Monday, August 8, 2016

BAVICHA Waunga Mkono Oparesheni UKUTA........Wasema Maandalizi Yote Yamekamilika, Wasisitiza Kutorudi Nyuma Septemba Mosi


BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), limetangaza kuunga mkono operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta (Ukuta) iliyotangazwa hivi karibuni na Kamati Kuu ya chama hicho.

Aidha, Bavicha wamemjibu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwamba hana mamlaka ya kuzuia operesheni hiyo kwa kuwa wanaifanya kisheria na yeye siyo msajili wa vyama vya siasa.

Makonda aliagiza Jeshi la Polisi kuzuia maandamano ya Ukuta, Ijumaa wakati akizungumza na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) katika kambi ya Ukonga.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi, alisema maandalizi ya kuunga mkono operesheni hiyo yamekamilika kwa nchi nzima.

“Kauli ya Mkuu wa Mkoa (wa Dar es Salaam) ya kusema kwamba polisi wahakikishe Ukuta haujengeki, haitekelezeki kwa sababu yeye hana mamlaka ya kufanya hivyo na wala si msajili wa vyama vya siasa hadi atoe kauli hiyo,” alisema Katambi.

“Zipo kesi nyingi zinazoonyesha wakuu wa mikoa kufanya kazi ambazo haziwahusu, hivyo kauli yake tutaipima kisheria,” alisema na kuongeza:

“Yeye akitaka aendelee kusema chochote akijisikia, lakini sisi tunamwambia kwamba mikutano yetu iko pale pale na tutaifanya nchi nzima.”

Katika mazungumzo yake na FFU, Makonda alisema askari wanafahamu sheria, hivyo wasisubiri mtu yeyote kuja kuwakumbusha juu ya jambo hilo.

Aidha, aliwataka polisi hao kutosubiri maelekezo mengine kwa kuwa Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais John Magufuli ameshaagiza kutofanyika kwa maandamano ya Ukuta yaliyopangwa kuwa Septemba mosi.

Makonda aliliagiza jeshi hilo kuhakikisha kwamba sheria zinafuatwa na kusiwapo kitu kinaitwa Ukuta ili wananchi waendelee na kazi zao kama kawaida.

Lakini Mwenyekiti wa Bavicha jana alisema: “Tunamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, ajiandae kutuma jeshi lake kulinda mikutano yetu.”

Kuhusu onyo la Rais Magufuli aliloitoa akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Singida kwamba Chadema isimjaribu kwa Ukuta, Katambi alisema chama hicho hakimjaribu.

Alisema Chadema itafanya maandamano nchi nzima kwa sababu kwa njia hiyo wanamsaidia kutoa mawazo yao kama vyama vya siasa kwa ajili ya kumsaidia kuendesha shughuli zake vizuri zaidi.

“Hatuna shida ya kumjaribu Rais, na wala si kwamba tunamchukia, na wala hatuna sababu ya kupinga uwapo wake, na hata ukiulizwa sasa kwamba Rais wako ni nani, lazima useme ni John Magufuli,” alisema Katambi.

“Tunapotoa dosari na kasoro tunamsaidia kuendesha nchi yake na watu walio chini yake.”

“Sisi kama vyama vya siasa tuna haki, tunajua yeye ndiye Rais, kama sisi hatukuweza kupata nafasi ya hiyo, haimaanishi kwamba ni vita, isipokuwa kupitia vyama vyetu, tuna sehemu ya kutoa mawazo yetu katika kuifanikishia serikali yake kuongoza vema pamoja na watu wake wa chini tena kwa mujibu wa sheria na inamsaidia yeye kuwa bora zaidi.
“Kwa hiyo kauli ya Rais sisi hatuna tatizo nayo.”

Katambi alisema taratibu zote za kisheria katika kutekeleza mikutano hiyo zitafuatwa.

Kamati Kuu ya chama hicho ilisema lengo la operesheni hiyo ni kuzuia matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia nchini.

