Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank- Walter Steinmeier amepinga shinikizo la Austria kusitisha mazungumzo ya Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya na kuutaka umoja huo kufikiria kwa mapana uhusiano wake na nchi hiyo.
Frank-Walter Steinmeir amesema uhusiano wa karibu katika masuala ya kisiasa, uchumi na ya kibinaadamu inamaanisha pande zote mbili zinapaswa kutafuta njia kusonga mbele wakiwa kama majirani badala ya kulenga tu katika muda wa mchakato wa mazumgumzo hayo ambayo kwa kweli yamekwama.
Amekaririwa akisema "Suala tafauti lililo na umuhimu mkubwa ni kuhusu namna ya kusimamia uhusiano na Uturuki katika hali hii ngumu na nini wanachoapswa kufanya kwa wale waliokamatwa kufuatia jaribio la mapinduzi.
Viongozi wa Ulaya wana wasi wasi kuhusu kiwango cha hatua za ukandamizaji zinazochukuliwa na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki kwa watuhumiwa wanaohusika na jaribio hilo la mapinduzi lililoshindwa hapo mwezi uliopita.
Adhabu ya kifo sio maadili ya Ulaya
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier wa kwanza (kushoto) wa pili kushoto ni waziri wa mambo ya nje wa Liechtenstein Bibi. Aurelia Frick wa tatu ni Sebastian Kurz wa Austria na wa nne ni waziri wa Luxemburg Jean Asselborn.
Akizungumza na waadishi wa habari Ijumaa usiku (05.08.2016)baada ya kukutana na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zinazozungumza Kijerumani huko Liechtestein , Steinmeier amesema kuirudisha upya hukumu ya adhabu ya kifo nchini Uturuki kama alivyodokeza Erdogan kutakuwa ni kinyume na maadili ya Umoja wa Ulaya.
Uhusiano wa serikali ya Uturuki na Umoja wa Ulaya hususan na Austria hapo Ijumaa uliingia katika hali ya kuchafuliana majina ambapo waziri wa mambo ya nje wa Uturuki ameiita Austria kuwa ni mji mkuu wa siasa kali za ubaguzi baada ya Kansela Christian Kern wa nchi hiyo kupendekeza kukomeshwa kwa mazungumzo ya Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya kutokana na kutopigwa kwa hatua kubwa tokea yalipoanza hapo hapo mwaka 2005.
Steinmeier alizungumza mara baada ya waziri wa mambo ya nje wa Austria Sebastian Kurz kutamka kwamba haoni kati ya mambo yote mawili kuweza kufanikiwa lile la ahadi waliyopatiwa wananchi wa Uturuki kusafiri barani Ulaya bila ya kuhitaji visa na kuendelezwa kwa mchakato wa nchi hiyo kujiunga na Umoja wa Ulaya.
Uturuki yadai kutimiza ahadi
Hadi sasa Uturuki imesema imetimiza ahadi zake kwa mujibu wa makubaliano ya kihistoria na Umoja wa Ulaya kwa nchi hiyo kuwazuwia wahamiaji wanaokimbilia Ulaya kupitia fukwe zake ili nchi hiyo ipatiwe msaada wa kifedha na ahadi ya kusafiri katika nchi za Umoja wa Ulaya bila ya kuhitaji visa pamoja na kuendelezwa kwa mchakato wa nchi hiyo kujiunga na Umoja wa Ulaya.
Uturuki inalalamika kwamba Umoja wa Ulaya hautimizi ahadi yake kwa upande wake.
Steinmeir anataraji kuanzisha tena mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Uturuki na Ujerumani ambapo amesema "atahakikisha mazungumzo na Uturuki yatakuwa hayafanyiki tu kwa kupitia vipaza sauti na kamera na kwamba hakuna njia mbadala hata kama ni vigumu katika nyakati hizi za matatizo."
Ujerumani ni maskani ya takriban watu milioni tatu wenye asili ya Uturuki na ina wasi wasi mkubwa kufuatia kukamatwa kwa maelf ya watu baada ya jaribio la mapinduzi lililoshindwa nchini humo mwezi uliopita.
No comments:
Post a Comment