Thursday, January 19, 2017

Lema na Mkewe Wakana Mashitaka Dhidi Yao......Mawakili Wake Waomba Kesi Ipelekwe Mahakama ya Katiba

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) jana alikana tuhuma za makosa ya jinai kwa pamoja na mkewe, Neema, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Nestory Barro, Lema na Neema walikana mashtaka ya kutuma ujumbe mfupi wa simu ya mkononi wenye matusi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Awali akiwasomea maelezo ya kesi hiyo Wakili wa Serikali Alice Mtenga alidai kuwa Lema na Neema, Agosti 20 mwaka jana, ndani ya Jiji la Arusha, walimtumia ujumbe wa simu ya kiganjani kwa mkuu huyo wenye lugha ya matusi, huku wakijua ni kosa kisheria.

Ilidaiwa kuwa ujumbe huo ulitumwa kutoka simu namba 0764-150747 kwenda namba 0766-757575 uliokuwa ukidai, “Karibu, tutakudhibiti kama Uarabuni wanavyodhibiti mashoga.”

Baada ya kuwasomea maelezo hayo ya awali, washtakiwa hao kwa pamoja walikiri kuwa ni wakazi wa Arusha na Lema ni Mbunge wa Arusha Mjini ila walikataa kusambaza ujumbe huo wa kumtukana Gambo na tarehe ya kukamatwa kwao.

Hakimu Barro aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 3, ambapo upande wa Jamhuri utaanza kuwasilisha ushahidi wake Gambo akiwa wa kwanza.

Baada ya kesi hiyo kuahirishwa, wakili wa Lema, John Mallya aliiambia mahakama wanatoa notisi ya kuwasilisha pingamizi la mdomo kwa kuwa hati ya mashtaka ina mapungufu, na baadaye wataomba mahakama iitupilie mbali hati hiyo.

Hata hivyo, Hakimu huyo alisema hoja za awali za pingamizi hilo zitasikilizwa Februari 3 pia.

Mbali na Mkuu wa Mkoa, Jamhuri inakusudia kuita mashahidi wengine wanne, ilielezwa.

Kwa mujibu wa Wakili wa Serikali Mtenga upande wake pia utakuwa na vielelezo vitatu vitakavyotolewa
mahakamani hapo.

Alisema mashahidi watano watakaotoa ushahidi wao ni Gambo, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha (RCO), George Katabazi, (ASP) Damasi Massawe, mhusika kutoka kampuni ya simu ya Vodacom pamoja na mtaalamu wa picha.

Pia alivitaja vielelezo watakavyovitoa katika kesi hiyo kuwa ni nakala ya taarifa za mawasiliano ya simu kutoka kampuni ya Vodacom, simu ya mshtakiwa mke wa Lema na taarifa ya uchunguzi kutoka kitengo kinachoshughulikia masuala ya kiuchunguzi (Forensic Bureau).

Wakati huo huo, wakili wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, John Mallya amemuomba Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Bernard Nganga kutoanza kusikiliza kesi ya kuhamasisha maandamano Septemba Mosi (Ukuta) inayomkabili Lema peke yake.

Akitoa ombi hilo jana, Mallya alidai kuwa kesi hiyo ya kuhamasisha maandamano kwa njia ya mtandao wa kijamii kisha kuusambaza Agosti Mosi hadi Agosti 26 mwaka jana, haifai kusikilizwa katika mahakama hiyo sababu kuna hoja za Kikatiba.

Alisema shahidi aliyeandaliwa kwa ajili ya kutoa ushahidi wake ambaye ni RCO, George Katabazi hapaswi kutoa ushahidi mahakamani hapo, sababu kesi hiyo ina hoja za kikatiba.

“Mheshimiwa kesi hii ukiiangalia ipo kikatiba zaidi na kwasababu ipo kikatiba basi sisi tunaenda Mahakama Kuu ikasikilizwe na majaji watatu ili tupewe tafsiri ya vifungu vya sheria," alisema Mallya.

Alisema kwa Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977 inampa haki kiongozi au mwanasiasa kufanya shughuli za kisiasa.

"Kuwakataza au kuingilia kati tunataka kujua huko Mahakama Kuu ya Katiba, nani ana mamlaka ya kuzuia maandamano."