Brazil yaonesha nia kuwekeza Tanzania kuzalisha umeme wa maji na mabaki ya miwa

Na Veronica Simba

Serikali ya Brazil imeonesha nia kuwekeza katika sekta ya nishati nchini hususan katika kuzalisha umeme kwa kutumia maji na mabaki ya miwa. Hayo yameelezwa jana jijini Dar es Salaam na Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Carlos Alfonso Puente, alipomtembelea Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ofisini kwake na kufanya mazungumzo naye.

Balozi Puente alimweleza Profesa Muhongo kuwa nchi yake inao ujuzi na uzoefu wa kutosha katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali hususan maji.

Alisema, Brazil ingependa kuchangia kufanikisha azma ya Rais John Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda.
“Kutekeleza mchakato wa kuifanya nchi kuwa ya Viwanda, unahitaji umeme mwingi unaotokana na vyanzo mbalimbali. Ni bahati nzuri kwamba Tanzania inazo njia za kufanikisha azma hiyo,” alisema.
Alisema kuwa, nchini Brazil, kuna Kampuni kubwa zenye uzoefu wa muda mrefu unaofikia miaka 20 hadi 40 katika kazi hiyo, ambazo huzalisha umeme wa maji nchini mwao na hata nje ya nchi.

Pia, alitaja eneo jingine ambalo nchi yake ina nia ya kuwekeza kuwa ni uzalishaji wa umeme unaotumia mabaki ya miwa ambayo aliielezea kuwa chanzo kizuri cha nishati safi.

Balozi Puente alisisitiza kuwa, Brazil ikiwa ni nchi inayozalisha miwa kwa kiwango kikubwa duniani, itasaidia kuleta mabadiliko katika sekta ya nishati kwa kuzalisha umeme unaotokana na mabaki ya miwa kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Kwa upande wake, Waziri Muhongo, akimjibu Balozi Puente, alikiri kuwa kuwa Brazil ina ujuzi, uzoefu na uwezo mkubwa hususan katika maeneo ambayo Balozi aliyataja na hivyo akamwambia nchi hiyo inakaribishwa kuwekeza Tanzania kwa kufuata masharti na utaratibu uliowekwa na Serikali.

Akizungumzia zaidi kuhusu utaratibu wa uwekezaji, Waziri Muhongo alieleza kwamba Serikali ya Tanzania, kupitia Wizara yake, inabadilisha utaratibu wa kupokea wawekezaji katika sekta husika.

Alisema, kunaandaliwa utaratibu maalum utakaokuwa wa wazi na kuruhusu ushindani kwa wenye nia ya kuwekeza kwa malengo ya kupunguza au kuondoa kabisa mazingira ya rushwa na muda mrefu unaotumika katika majadiliano pasipo sababu za msingi.

Profesa Muhongo alifafanua zaidi kwamba, Serikali itaweka mazingira mazuri zaidi ya ushindani kwa kuandaa maelezo ambayo pamoja na mambo mengine yatabainisha aina mbalimbali za vyanzo vya umeme vilivyopo nchini pamoja na maeneo vilipo.

Alisema, Kampuni zenye nia ya kuwekeza zitakaribishwa kupendekeza viwango vya bei vitakavyotumika kuuza umeme utakaozalishwa na zitashindanishwa, ambapo washindi wachache watachaguliwa kwa ajili ya majadiliano kabla ya kuingia mkataba wa uwekezaji husika.
“Kwa hivyo, tunaandaa kabrasha maalum litakalokuwa na maelezo husika na litakuwa tayari mwezi wa Septemba mwaka huu. Kabrasha hilo lenye maelezo litatumika kama mwongozo wa ushindanishaji maombi mbalimbali ya uwekezaji hususan katika kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali kwa uwazi,” alisisitiza.
Alivitaja vyanzo hivyo kuwa ni pamoja na gesi asilia, makaa ya mawe, maji, jua, upepo, jotoardhi, mawimbi ya bahari pamoja na nishati mbadala. Waziri Muhongo alisema kuwa maelezo hayo maalum yatasambazwa kwa wadau mbalimbali wa sekta husika wakiwemo wale wote wenye nia ya kuwekeza ikiwa ni pamoja nan chi ya Brazil kupitia Ubalozi wake hapa nchini.
“Kwa kutumia Kabrasha hilo maalum lenye maelezo husika, wewe Balozi utaweza kuwashawishi wafanyabiashara kutoka nchini kwako kutoa mapendekezo ya uwekezaji ambayo yana vigezo vyote muhimu vinavyoshawishi wapate fursa husika za uwekezaji katika sekta ya nishati,” Profesa Muhongo alimweleza Balozi Puente.
Kuhusu Mradi mkubwa wa ujenzi wa Bomba la kusafirisha mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania, ambao pia Brazil imeonesha nia kuwa ingependa kuwekeza kwa kushirikiana na Tanzania; Profesa Muhongo alisema Serikali itaweza kulisemea hilo baada ya kipindi cha miezi takribani 45 kupita, ambapo mambo yote ya kisheria kuhusu Mradi huo yanatarajiwa kuwa yamekamilika.

