Tuesday, September 13, 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa awataka watanzania kudumisha amani



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini zote kutumia nyumba za ibada kuwahamasisha waumini wao umuhimu wa kulinda na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.

Amesema Serikali itahakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa nchini ili Watanzania wawe na uhakika wa kuendelea kufanya kazi zao za kuwaingizia kipato na kuwaletea tija.

Waziri Mkuu ametoa wito huo jana (Jumatatu, Septemba 12, 2016) wakati akizungumza na waumini wa dini ya kiislam mara baada ya kumaliza kuswali sala ya Eid El Haji kwenye viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke Dar es Salaam.

“Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote nchini. Wito wangu kwa viongozi wa dini msisitize waumini juu ya utunzaji wa amani pamoja na kukemea vitendo viovu ili Taifa lizidi kusonga mbele,” amesema.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi kuendelea kuwaombea mahujaji waliopo mjini Makka na Madina nchini Saudi Arabia wakiendelea na ibada ya hijja warudi salama.

Pia Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kuwasaidia kwa hali na mali watu waliokumbwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera ambako jumla ya watu 16 walifariki na wengine 253 kujeruhiwa.

Pia maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1264 zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma

Awali akisoma hutuba ya Eid viwanjani hapo Sheikh Nurdin Kishki alisema dini ya Uislamu ni dini ya amani hivyo amewaomba waislamu kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani yakiwemo mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Sheikh Kishki amesema ni muhimu watu kulinda amani kwani ikitoweka ni vigumu kuirudisha, alitolea mfano wanachi wa nchi za Libya na Misri ambazo hadi sasa zimeshindwa kuirudisha.

Amesema mtu yeyote anayejihusisha na vitendo vya uwamwagaji wa damu, kudhulumu mali za watu pamoja na kuwavunjia heshima wenzake atakuwa ameangamia, hivyo amewataka Watanzania hususan wakazi wa Temeke kujiepusha navyo.

“Temeke sasa inaongoza kwa matukio ya mauaji, wanaua hadi walinzi. Askari wameuawa bila hatia, jambo hili linasikitisha sana. Watu waliokuwa wanafanya kazi ya kulinda raia na mali zao wanauawa bila ya hatia! Ameongea kwa masikitiko na kuwaomba Watanzania wajiepuszhe na vitendo hivyo.

Katika hatua nyingine Sheikh Kishki ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuonyesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo hivyo amewaomba wananchi wawe mstari wa mbele kutoa ushirikiano ili taifa liweze kusomba mbele.

“Ndugu zangu tumepewa heshima kubwa leo kuswali Eid na Mheshimiwa Waziri Mkuu tena amekuja hapa kwenye viwanja hivi vya Mwembe Yanga, hii inaonyesha ukaribu wa viongozi wetu wakuu kwa wananchi wao hususan wa hali ya chini,” amesema.
Unknown Web Developer

Morbi aliquam fringilla nisl. Pellentesque eleifend condimentum tellus, vel vulputate tortor malesuada sit amet. Aliquam vel vestibulum metus. Aenean ut mi aucto.

Makamu Wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan Awasili Lusaka Kumwakilisha Rais Dkt. Magufuli Kwenye Sherehe Za Kula Kiapo Rais Wa Zambia Edgar Lungu



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akilakiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Michezo na Maendeleo ya Watoto Mhe. Agnes Musunga mara baada ya kutua  katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kenneth Kaunda jijini Lusaka, Zambia, leo Jumatatu Septemba 12, 2016  tayari kwa kumuwakilisha Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwenye sherehe za kuapishwa rais wa sita wa nchi hiyo Mhe. Edgar Lungu leo Jumanne Septemba 13, 2016 katika uwanja wa Mashujaa jijini Lusaka

Makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea shada la maua  mara baada ya kutua  katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kenneth Kaunda jijini Lusaka, Zambia, leo Jumatatu Septemba 12, 2016  tayari kwa kumuwakilisha Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwenye sherehe za kuapishwa rais wa sita wa nchi hiyo Mhe. Edgar Lungu leo  Jumanne Septemba 13, 2016 katika uwanja wa Mashujaa jijini Lusaka.