Naye wakili wa Serikali Mtenga alimuomba hakimu kutupa pingamizi la Mallya alilolitoa mahakamani hapo, badala yake kesi hiyo iendelee kusikilizwa kwani upande wa Jamhuri tayari ulishamuandaa
shahidi wake.

Hakimu Nganga alisema amesikia hoja za mawakili hao wa pande zote mbili na yeye anaendelea na kesi hiyo baada ya aliyekuwa
 
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Augutino Rwezile kupanda cheo na kuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kitengo cha biashara.

Alisema atatoa uamuzi wa kesi hiyo, kusikilizwa au kwenda kwa majaji watatu Februari 8.

Kajala Masanja akanusha binti yake kuharibikiwa kimaadili, ni baada ya video ya Ngono kusambaa mtandaoni

Katika mitandao mbalimbali ya kijamii ipo video iliyosambaa ambayo inamuhusu binti mdogo wa chini ya miaka 18 akifanya mapenzi na mtu mzima ndani ya Gari.

Awali ilisemekana kuwa katika video hiyo binti aliyeonekana ni Paula Paul ambaye ni mtoto wa staa wa filamu Kajala Masanja hali ambayo ilimfanya muigizaji huyo kukanusha uvumi huyo.

Muigizaji huyo kupitia instagram ameandika:
"Hey everyone….jamani mimi sina shida na mtu kama akinichukia au akinisema mimi kwa kitu chochote kile…kwasababu najua binadamu kuongea mmezoea..ila katika kuongea kwenu,kuingilia na kujudge my life naomba msimuingize mtoto wangu…
"Sijawahi kumuomba mtu anisaidie kulea hata siku moja…mimi nimeona kuna video insambaa mnasema ni mwanangu na mnajua kabisa sie paula huyo ila ilimradi tu mfurahishe roho zenu…nilinyamaza…ila sasa naona mnakoelekea ni pabaya..mnahisi yeye hana moyo? Au mnahisi haumii?.
"Mwanangu anasoma na sitaki mumchanganye na mambo yenu ya kipuuzi…vitu vibaya mnavyo muombea mwanangu viwarudie wenyewe…leave my daughter alone jamani…give us a break..fanyani tu mambo yenu yatakayofanya mpate faida katika maisha”,
 
 

Video | Bill Nass Feat. Mwana FA - Mazoea [Official Music Video]

Mpenzi wa Ray Kigosi, Chuchu Hans ajifungua mtoto wa kiume

Mpenzi wa msanii mkongwe wa filamu Ray Kigosi, Chuchu Hans amejifungua mtoto wa kiume wiki hii, Ray amethibitisha.
 
Muigizaji huyo ameonyesha furaha yake kwa kuwa huyo ni mtoto wake wa kwanza.

“Asante mungu kwa kuniletea pacha wangu asante my lovely mzungu kwa kunipa heshima kubwa kunifanya niitwe baba, mungu wangu wa haki asiyeshindwa na jambo akubariki sana,” muigizaji huyo aliandika Instagram.

Aliongeza, “Sasa msianze maneno yenu kwamba mwanangu amekunnywa maji, mtoto bado ni mchanga maana watu wa Insta kiboko lakini hawaishi mtoni,”

Kwa upande wa Chuchu Hans huyo ni mtoto wake wa pili, mtoto wake wa kwanza alizaa na mume wake wa zamani.
 

 

Tuesday, September 13, 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa awataka watanzania kudumisha amani


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini zote kutumia nyumba za ibada kuwahamasisha waumini wao umuhimu wa kulinda na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.

Amesema Serikali itahakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa nchini ili Watanzania wawe na uhakika wa kuendelea kufanya kazi zao za kuwaingizia kipato na kuwaletea tija.

Waziri Mkuu ametoa wito huo jana (Jumatatu, Septemba 12, 2016) wakati akizungumza na waumini wa dini ya kiislam mara baada ya kumaliza kuswali sala ya Eid El Haji kwenye viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke Dar es Salaam.

“Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote nchini. Wito wangu kwa viongozi wa dini msisitize waumini juu ya utunzaji wa amani pamoja na kukemea vitendo viovu ili Taifa lizidi kusonga mbele,” amesema.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi kuendelea kuwaombea mahujaji waliopo mjini Makka na Madina nchini Saudi Arabia wakiendelea na ibada ya hijja warudi salama.

