya mashtaka, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Wankyo Simon alidai mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Juni 2, mwaka huu katika jengo la Tanzania Tower lililopo Barabara ya Sam Nujoma.

Mwendesha mashtaka huyo alidai siku hiyo, mshtakiwa aliandika kupitia simu yake ya mkononi ujumbe wenye lugha ya kumdhalilisha Rais Magufuli na kisha kuusambaza kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp wakati akijua kuwa ni kinyume cha sheria.

Mshtakiwa alikana shtaka hilo na Hakimu Bankika alimtaka kuwa na mdhamimi mmoja kutoka taasisi inayotambuliwa kisheria ambaye atasaini dhamana ya Sh5 milioni na kufanikiwa kutimiza sharti hilo, hivyo kuachiwa kwa dhamana.

Awali, upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakalika na kuiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine. Hakimu Bankika aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 18, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Wakati huohuo, kitendo cha baadhi ya wadau kumchangia Issack Habakuki aliyepatikana na hatia ya kumtukana Rais Magufuli mkoani Arusha, kilitinga bungeni baada ya wabunge kuitaka Serikali kutoa maelezo ya kina iwapo hakimdhalilishi kiongozi huyo wa juu nchini.

Mwongozi huo uliombwa na Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia akimtaka Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe atolee ufafanuzi jambo hilo.

Mahakama mkoani Arusha ilimtia hatiani kijana huyo mapema mwezi huu kwa kumtukana Rais katika ukurasa wake wa Facebook na kumhukumu kulipa faini ya Sh7 milioni au kwenda jela miaka mitatu na wiki iliyopita, wakazi wa Arusha walimchangia Sh4.5 milioni kukamilisha faini hiyo.

Waziri Dk Mwakyembe alisema suala hilo ni zito linalomgusa Rais na kuomba Naibu Spika Dk Tulia Ackson kumruhusu kwenda kufanya mashauriano na kumpa nafasi ya kuja kutoa msimamo wa Serikali katika mkutano huu unaomalizika Julai Mosi.

Askofu Gwajima Kusakwa na Interpol Popote Alipo

Siku moja baada ya wakili wa Askofu wa kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, Peter Kibatala kuwaandikia barua Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda Simon Sirro amesema hawafanyi kazi kwa kufuata barua ya askofu huyo. 
Sirro alithibitisha kupata barua hiyo, lakini akasema kuwa wanaendelea kumtafuta popote pale alipo na wakifahamu watamtia nguvuni.

Sakata la kutafutwa kwa kiongozi huyo linazidi kushika kasi kutokana na sintofahamu ya kubaini alipo, ikiwamo kambi ya muda wa saa saba iliyowekwa na polisi nyumbani kwa Gwajima, ambayo haikuwa na mafanikio wiki iliyopita.

Baada ya sintofahamu ya wiki nzima huku kukiwa na uvumi kuwa yupo nje ya nchi na wengine wakidai yupo nchini, juzi wakili Kibatala aliwasilisha barua Polisi akidai mteja wake yupo nje ya nchi na aliposafiri hakuwa anajua kama anatafutwa na polisi.

Katika barua hiyo Kibatala alisema ameelekezwa na mteja wake kufikisha ujumbe huo na akirejea atajisalimisha polisi kuitikia wito huo.

Jana Kibatala alisisitiza kuwa: “Kwa sasa yupo nje ya nchi akihubiri injili, alisafiri kabla ya kupata taarifa kuwa anatafutwa na polisi ana mashauri katika Mahakama ya Kisutu Julai Mosi, hivyo kabla ya hapo atakuwa amesharejea.”

Lakini Sirro alisema barua hiyo ni kujitetea ambako hakuna maana na wanachofanya wao ni kuendelea kumtafuta badala ya kusubiri ajisalimishe kama ulivyoandikwa waraka huo.

“Suala la kutupa taarifa za kujifanya alikuwa hafahamu kama anatafutwa si kweli, tukifahamu mahali alipo hata sasa hivi tunakwenda kumkamata, hatufanyi kazi kwa kufuata maelekezo yake,” alisema Kamanda Sirro.

Sirro alifafanua kuwa bado wanafuatilia kubaini kama yupo nchini au nje ya nchi, wakitambua ni nje nchi atakamatwa huko huko kwa msaada wa Interpol.

“Hatujafahamu alipo hata huko nje Interpol wapo kuwashughulikia watu kama hawa wanaofanya ukorofi nchini na kukimbilia nje ya nchi wakidhani wanatatua tatizo, kumbe wanaliahirisha,” alisema Sirro.

Tuesday, June 21, 2016

Nape: CCM Imejaa Majipu

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema ndani ya chama hicho tawala kuna majipu mengi yanayohitaji kutumbuliwa. 

Kwa mujibu wa katibu huyo wa uenezi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi, hatua hiyo ndiyo njia pekee ya kuleta mapinduzi na mageuzi ndani ya chama hicho. 
Amesema chama hicho kilishaingiliwa na makolokolo, hivyo yanahitaji kusafishwa yote kwa mustakabali wake. 
Kauli ya Nape ni sawa na ile iliyowahi kutolewa na viongozi wakuu wa nchi. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan mwanzoni mwa mwaka huu akiwa mkoani Tanga alisema ndani ya CCM kuna watu majipu ambao wameficha makucha ili wasijulikane uovu wao. 
Siku ambayo Rais John Magufuli alipewa cheti na Tume ya Uchaguzi (NEC) baada ya kushinda uchaguzi alikwenda kwenye ofisi ndogo za CCM Lumumba na kuhutubia huku akisisitiza kuwa ndani ya chama hicho kuna watu wanafiki. 
Nape anasema pamoja na kutumbua majipu, chama hicho pia kinahitaji kujitathimini muundo wake kwa kuwa uliopo sasa ni mkubwa na hauendani na hali halisi ya kipato cha chama.
“Muundo wetu ni mzigo mzito unaongeza urasimu. Kwa mfano wajumbe wa NEC hivi sasa wapo zaidi ya 400 ni mzigo mkubwa kwa chama matokeo yake walitumia fursa kutafuta ubunge, inahitaji marekebisho makubwa kwa kuwa uchumi wa chama ni mdogo kwa sasa, tunategemea ruzuku tu. "- Nape
Alisema hata katika upande wa watumishi wa chama wapo wengi sana na wote si wanasiasa, robo tu ndiyo wanasiasa.

