Sunday, May 1, 2016

Auawa na Mdogo wake Baada ya Kumfumania Akifanya Mapenzi na Mkewe


Mkazi wa Mahembo Manyanda Manyilizu (40) ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani na mdogo wake baada ya kumfumania akiwa na mkewe.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Dismas Kisusi alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi katika Kijiji cha Mawemilu.

“Manyilizu alimkuta mdogo wake akifanya mapenzi na mkewe, alivyomuhoji, mdogo wake alichukua kitu akampiga nacho kichwani hivyo alifariki dunia wakati akiendelea na matibabu katika zahanati ya Kijiji cha Mawemilu,” alisema Kisusi.

Alidai mtuhumiwa na mwanamke walikimbia baada ya kufanya tukio hilo.

Katika tukio jingine, watu wawili wameuawa kwa kupigwa mawe na marungu kisha miili yao kuchomwa moto na wananchi.

Kisusi alisema tukio hilo lilitokea juzi katika Kijiji cha Shimba wilayani Kahama.

Kisusi alisema watu hao walituhumiwa kuwa ni majambazi baada ya kumvamia Mchongaraji Ndalawa (65), akiwa amelala nyumbani kwake wakimtaka awape fedha.

“Alivyosema hana walimkata kwa panga kichwani, ndipo wananchi walijichukulia sheria mkononi kwa kuwaua,” alisema.

Majeruhi huyo amelazwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama na hali yake inaendelea vizuri.

Serikali kutumia shilingi bilioni 59.5 kuwezesha vijiji nchi nzima


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dokta Philip Mpango, amesema kuwa serikali imepanga kutumia shilingi 59.5bn kwaajili ya kuviwezesha vijiji nchi nzima katika kipindi cha mwaka fedha 2016/2017

Dokta Mpango, aliwaambia wabunge mjini Dodoma, jana tarehe 30, Machi, 2016, kwamba fedha hizo ni kwajili ya kukiwezesha kila kijiji shilingi 50m kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali.

Alisema kuwa fedha hizo zimewekwa kwenye mfuko wa Hazina, ili kuwawezesha wadau na taasisi zitakazo husika  kupanga utaratibu mzuri wa matumizi ya fedha hizo.

“Fedha hizi zitaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu” aliongeza Waziri Mpango

Akizungumza kuhusu mikopo ya wanawake na vijana, Dokta Mpango, alisema kuwa serikali, kupitia Ofisi hiyo ya Waziri  Mkuu, imepanga kutumia shilingi 1bn kuendeleza ujuzi kwa vijana wasio na ajira na shilingi 1.955bn kuwainua wanawake kiuchumi

Alifafanua kuwa halmashauri za wilaya, miji na majiji zitaendelea na utaratibu wao wa kutenga asilimia 5 ya mapato yao ya ndani kutoa mikopo kwa vijana na asilimia nyingine 5 kwaajili ya kuwawezesha wanawake katika maeneo yao.

Serikali Yaendelea Kuhakiki Madeni ya Walimu


WAZIRI wa Fedha na Mipango Mhe. Dakta Philip Mpango, ameliambia Bunge mjini DODOMA, jana tarehe 30, Aprili, 2016, kwamba serikali inaendelea kuhakiki madeni ya walimu yaliyowasilishwa kwaajili ya malipo baada ya kubaini kuwepo kwa udanganyifu kwenye baadhi ya madai hayo

Alisema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2015/2016, serikali ilipokea madai yenye jumla ya shilingi Bilioni 29 na Milioni 800 na imelipa  20.125bn, huku madai mengine yakizuiwa baada ya kubainika hayakuwa halali.

Alitolea mfano wa mtumishi mmoja aliyewasilisha madai ya shilingi 600m badala ya shilingi laki 6, huku madai mengine yaliyolipwa miaka ya nyuma yakiwasilishwa kama madeni mapya

Dakta Mpango alisema kuwa serikali inathamini mchango wa walimu katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini na kwamba itaendelea kulipa madai yao na watumishi wengine wa umma baada ya kuyachambua, kuyahakiki na kujiridhisha kuwa ni halali.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumapili Ya Tarehe Moja Mwezi wa 5



Memphis Depay anaondoka Man United? maamuzi yake haya yanawashangaza wengi

Winga mshambuliaji wa klabu ya Man United ya Uingereza Memphis Depay jina lake limeingia kwenye headlines tena, baada ya kufanya kitendo ambacho huenda kikawa na maana ya kuashiria yeye kuondoka au kukosa furaha ndani ya Man United.
Memphis amewashangaza wengi hususani mashabiki wake wa Man Unitedwanaomfollow katika account yake ya Instagram, baada ya kuona winga huyo kaamua kufuta picha zote katika Instagram yake zinazohusu Man United ambazo aliwahi kupost na kubakisha moja akiwa na mpenzi wake pekee.
Screen-Shot-2016-05-01-at-8.09.31-AM-1024x636
Memphis katika account yake ya Instagram amefollow watu 11 pamoja na account yaMan United  pekee, kati ya hao hakuna mchezaji mwenzake wa Man Unitedaliyemfollow, kitu ambacho kimeandikwa na mitandao mingi ya Ulaya kuwa huenda winga huyo anataka kuondoka Man United.