Pia Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kuwasaidia kwa hali na mali watu waliokumbwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera ambako jumla ya watu 16 walifariki na wengine 253 kujeruhiwa.

Pia maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1264 zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma

Awali akisoma hutuba ya Eid viwanjani hapo Sheikh Nurdin Kishki alisema dini ya Uislamu ni dini ya amani hivyo amewaomba waislamu kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani yakiwemo mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Sheikh Kishki amesema ni muhimu watu kulinda amani kwani ikitoweka ni vigumu kuirudisha, alitolea mfano wanachi wa nchi za Libya na Misri ambazo hadi sasa zimeshindwa kuirudisha.

Amesema mtu yeyote anayejihusisha na vitendo vya uwamwagaji wa damu, kudhulumu mali za watu pamoja na kuwavunjia heshima wenzake atakuwa ameangamia, hivyo amewataka Watanzania hususan wakazi wa Temeke kujiepusha navyo.

“Temeke sasa inaongoza kwa matukio ya mauaji, wanaua hadi walinzi. Askari wameuawa bila hatia, jambo hili linasikitisha sana. Watu waliokuwa wanafanya kazi ya kulinda raia na mali zao wanauawa bila ya hatia! Ameongea kwa masikitiko na kuwaomba Watanzania wajiepuszhe na vitendo hivyo.

Katika hatua nyingine Sheikh Kishki ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuonyesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo hivyo amewaomba wananchi wawe mstari wa mbele kutoa ushirikiano ili taifa liweze kusomba mbele.

“Ndugu zangu tumepewa heshima kubwa leo kuswali Eid na Mheshimiwa Waziri Mkuu tena amekuja hapa kwenye viwanja hivi vya Mwembe Yanga, hii inaonyesha ukaribu wa viongozi wetu wakuu kwa wananchi wao hususan wa hali ya chini,” amesema.

Makamu Wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan Awasili Lusaka Kumwakilisha Rais Dkt. Magufuli Kwenye Sherehe Za Kula Kiapo Rais Wa Zambia Edgar Lungu


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akilakiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Michezo na Maendeleo ya Watoto Mhe. Agnes Musunga mara baada ya kutua  katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kenneth Kaunda jijini Lusaka, Zambia, leo Jumatatu Septemba 12, 2016  tayari kwa kumuwakilisha Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwenye sherehe za kuapishwa rais wa sita wa nchi hiyo Mhe. Edgar Lungu leo Jumanne Septemba 13, 2016 katika uwanja wa Mashujaa jijini Lusaka

Makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea shada la maua  mara baada ya kutua  katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kenneth Kaunda jijini Lusaka, Zambia, leo Jumatatu Septemba 12, 2016  tayari kwa kumuwakilisha Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwenye sherehe za kuapishwa rais wa sita wa nchi hiyo Mhe. Edgar Lungu leo  Jumanne Septemba 13, 2016 katika uwanja wa Mashujaa jijini Lusaka.

Taarifa rasmi ya serikali kuhusu tetemeko la ardhi mkoani Kagera


1 Tukio la tetemeko:

Tarehe 10/09/2016 saa 9 na dakika 27 mchana kumetokea tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
 
Kitovu cha tetemeko hilo ni kwenye makutano ya latitudo 10 06’ na longitudo 31055’ eneo ambalo ni kilomita 20 kaskazini mashariki mwa kijiji cha Nsunga na kilomita 42 kaskazini magharibi mwa mji wa Bukoba (Picha Namba 1 na 2). Kitovu hicho kilikuwa kilomita 10 chini ya ardhi kwenye eneo hilo.

Picha Namba 1: Kitovu cha tetemeko la ardhi Kagera (Mduara)
Picha Namba 2: Kitovu cha tetemeko la ardhi Kagera (Nyota nyekundu)
 
Nguvu za mtetemo wa ardhi wa tetemeko hilo ni 5.7 kwa kutumia skeli ya “Richter” ukubwa ambao ni wa juu sana kiasi cha kuleta madhara makubwa. Kutokana na ukubwa huu maeneo mengi ya mkoa wa Kagera ikijumuisha mji wa Bukoba yamepatwa na madhara makubwa sana ikijumuisha nyumba nyingi kupasuka (Picha Namba 3 na 4), watu wengi kujeruhiwa kwa kuangukiwa na vifusi na kuta za nyuma ambapo inakisiwa kuwa watu 13 wamepoteza maisha yao.