Aidha, Profesa Muhongo alitumia fursa hiyo kuomba nafasi za masomo nchini Brazil kwa wanafunzi wa kitanzania katika ngazi za Shahada za Uzamili na Uzamivu katika sekta ya Nishati hususan Mafuta na Gesi, kwa kuzingatia kuwa Brazil imeendelea sana katika sekta hiyo.
“Ninyi mnazo Taasisi bora kabisa za Utafiti duniani. Mnafanya vizuri sana katika maeneo mbalimbali.”
Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, Brazil ni miongoni mwa nchi Tano (5) bora duniani zinazozalisha umeme kwa kutumia nishati jadidifu kwa sababu umeme mwingi wanaozalisha unatokana na maji, kutoka katika Mito mikubwa waliyonayo.


Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Carlos Alfonso Puente (Kushoto), akisaini Kitabu cha Wageni ofisini kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kulia), alipomtembelea Waziri na kufanya naye mazungumzo kuhusu ushirikiano baina ya nchi hizo mbili hususan katika uwekezaji kwenye sekta ya nishati.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kushoto), akimsikiliza kwa makini Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Carlos Alfonso Puente (kulia), wakati Balozi huyo alipomtembelea Waziri Ofisini kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni na kufanya mazungumzo naye kuhusu masuala ya uwekezaji katika sekta za nishati na madini. Wengine pichani ni Maafisa wa Wizara waliohudhuria mkutano huo.

Mama Mwenye VVU Pamoja na mtoto wake wakutwa wamekufa mlimani MKAZI wa wilayani Chato


MKAZI wa wilayani Chato mkoani Geita, Rose Joseph (32) aliyekuwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi na mtoto wake mwenye umri wa miaka kati ya minne na mitano, wamekutwa mlimani wakiwa wamekufa katika mazingira ya kutatanisha katika kijiji cha Nafuba kilichoko ndani ya Ziwa Victoria wilayani Bunda mkoani Mara.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nafuba, Zakaria Kachimu alisema tukio hilo liligundulika juzi saa 9:00 mchana katika eneo la mlima huo, baada ya wananchi waliopita katika eneo hilo kuona kwanza mwili wa mwanamke huyo.

Alisema baadaye wananchi walifanikiwa kumtafuta mtoto wake na kumkuta pia akiwa amekufa katika eneo lingine. 

Kachimu alisema mwanamke huyo alifika kisiwani hapo Julai 25, mwaka huu, akiwa na mtoto mdogo wa kiume aitwaye Kababu, akiwa anatafuta kazi ya kuhudumia kwenye mgahawa.

Alisema kuwa kulingana na afya ya mwanamke huyo kudhoofika, kila sehemu alikokwenda kutafuta ajira hiyo alikataliwa. Baada ya kukosa ajira hiyo mwanamke huyo alikwenda kwa jamaa yake ambaye pia ni mwanamke aliyeko kisiwani hapo na kuishi nyumbani hapo.

Baadaye mwanamke huyo alikwenda kutibiwa katika zahanati moja iliyoko kisiwani hapo na ikagundulika kuwa ana mambukizi ya virusi vya Ukimwi na kuambiwa aende katika Kituo cha Afya Kisorya kwa ajili ya kujiunga kwa kupewa dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi (ARVs).

