Jeshi la Syria limesema Jumamosi(09.07.2016) limerefusha usitishaji
mapigano nchi nzima licha ya kutokea mapambano makali kuwania kudhibiti
barabara pekee kuingialia maeneo yanayodhibitiwa na waasi katika mji wa
Aleppo
Mashambulizi hayo ya makombora yamewauwa zaidi ya raia 50 katika mji huo wa kaskazini.Shirika la habari la Syria SANA limesema uongozi wa jeshi umerefusha , "muda wa siku tatu wa utulivu" ambao ulimalizika usiku wa manane siku ya Ijumaa. Usitishaji huo sasa utaendelea kwa masaa mengine 72 hadi usiku wa manane siku ya Jumanne.
Tamko la kusitisha mapigano lililotangazwa siku ya Jumatano limeingiliana na kuanza kwa sikukuu ya Idd ul-Fitr, ambayo inaadhimisha mwisho wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kiasi ya raia 155, ikiwa ni pamoja na watoto 48, waliuwawa katika mapigano yaliyotokea katika sehemu mbali mbali za Syria wakati wa sikukuu hiyo iliyodumu kwa siku tatu, limeripoti shirika la linaloangalia haki za binadamu nchini Syria.
Tangazo la kurefusha usitishaji mapigano
Kurefushwa kwa usitishaji mapigano kulitangazwa wakati majeshi ya serikali na waasi yakiendelea kupigana kuwania udhibiti wa njia pekee kuingia katika eneo la mashariki ya mji wa Aleppo linalodhibitiwa na waasi, huku kukiwa na mashambulizi ya makombora kutoka kila upande katika sekta zote za mji huo uliogawika.
Shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria limeripoti mashambulizi mawili ya mabomu ya kujitoa muhanga katika magari yaliyofanywa na tawi la al-Qaeda , la al-Nusra Front, katika jaribio la kuyarejesha nyuma majeshi ya serikali ambayo siku ya Alhamis yamedhibiti na kuzuwia barabara muhimu ya Castello, njia pekee ya kujipatia mahitaji kwa eneo linaloshambuliwa sana la mashariki.
Shirika la habari la Syria SANA, likinukuu duru za kijeshi ambazo hazikutajwa , limesema kwa majeshi ya serikali siku ya Jumamosi yalipanua udhibiti wao kuzunguka barabara muhimu ya Castillo.
Hasara kubwa kwa waasi
Hatua hiyo inayodaiwa ya kusongambele imekuja baada ya majeshi ya serikali kutoa kipigo kikali na kusababisha "hasara kubwa" katika kile shirika hilo ilichosema kuwa ni "magaidi" likimaanisha waasi wanaopigana kuuondoa utawala wa rais Bashar al-Assad.
Kiasi ya raia 38 waliuwawa usiku wa Ijumaa katika mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na waasi katika eneo la Aleppo magharibi linalodhibitiwa na serikali, kwa mujibu wa shirika hilo linaloangalia haki za binadamu, ambalo linakusanya ripoti zake kutokana na mtandao wake wa wanaharakati ndani ya Syria.
Wakati huo huo , kiasi ya raia 17 wameuwawa , ikiwa ni pamoja na watoto sita , waliouwawa katika mashambulizi ya makombora na ya anga yaliyofanywa na jeshi la serikali katika sekta ya mashariki ya mji wa Aleppo.
Marubani wawili wa Urusi waliuwawa na wapiganaji wa Dola la Kiislamu baada ya kuidungua helikopta yao
Na marubani wawili raia wa Urusi wamefariki karibu na mji wa Syria wa
Palmyra wakati helikopta yao ilipodunguliwa na wapiganaji wa Dola la
Kiislamu, na kufikisha idadi ya wanajeshi wa Urusi waliouwawa nchini
Syria kufikia 12, imesema serikali ya Urusi.Wizara ya ulinzi imesema helikopta ya Syria ikirushwa na marubani Riafagat Khabibulin na Yevgeni Dolgin " ilishambuliwa " na wapiganaji wa IS jana Jumamosi na kuanguka na kuwauwa marubani wote wawili.
No comments:
Post a Comment