Picha namba 3: Nyumba iliyobomolewa na tetemeko la ardhi Bukoba.
Picha namba 4: Nyumba ziliyobomolewa na tetemeko la ardhi Bukoba.
 
2 Sababu za kutokea tetemeko hilo:
Kwa kuwa kitovu cha tetemeko hilo kiko chini sana ya ardhi (Km 10) na kwa kutafasiri umbile la mawimbi ya tetemeko hilo yaliyonakiliwa na vituo vya kupimia matetemeko ya ardhi (Picka Namba 5) inaonekana kuwa tetemeko hilo limetokana na misuguano ya mapange makubwa ya ardhi iliyopasuliwa na mipasuko ya ardhi mithili ya mipasuko kwenye bonde la ufa. Kwa kuwa eneo lililokumbwa na tetemeko la ardhi liko karibu na mkondo wa magharibi wa bonde la ufa la Afrika Mashariki inakisiwa kuwa mtetemo huu umesababishwa na kuteleza na kusiguana ka mapande ya miamba juu ya mipasuko ya ardhi ya bonde hilo la ufa.

Picha Namba 5: Umbile la mawimbi ya tetemeko la ardhi la tarehe 10 Septemba mkoani Kagera.
 
3 Upimaji wa matetemeko ya ardhi.
Mapaka sasa na duniani kote hakuna vifaa au taratibu za kuweza kutabiri utokeaji wa matetemeko ya ardhi. Vifaa vyote na taratibu zote za kuratibu/kupima matetemeko ya ardhi vinapima ukubwa na tabia ya tetemeko baada ya tetemeko kutokea.
 
4 Tafiti za kina.
Wakala wa Jiolojia Tanzania umepeleka wataalamu katika eneo la tukio ili kuendelea kufanya utafiti wa kina juu ya tetemeko hilo. Taarifa zaidi juu ya tukio hili zitaendelea kutolewa kulingana na matokeo ya tafiti hizo pamoja na tafasiri ya taarifa na takwimu za matetemeko ya ardhi zinazonakiliwa na vituo vya kupimia matetemeko ya ardhi nchini hususan kituo cha Geita ambacho ndicho kilicho karibu sana na eneo la tetemeko hili .
 
5 Mambo Muhimu ya Kuzingatia Kuepuka Madhara Yanayoweza Kusababishwa na Tetemeko la Ardhi
i. Kabla ya tukio:
(a) Elimu ya tahadhari inapaswa itolewe ili kila mmoja aelewe nini cha kufanya linapotokea tetemeko la ardhi ikiwa ni pamoja na kupata mafunzo kutoka kwa watu wa msalaba mwekundu kuhusu namna ya kuhudumia majeruhi ama wahanga na pia jeshi la zima moto ili kupata elimu kuhusu namna ya kutumia kizimamoto. Elimu na mafunzo hayo yatasaidia kuwaweka watu katika hali ya tahadhari na hii itasaidia kupunguza taharuki wakati wa tukio kwa vile watakuwa sasa wanajua namna ya kuchukua tahadhari.
(b) Kufanya mazoezi ya kuchukua tahadhari hizo mara kwa mara ili kujizoesha kwani mara nyingi wakati wa matukio ya majanga kama hayo watu huchelewa kuchukua uamuzi wa haraka kujinusuru kwani huwa bado wanajiuliza kwamba wafanye nini. Hivyo mazoezi ya mara kwa mara ya jinsi ya kuchukua tahadhari humfanya mtu kufanya uamuzi wa haraka pindi tukio linapotokea.
(c) Wananchi pia wanashauriwa kujenga nyumba bora na imara kwa kuzingatia viwango halisi vya ujenzi, kuweka misingi imara wakati wa ujenzi, kupata ushauri wa kitaalamu wa aina ya majengo yanayofaa kujengwa katika eneo husika kulingana na ardhi ya mahali hapo, kuepuka ujenzi wa nyumba katika miinuko mikali yenye kuambatana na mawe/ miamba (suspended boulders) na kuepuka ujenzi wa makazi katika maeneo tete yenye mipasuko ya miamba (faults) na uwezekano mkubwa wa kutokea matetemeko.