Hata hivyo ilielezwa kuwa mwanamke huyo hakwenda kwenye kituo hicho kama alivyoshauriwa na mganga wa zahanati hiyo.

Aidha, Ofisa Mtendaji huyo alisema siku ya tukio wananchi waliopita katika eneo hilo walikuta mwili wa mwanamke huyo katika mlima huo na kuamua kutoa taarifa, ambapo tena walianza kutafuta mtoto wake na kukuta pia akiwa amekufa katika eneo lingine.

Alisema kuwa chanzo cha vifo hivyo ni cha kutatanisha na kwamba huenda mtoto huyo alikufa kwa njaa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhani Ng’anzi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Alisema upelelezi unafanyika kujua chanzo cha vifo hivyo.

Mkuu wa Wilaya ya Nzega Awapiga Marufuku Madiwani na Wabunge Kufanya Mikutano ya hadhara nje ya maeneo yao waliyochaguliwa


SERIKALI wilaya ya Nzega mkoani Tabora imepiga marufuku wabunge na madiwani wa vyama vyote, kutofanya mikutano ya hadhara nje ya maeneo yao waliyochaguliwa.

Imechukua hatua hiyo ili kuepusha uchochezi wa kisiasa, ambao unaweza kujitokeza na kuhatarisha amani.

Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngupulla amesema viongozi hao wanapaswa kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao ya uchaguzi.

Amesema mbunge ama diwani, haruhusiwi kufanya mikutano nje ya eneo lake na endapo atabainika, atachukuliwa hatua kali za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kufikishwa katika vyombo vya dola.

Amesema serikali imetoa agizo hilo ili wananchi waweze kupata taarifa za maendeleo na sikuendelea kutoa lugha za kukashifu viongozi wa serikali.

Ngupulla aliongeza kuwa serikali haijakataza mikutano ya siasa, bali viongozi hao wanapaswa kufanya siasa safi katika maeneo yao na si kutoka nje ya maeneo yao, kwani wanaweza kuhatarisha amani ya nchi.

Polisi wazuia ghafla mkutano wa CHADEMA Chalinze........Mbowe Asema Wapo Tayari Kufa Kwa Kupigania Demokrasia


Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limefuta mkutano wa hadhara wa Chadema uliopangwa kufanyika katika Uwanja wa Miembe Saba mjini Chalinze.
Mkutano huo uliokuwa ufanyike jana, ulikuwa uhutubiwe na Waziri Mkuu mstaafu na mjumbe wa kamati ya Chadema, Frederick Sumaye. Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Pwani Baraka Mwago alisema jana kuwa alishangazwa na hatua hiyo ya ghafla ya polisi kwa kuwa mkutano huo ulifuata taratibu zote na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chalinze, aliruhusu kufanyika kuanzia saa 6.00 mchana hadi saa 12.00 jioni. Alisema wakati maandalizi yote yakiwa tayari, ilipotimia saa nane mchana waliitwa polisi na kuelezwa kuwa mkutano huo umezuia kwa maelezo kuwa intelijensia ya polisi imeonyesha kuwa ungehudhuriwa na viongozi wengi wa kitaifa, hivyo polisi Chalinze haijajipanga kutoa ulinzi kwa viongozi hao. “Hii sababu imetushangaza kwa sababu kiongozi wa kitaifa ambaye angehudhuria ni Sumaye peke yake." Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema kipengele cha 7.5.3 (f) inamtambua mjumbe wa kamati kuu au baraza kuu anayeishi katika mkoa kuwa ni mjumbe wa baraza la mkoa husika. “Kutokana na kipengele hicho, Sumaye ana sifa za kuhudhuria mkutano huu kwa sababu anaishi Kiluvya wilayani Kisarawe,” alisema Mwagu. Alisema lengo la mkutano huo, lilikuwa ni kuutambulisha uongozi mpya wa Chadema kwa wananchi baada ya kufanyika uchaguzi mdogo Juni 4, mwaka huu wilayani Mkuranga. Katibu wa Chadema mkoani humo, Halfani Milambo alisema waliandika barua kuwataarifu polisi na likakubali, lakini walishangazwa kuzuiwa baada ya kufika katika Uwanja wa Miembe Saba walikotakiwa kufanya mkutano. “Tuliwaandikia barua tarehe Agosti 4 na siku iliyofuata Agosti 5 tulikubaliwa na Mkuu wa Polisi Chalinze (OCD), SSP J. Magomi kufanya mkutano kwa masharti,” alisema.Alitaja masharti ambayo jeshi hilo liliwapa kuwa ni pamoja na kutokuwapo kwa maandamano ya bodaboda, ya miguu au magari, kutokukashifu chama au utawala wa kiongozi yeyote na kuzingatia muda wa kuanza na kumaliza mkutano. Alisema kuwa cha kushangaza jana baada ya kukamilisha maandalizi yote ikiwamo kufanya matangazo na kufunga vyombo vya muziki, baadhi ya viongozi waliitwa kwenye Ofisi ya Polisi Wilaya ya Chalinze na kuambiwa wasifanye mkutano huo. Alisema walielezwa kuwa ujumbe ambao unaenea kwenye mtandao unasema mkutano huo utaleta watu wengi sana, hivyo usalama utakuwa mdogo. Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Boniventura Mushongi alisema lengo la Polisi si kuwakataza kufanya mkutano, lakini kilichoonekana ni kuwa walikiuka maelekezo kwani awali walipaswa kufanya mkutano wa ndani na si wa nje. “Sisi hatuwakatazi kufanya mikutano yao, lakini ni vema wafuate makubaliano, maana sisi Jeshi la Polisi tuliwaruhusu wafanye mkutano wa ndani lakini tulishangazwa kuona wanaanza kufanya nje huku wakipiga muziki,” alisema. Mushongi alisema pia polisi inazuia mikutano yote ambayo haina madiwani wala wabunge katika eneo husika, jambo ambalo halikuwa kwenye maelekezo ya OCD. “Chadema katika eneo la Chalinze hawana diwani wala mbunge, hivyo wamekosa sifa za kufanya mkutano huu. Kama ni kikao cha ndani hatuna tatizo wafanye hata wakialika watu 200,” alisema Mushongi. Hata hivyo, Mushongi alisema Chadema Pwani walipopeleka barua ya maombi mkutano huo walipewa masharti hayo. Mbowe: Tuko tayari kwa lolote Wakati hayo yakiendelea, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema yeye na makamanda wake wako tayari kwa lolote kwa ajili ya kutetea misingi thabiti ya utawala bora unaoheshimu utawala wa sheria. Akizungumza  jana, Mbowe alisema hakuna mtu wa kuwafundisha makamanda wa Chadema, hivyo mikutano ya Ukuta itafanyika nchi nzima kuanzia Septemba Mosi. “Ambao hawako tayari warudi nyuma, hakuna aliyelazimishwa, watuache sisi tutangulie wa kufa wafe na wa kupona wapone. Haiwezekani mtu apuuze sheria, avunje katiba halafu taifa linyamaze,” alisema. “Sisi