Kwa mujibu wa Nape, kwa sasa kinachohitajika ni kutengeneza chama kidogo ili gharama ya kuendesha iwe ndogo. 
Alisema sababu nyingine ya kusafisha chama kutokana na urasimu uliopo; “Lazima tupunguze mlolongo wa vikao vya kutoa maamuzi lakini pia tuangalie upya sera na taratibu zetu.” 
 Akizungumzia watu wenye tabia ya kuhama vyama kama ilivyotokea kwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa na kundi lake, Nape alisema yeye si muumini wa hilo.

“Mimi siamini katika kuhama  vyama ni sawa na kumsilimisha Papa. Kwangu kuchukua watu kutoka upinzani ni sawa na gari zima kuwekewa vifaa chakavu. Watanzania waliopo katika vyama vya siasa hawazidi milioni 10 kwa nini tunyang’anyane wakati kuna zaidi ya watu milioni 45."- Nape

Akizungumzia utendaji wa Rais John Magufuli, Katibu huyo wa uenezi wa chama hicho anayetarajia kustaafu hivi karibuni katika mkutano mkuu alisema ameanza vizuri na kwamba mtindo wake wa kutumbua majipu ndiyo hasa ulikuwa ufanyike baada ya wananchi kukosa imani na Serikali kwa muda mrefu.
 “Yanayotekelezwa hivi sasa na Rais Magufuli ni ripoti yetu. Baada ya kuzunguka nchi nzima tuligundua mambo mengi na ili kukiweka salama chama hatuna budi kuhakikisha tunasafisha uozo wote. 

“Ilifika wakati wawekezaji wamechukua ardhi hawaitumii, wananchi hawana ardhi tena matokeo yake ni migogoro kila kukicha, walimu wanadai haki yao watu wenye mamlaka hawatimizi wajibu wao matokeo yake kukaanza kujengeka hisia kwamba walimu ni wapinzani.

 "Hivi mtu anakuwaje mpinzani kama anadai haki yake? Mlipe kwanza haki yake uone kama ataendelea na malalamiko,” alisisitiza Nape ambaye aliingia rasmi katika siasa akiwa kijana mdogo wa miaka 20 tu. 
Alisema Rais Magufuli amerejesha heshima kwani nchi ilifika mahali ambapo wezi wa mali ya umma walionekana ndiyo wajanja na wale ambao walikuwa wana maadili walionekana legelege. 
Alisema jamii ilipotea na Taifa lilikuwa likijenga jamii ya ajabu ya watu mafisadi, wezi na wasioogopa mali ya umma na hawakuwa na wa kuwazuia kufanya wanavyotaka. 
 Akizungumzia mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya chama chake uliofanyika mkoani Dodoma mwishoni mwa mwaka jana Nape alisema vikao vilikuwa vya moto sana. 
“Wakati mwingine tulikaa katika mkutano mpaka saa tisa usiku na hata mkitoka hamtazamani usoni kila mmoja anaingia katika gari na kuondoka, palichemka sana.” 
Hata hivyo, Nape alisema anashukuru Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Jakaya Kikwete kwa kuwa na kifua na hiyo ndiyo siri ya kufanikisha mchakato huo. 
Alisema Kikwete ni mtoto wa CCM hivyo ilikuwa rahisi kumkata yeyote kwani uzoefu wake ndani ya chama ulisaidia na kwamba itachukua muda mrefu kupata kiongozi kama yeye lakini pia hawawezi kupuuza kazi iliyofanywa na Katibu Mkuu wa chama hicho Abdulrahman Kinana. 
“Ukongwe ulituvusha lakini pia wazee wakarekebisha mambo tukavuka salama, hali ilikuwa mbaya lakini ndiyo demokrasia,” alisisitiza Nape ambaye ni mtoto wa mwanasiasa mkongwe, marehemu Moses Nnauye. CCM itafanya mkutano mkuu Julai 23 mwaka huu.

Wataalamu wa Prescion Air na TCAA Waelekea Zanziba r Kuchunguza Tukio la Ndege Kuwaka Moto

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), wakishirikiana na mafundi wa Kampuni ya Ndege ya Prescion Air wameelekea Zanzibar kuchunguza tukio la ndege ya kampuni hiyo kupata hitilafu na kuwaka moto na kusitisha safari.

Tukio hilo lilitokea Juni 16 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Karume mjini Zanzibar. 
Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Mawasiliano wa Prescion Air, Azda Mkullo inasema wamepeleka injini mbadala kwa ajili ya kufungwa.

Inaongeza kuwa baada ya tukio hilo ilimlazimu rubani kuchukua hatua za kuuzima moto na kuirudisha ndege kwenye eneo la maegesho. 
Ndege hiyo wakati ikipata hitilafu ilikuwa imefanya safari zake kati ya Kilimanjaro na Dar es Salaam.Ndege hiyo PW432 ilikuwa na abiria 34 na wahudumu wanne wote walitoka salama.