SERIKALI wilaya ya Nzega mkoani Tabora imepiga marufuku wabunge na madiwani wa vyama vyote, kutofanya mikutano ya hadhara nje ya maeneo yao waliyochaguliwa.
Imechukua hatua hiyo ili kuepusha uchochezi wa kisiasa, ambao unaweza kujitokeza na kuhatarisha amani.
Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngupulla amesema viongozi hao wanapaswa kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao ya uchaguzi.
Amesema mbunge ama diwani, haruhusiwi kufanya mikutano nje ya eneo lake na endapo atabainika, atachukuliwa hatua kali za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kufikishwa katika vyombo vya dola.
Amesema serikali imetoa agizo hilo ili wananchi waweze kupata taarifa za maendeleo na sikuendelea kutoa lugha za kukashifu viongozi wa serikali.
Ngupulla aliongeza kuwa serikali haijakataza mikutano ya siasa, bali viongozi hao wanapaswa kufanya siasa safi katika maeneo yao na si kutoka nje ya maeneo yao, kwani wanaweza kuhatarisha amani ya nchi.
No comments:
Post a Comment