tumeamua kuchukua mzigo huo kwa niaba ya wananchi wote. Kama ataua wacha aue tu, kama atatufunga wacha atufunge tu lakini tutakuwa tumeacha legacy (kumbukumbu) duniani,”alisisitiza. Mbowe alisema sifa ya kiongozi bora anayeheshimu misingi ya kidemokrasia ni kuheshimu utawala bora unaoheshimu utawala wa sheria. Kwa mujibu wa Mbowe, Rais anakiuka Katiba na sheria za nchi zinazoruhusu vyama vya siasa kuendesha mikutano ya hadhara na hakuna mtu ndani ya CCM anayezungumzia hilo. Mbowe alisema Rais amejisahau kuwa yeye (Mbowe) ni mwenyekiti wa taifa kama alivyo Rais, hivyo anastahili kuzunguka nchi nzima kujenga uhai wa chama. “Rais anazunguka kwenye mikoa anavisema vyama vya upinzani na kutoa amri mbalimbali lakini sisi (upinzani) hatuna jukwaa la kujibu au kutoa ufafanuzi. Anasema tusubiri hadi 2020,” alilalamika Mbowe. “Rais anatoa amri, wakuu wake wa mikoa wanatoa amri, wakuu wa wilaya wanatoa amri, watu wanafukuzwa kazi ovyo. Nchi haiwezi kwenda kwa staili hii,” alisema. “Wewe unanyanyuka tu na kusema watu wahamie Dodoma kivipi? Issue ya kuhamia Dodoma ni suala la kitaifa siyo mamlaka ya mtu mmoja tu kwa kuwa ni Rais.”
 “Hata Nyerere 1973 alipopitisha hoja ya watu kuhamia Dodoma kilikuwa ni kikao cha NEC ya Tanu. Mpaka leo hakuna sheria ya kuhamia Dodoma na nchi hii inaoongozwa kwa sheria.” 
Mbowe alisema kwa kutambua kuwa hakuna sheria ya kuhamia Dodoma, ndiyo maana Ilani ya CCM (2015-2020) imeeleza kutengeneza sheria ya kuhamia makao makuu Dodoma. “Hakuna sheria. Rais hawezi kuamua matakwa yake binafsi yakawa ni sheria ya nchi. Alipaswa apeleke muswada wa sheria bungeni na ipitishwe na Bunge siyo kauli ya mtu mmoja,” alisisitiza Mbowe. Lissu: Tutafuata sheria Wakati huohuo, mwanasheria Mkuu wa Chadema na mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amesema katika utekelezaji wa Ukuta watafuata sheria kwa kupeleka barua za taarifa ya mikutano kwa wakuu wa polisi nchi nzima saa 48, kabla ya kuanza mikutano hiyo Septemba Mosi mwaka huu. Akizungumza juzi katika mahojiano na Redio ya Sauti ya Ujerumani (DW), Lissu alisema mikutano hiyo itafanywa kwa kufuata sheria na taratibu ikiwamo kutoa taarifa kwa wakuu wa polisi wa wilaya. Lissu ambaye aliachiwa na mahakama juzi kwa dhamana, alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa kwanini chama chake kisitafute njia mbadala ya operesheni Ukuta ambayo Serikali imesema itakabiliana nayo kwa njia yoyote ile. “Tumesema hatutafanya mkutano wowote usiokuwa na taarifa.Tutapeleka taarifa kwa wakuu wa polisi wilaya wote Tanzania nzima kama inavyotakiwa. Sasa hiyo hatuvunji sheria, tunatekeleza sheria,” alisema Lissu. Mbunge huyo, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uchochezi na kuidharau mahakama, alibainisha kuwa mikutano ya hadhara kuanzia Septemba Mosi, itafanyika kwa mujibu wa sheria za nchi kama Katiba ya nchi na sheria ya vyama vya siasa inavyoeleza. Alisema sheria inasema chama cha siasa ambacho kimeandikishwa kikitaka kufanya mkutano wowote wa hadhara wa siasa, kinatakiwa kupeleka barua ya taarifa kwa mkuu wa polisi wa wilaya saa 48 kabla ya mkutano huo. “Sheria inasema huyo ambaye tunampelekea taarifa atupe ulinzi kwenye mikutano yetu. Ndicho tunachotaka,” alisema Lissu. Alipoulizwa kama ni sawa iwapo polisi ikisema haiwezi kuwapa ulinzi na wasifanye mkutano katika eneo husika kwa wakati huo, Lissu alijibu,“(OCD) Ana uwezo wa kutuambia msifanye leo, msifanye kwenye eneo hili au msifanye saa hii, lakini hana uwezo wa kukataa katakata.” 
Mbunge huyo alisema kilichotokea nchini na kinachofanyika sasa si mikutano kudhibitiwa bali inakatazwa. “Hakuna sheria inayokataza au inayowapa mamlaka ya kukataza mikutano moja kwa moja kama hakuna tangazo la hali ya hatari,”alisema Lissu. Alisema kama Magufuli hataki mikutano atangazie dunia kwamba Tanzania ina hali ya hatari. “Akitangaza hali ya hatari tutamwelewa na wengine tutamuuliza kilichotokea ni kitu gani mpaka kuwe na hali ya hatari,” alisema Lissu