Serikali Yaokoa Sh. Bilioni 15.4 za Mishahara HEWA Machi hadi Aprili 24


Serikali imetangaza kuokoa kiasi cha Sh15.4 bilioni katika kipindi cha kuanzia Machi hadi Aprili 24 ambacho kingelipwa kwa watumishi hewa 8,236 ambao wamebainika hadi sasa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Angela Kairuki aliliambia Bunge jana kuwa kazi ya kuwasaka watumishi hewa bado inaendelea nchini kote.

Alisema watumishi hao wamebainika katika maeneo mbalimbali na kati yao 1,614 ni wa Serikali Kuu na 6,624 wa Serikali za Mitaa.

Waziri alisema kuwapo kwa watumishi hewa kumewafukuzisha kazi maofisa 56 na taratibu za kuwafungulia kesi mahakamani zinaendelea ikiwamo kutakiwa kulipa hasara yote ambayo waliisababisha.

Alisema mapambano dhidi ya watumishi hewa ni endelevu ili kukomesha tabia hiyo inayolitia hasara taifa.

“Mheshimiwa Rais alitangaza siku za hivi karibu na mtaona nami natangaza leo idadi ikiwa juu kuliko aliyotangaza Rais na vyombo vingine vitaendelea kutangaza maana tuko kwenye kazi kila siku,”alisema Kairuki.

Alitaja changamoto kubwa katika wizara yake ni kuwa ni tofauti ya mishahara kwa wafanyakazi ambayo inaonekana ni kubwa kati ya mtu wa chini na wa juu yake, jambo alilosema Rais ameamua kulisimamia ili kulipunguza.

“Tofauti ya mishahara ni kubwa, kuna baadhi ya maeneo mtu anatakiwa kupokea mshahara wa miezi 50 au 30 ili aweze kumfikia mwenzake mwenye mshahara mmoja tu,” alisema Kairuki.

Kuhusu suala la ajira, alisema katika mwaka wa fedha wa 2016/17, Serikali imepanga kuajiri watumishi 71,496 kuanzia mwezi huu na akawataka waajiri kuacha kuwahamisha watumishi endapo hakuna fedha za kuwalipa.

Wafungwa Wanaosubiri Kunyongwa Magerezani Wafikia 465

IDADI ya Watanzania wanaosubiri kunyongwa imekuwa ikiongezeka na hadi sasa imefikia 465 kutokana na hukumu ya kifo kutotekelezwa tangu mwaka 1994. 

Ripoti iliyotolewa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika mafunzo kwa waandishi wa habari mjini Morogoro juzi, imebainisha kuwa hakuna hukumu yoyote ya kifo iliyosainiwa na Rais ili kutekelezwa hadi Oktoba 2015 kulipofanyika Uchaguzi Mkuu ambao Rais Magufuli aliibuka mshindi.

Ripoti hiyo ya Mpango wa Kujitathmini Kuhusu Hali ya Utekelezaji wa Haki za Binadamu (UPR), unaotekelezwa kwa mara ya pili nchini, imeonesha kuwa kuna mahabusu 465 wanaosubiri adhabu ya kifo, kati yao wanaume ni 445 na wanawake ni 20.

Wanaharakati 
Akiwasilisha ripoti hiyo, Ofisa Uchunguzi Mkuu wa Tume hiyo, Philemon Mponezya, alisema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, inaitaka Serikali kufuta adhabu hiyo kwa kuwa haitekelezeki lakini baadhi ya asasi hasa zinazohusika na haki za walemavu wa ngozi, zinapinga kufutwa kwa adhabu hiyo.

Baadhi ya asasi zinazopinga kufutwa kwa hukumu ya kifo ni taasisi ya Under The Same Sun (UTSS), ambayo inasema katika utafiti waliofanya, wahusika wanataka hukumu hiyo hasa inayohusu watu walioua albino, itekelezwe mpaka hapo mauaji hayo yatakapokoma.

Hata hivyo, Mponezya alisema watetezi wengi wa haki za binadamu wanataka adhabu hiyo ifutwe kwa kuwa ni kinyume cha haki za binadamu na kwa Tanzania, imekuwa mbaya zaidi kwa kuwa baadhi ya wahukumiwa wamesubiri zaidi miaka 20 bila hukumu dhidi yao kutekelezwa, jambo linalowaathiri kisaikolojia.

“Tume inasisitiza Serikali iangalie upya hukumu hii na kuiondoa kwa sababu ya utekelezaji wake. Tangu mwaka 1994 hadi leo watu 465 wanasubiri adhabu hiyo, hakuna aliyenyongwa. Kila mlango unapogongwa unahisi ni wewe kumbe la, tunadhani iondolewe maana haitekelezwi,” alisema Mponezya.