ii Wakati wa tukio:
(a) Wakati wa tukio la tetemeko la ardhi unashauriwa kukaa mahali salama kama vile sehemu ya wazi isiyo na majengo marefu, miti mirefu na miinuko mikali ya ardhi. Watu wanashauriwa kukaa nje ya nyumba katika sehemu za uwazi.
(b) Endapo tetemeko litakukuta ukiwa ndani ya nyumba unashauriwa ukae chini ya uvungu wa meza imara, ama kusimama kwenye makutano ya kuta na pia ukae mbali na madirisha na makabati ya vitabu, vyombo au fenicha ili kuepuka kuangukiwa na vitu hivyo.
(c) Unashauriwa usitembee umbali mrefu kwa lengo la kutafuta mahali salama kwa sababu tetemeko la ardhi hutokea ghafla na huchukua muda mfupi. Takwimu zinaonesha kwamba watu wanaotaharuki na kukimbia ovyo wakati wa tukio la tetemeko ndio hupata madhara ama kuumia.
(d) Salimisha macho yako kwa kuinamisha kichwa chako wakati wa tukio.
(e) Baki mahali salama hadi hapo mitetemo itakapo malizika na kisha ujikague kuona kama hujaumia na ndipo utoe msaada kwa wengine ambao watakuwa wameumia.
(f) Ondoka mahali ulipo kwa uangalifu kuepuka vitu ambavyo vitakuwa vimedondoka na kuvunjika kwani vinaweza kukudhuru.
(g) Jiandae kwa mitetemo itakayofuata baada ya mtetemo mkuu. Tetemeko kuu huwa mara nyingi linafuatiwa na mitetemo mingi midogo midogo.
(h) Kumbuka kuwa matukio ya matetemeko ya ardhi huweza kuambatana na moto hivyo jihadhari na matukio ya moto kwa vile tetemeko la ardhi linaweza kusababisha kupasuka kwa mabomba ya gesi au kukatika kwa nyaya za umeme ama kuharibika kwa vifaa vinavyotumia umeme na kusababisha hitilafu ya umeme.
(i) Kama uko nje ya jengo wakati tetemeko linatokea unashauriwa kubaki nje, simama mahali pa wazi na uwe mbali na majengo, miti mikubwa, nguzo na nyaya za umeme na ujikinge kichwani kadri inavyowezekana kwani paa za nyumba, miti, nguzo na nyaya za umeme vinaweza kudondoka na kuleta madhara.
(j) Endapo utakuwa unaendesha chombo cha moto wakati wa tukio la tetemeko la ardhi unashauriwa usimame kwa uangalifu sehemu salama na usubiri hadi mitetemo imalizike ndipo uendelee na safari yako kwani tetemeko linaweza kusababisha barabara au madaraja kukatika.
(k) Endapo utakuwa kwenye maeneo ya miinuko au milima uwe mwangalifu ili kuepuka kuporomokewa na mawe au kuangukiwa na miti,
(l) Baada ya mitetemo kumalizika endapo itakulazimu kuondoka mahali ulipo ukiwa katika jengo refu unashauriwa kutumia ngazi badala ya lifti au kipandishi.

iii Baada ya tukio:
(a) Wananchi wanashauriwa baada ya tukio kuzima umeme katika majengo ili kuepuka kutokea kwa hitilafu ya umeme kwani mitetemo huenda ikaendelea tena.
(b) Kukagua majengo kwa uangalifu ili kuhakikisha kama hayakupata madhara kama vile nyufa n.k,na kwamba yanaweza kuendelea kutumika na kama ikibidi basi unashauriwa kuwaita wataalamu wa majengo ili wayafanyie ukaguzi.
(c) Endapo utaangukiwa na vitu vizito usijaribu kutumia nguvu nyingi ili kujinasua kwani hujui vitu hivyo vina uzito kiasi gani, omba msaada kwa kuita kwa sauti lakini usifanye hivyo mara nyingi ili usipoteze nguvu nyingi mwilini maana hujui ni lini utaokolewa,
(d) Toa msaada unaowezekana kwa watu walioathirika na tetemeko na utoe taarifa kwa vyombo vinavyohusika na uokoaji.
 
Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST)
S.L.P. 903
Dodoma
Tanzania
Simu: 0262323020
Tovuti: www.gst.go.tz