Sunday, July 10, 2016

Download | Snura - Shindu [Audio]















Barua pepe za Hillary Clinton kuchunguzwa upya

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema itaanzisha uchunguzi mpya kuangalia kama waziri wake wa zamani Hillary Clinton alifanya makosa kwa kutumia anuani binafsi ya barua pepe katika mawasiliano ya kikazi.
Hillary Clinton: Kivuli cha barua pepe kinamwandama. Hillary Clinton: Kivuli cha barua pepe kinamwandama.
Msemaji wa wizara hiyo John Kirby amesema watakuwa na uwazi mkubwa iwezekanavyo, lakini hawatajiwekea muda wa mwisho wa kukamilisha mchakato huo. Kirby amesema hatua hiyo ni baada ya kuhitimishwa kwa uchunguzi wa wizara ya sheria, ambao ulisema hakutakuwapo mashitaka yoyote dhidi ya Hillary Clinton.
Kirby vile vile amekanusha shutuma kwamba wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marakeni ina utamaduni wa uzembe kuhusu masuala ya mawasiliano.
''Madai ya kwamba wizara hii kama taasisi, ina utamaduni wa uzembe, hatukubaliano nayo, na kama alivyosema mkurugenzi wa FBI, hayo siyo kweli, wala hayakuwa sehemu ya uchunguzi na mapendekezo yaliyotokana na uchunguzi huo.'' Amesema Kirby.
Clinton ayaponyoka mashitaka
Mkurugenzi wa FBI James Comey amehojiwa na kamati ya uchunguzi ya bunge Mkurugenzi wa FBI James Comey amehojiwa na kamati ya uchunguzi ya bunge
Mwanzoni mwa wiki hii shirika la upelelezi la Marekani, FBI lilipendekeza Bi Clinton ambaye ananuia kugombea urais wa Marekani katika uchaguzi wa Novemba mwaka huu, asifunguliwe mashitaka yoyote, kutokana na kutumia kwake anuani binafsi ya barua pepe kwa masuala nyeti ya kikazi, wakati alipokuwa waziri wa mambo ya nchi za nje kati ya mwaka 2009 na 2013. Pendekezo hilo liliheshimiwa na wizara ya sheria.
Ingawa uamuzi huo ulimpa ahueni Bi Clinton, mkurugenzi wa FBI James Comey alisema bayana kwamba Clinton alifanya uzembe kupita kiasi katika mawasiliano hayo ya barua pepe.
Pendekezo la kutomfungulia mashitaka Hillary Clinton liliwachukiza warepublican, akiwemo Donald Trump ambaye anatarajiwa kuwa mpinzani wa Bi Clinton katika uchaguzi wa Novemba, wakisema kiongozi huyo amekwepa mkondo wa sheria kutokana na hadhi yake kama mwanasiasa wa ngazi ya juu.
FBI kibanoni
Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden na Hillary Clinton Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden na Hillary Clinton
Jana Mkurugenzi wa FBI alilazimika kulitetea pendekezo la kutomshitaki Bi Clinton, katika kamati ya bunge inayohusua uchunguzi.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje John Kirby hakutoa maelezo zaidi kuhusu uchunguzi huu mpya, mbali na kusema utakuwa na uwazi mkubwa,na utaheshimu majukumu yao kisheria.
Mkurugenzi wa FBI amesema miongoni mwa barua pepe 30,000 ambazo Hillary Clinton alizikadhi kwa shirika lake, 100 zilikuwa na taarifa nyeti. Nyingine 2000 zilipandishiwa hadhi ya unyeti, na kufanywa nyaraka za siri.
Wakati sakata hilo likiendelea kuvuma, Bi Hillary Clinton ameungana na makamu wa rais wa Marekani Joe Biden katika kampeni jimboni Pennsylvania, katika kuhamasisha umoja ndani ya chama cha Democratic, kabla ya mkutano wake mkuu utakaoanza tarehe 25 mwezi huu.