Wananchi wagawanyika 
Tume hiyo ilikiri kwamba, Tanzania imeshindwa kutekeleza adhabu hiyo kwa miaka mingi kutokana na Serikali kueleza kuwa jamii imegawanyika kuhusu hukumu hiyo. 

Wapo wanaotaka ifutwe lakini wengi wanataka iendelee kutekelezwa kutokana na ongezeko la mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina na albino.

Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mark Mulumbo, alipotakiwa kufafanua kuhusu mtazamo wa kisheria na kiserikali kuhusu utekelezaji wa adhabu hiyo katika mafunzo hayo, alikiri kwamba tafiti zilizofanywa nchini zimeonesha kuwa, kuna mgawanyiko kwa wananchi kuhusu adhabu hiyo.

“Tume kadhaa zilizoundwa kupata maoni ya wananchi, zilitoa matokeo kuwa wananchi wengi bado hawataki adhabu iondolewe, wanataka iendelee kuwapo, sasa Serikali inafanya kazi kwa matakwa ya wananchi, si vinginevyo,” alisema Mulumbo.

Akifafanua zaidi, alisema hata katika mchakato wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hali hiyo ilijitokeza kwamba Watanzania wengi hawaoni kama muda ni mwafaka kufuta adhabu hiyo. 

Marais 
Kuhusu marais kushindwa kusaini hukumu hiyo, Mulumbo alisema upo mtazamo wa aina mbili kuhusu jambo hilo; wa kiimani na kisheria.

Alisema pamoja na kwamba nchi haina dini, marais wote waliowahi kuchaguliwa mpaka wa Awamu ya Tano, wana imani za kidini. 

“Siwasemei kwamba imani zao ni sababu, lakini huenda ni sababu.Ila kisheria rais hahukumiwi akisaini hukumu hiyo, sasa hilo mimi siwezi kulisemea ila sheria zinaweza kuangaliwa zaidi, ili zimpe rais nafasi ya kumpa mhusika kifungo cha maisha. 

“Lakini hapo napo kuna mtazamo mwingine, maana kuna hoja kwamba kwa nini aliyeua na kupatikana na hatia afungwe maisha. Je, iko wapi haki ya aliyeuawa?” Alifafanua Mulumbo kwa mtazamo wake.

Wanaoipenda 
Mwanasheria wa UTSS aliyewasilisha mada katika mafunzo hayo, Perpetua Senkoro, ambaye pia ana ulemavu wa ngozi, alisema  kwamba, utafiti uliofanywa na taasisi hiyo kwa walemavu wa ngozi (albino) kuhusu hukumu hiyo, umeonesha jamii inataka iendelee kuwapo, na itekelezwe.

Senkoro alisema wana imani sawa na wanaharakati wenzao wa haki za binadamu kuwa dhana ya hukumu ni kumfanya mkosaji abadilike na hukumu ya kifo haitoi nafasi ya kubadilika, lakini kwao kutokana na namna wanavyouliwa kwa imani za kishirikina, hilo si suala la tabia bali ni imani na hivyo muuaji hawezi kubadilika, wanaona heri iendelee kuwapo na itekelezwe.

“Wengi wa jamii yetu wanataka hukumu iendelee kuwapo mpaka hapo mauaji kwa albino yatakapokoma na itekelezwe. Wauaji wa albino wanaua kwa imani si tabia, wanatumwa na watu wenye fedha, kiungo kinauzwa Dola za Marekani 2,000, tena tunaona wanaokamatwa ni vidagaa, bado mapapa hatuyaoni, tunaomba Serikali (ya Magufuli) iwatafute vigogo na tuone hukumu hii ikitekelezwa ili kumaliza imani hizi zinazowanyima haki baadhi yetu ya kuishi,” alisema Senkoro.

Pamoja na Tanzania kuridhia mapendekezo kadha wa kadha ya haki za binadamu, bado Mei 9 hadi 12 mwaka huu, katika mkutano wa Geneva, Uswisi itaulizwa utekelezaji wa mapendekezo mengine na msimamo wa nchi kuhusu kufuta adhabu ya kifo.

Mkutano huo utahudhuriwa na asasi mbalimbali za utetezi wa haki za binadamu nchini, viongozi wa serikali pamoja na tume za haki za binadamu, ambapo nchi zaidi ya 190 zinatarajiwa kushiriki.

Ripoti mpya ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, imeonesha kuwa idadi ya watu waliouawa mwaka 2015 katika utekelezaji wa hukumu ya kifo ni kubwa zaidi tangu mwaka 1990.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu 1,634 waliuawa mwaka jana sawa na asimilia 50 ya waliouawa mwaka 2014. Aidha takwimu hizo hazihusu utekelezaji wa hukumu hiyo nchini China, ambako takwimu za adhabu hiyo huwa siri ingawa zinatajwa kuwa kubwa. 

Nchi zinazotajwa kutekeleza zaidi hukumu hiyo mwaka jana ni Iran, Pakistan na Saudi Arabia ambako asilimia 90 adhabu hiyo ilitekelezwa.