Unknown Web Developer

Morbi aliquam fringilla nisl. Pellentesque eleifend condimentum tellus, vel vulputate tortor malesuada sit amet. Aliquam vel vestibulum metus. Aenean ut mi aucto.

Taarifa rasmi ya serikali kuhusu tetemeko la ardhi mkoani Kagera



1 Tukio la tetemeko:

Tarehe 10/09/2016 saa 9 na dakika 27 mchana kumetokea tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
 
Kitovu cha tetemeko hilo ni kwenye makutano ya latitudo 10 06’ na longitudo 31055’ eneo ambalo ni kilomita 20 kaskazini mashariki mwa kijiji cha Nsunga na kilomita 42 kaskazini magharibi mwa mji wa Bukoba (Picha Namba 1 na 2). Kitovu hicho kilikuwa kilomita 10 chini ya ardhi kwenye eneo hilo.

Picha Namba 1: Kitovu cha tetemeko la ardhi Kagera (Mduara)
Picha Namba 2: Kitovu cha tetemeko la ardhi Kagera (Nyota nyekundu)
 
Nguvu za mtetemo wa ardhi wa tetemeko hilo ni 5.7 kwa kutumia skeli ya “Richter” ukubwa ambao ni wa juu sana kiasi cha kuleta madhara makubwa. Kutokana na ukubwa huu maeneo mengi ya mkoa wa Kagera ikijumuisha mji wa Bukoba yamepatwa na madhara makubwa sana ikijumuisha nyumba nyingi kupasuka (Picha Namba 3 na 4), watu wengi kujeruhiwa kwa kuangukiwa na vifusi na kuta za nyuma ambapo inakisiwa kuwa watu 13 wamepoteza maisha yao.

Picha namba 3: Nyumba iliyobomolewa na tetemeko la ardhi Bukoba.
Picha namba 4: Nyumba ziliyobomolewa na tetemeko la ardhi Bukoba.
 
2 Sababu za kutokea tetemeko hilo:
Kwa kuwa kitovu cha tetemeko hilo kiko chini sana ya ardhi (Km 10) na kwa kutafasiri umbile la mawimbi ya tetemeko hilo yaliyonakiliwa na vituo vya kupimia matetemeko ya ardhi (Picka Namba 5) inaonekana kuwa tetemeko hilo limetokana na misuguano ya mapange makubwa ya ardhi iliyopasuliwa na mipasuko ya ardhi mithili ya mipasuko kwenye bonde la ufa. Kwa kuwa eneo lililokumbwa na tetemeko la ardhi liko karibu na mkondo wa magharibi wa bonde la ufa la Afrika Mashariki inakisiwa kuwa mtetemo huu umesababishwa na kuteleza na kusiguana ka mapande ya miamba juu ya mipasuko ya ardhi ya bonde hilo la ufa.

Picha Namba 5: Umbile la mawimbi ya tetemeko la ardhi la tarehe 10 Septemba mkoani Kagera.
 
3 Upimaji wa matetemeko ya ardhi.
Mapaka sasa na duniani kote hakuna vifaa au taratibu za kuweza kutabiri utokeaji wa matetemeko ya ardhi. Vifaa vyote na taratibu zote za kuratibu/kupima matetemeko ya ardhi vinapima ukubwa na tabia ya tetemeko baada ya tetemeko kutokea.
 
4 Tafiti za kina.
Wakala wa Jiolojia Tanzania umepeleka wataalamu katika eneo la tukio ili kuendelea kufanya utafiti wa kina juu ya tetemeko hilo. Taarifa zaidi juu ya tukio hili zitaendelea kutolewa kulingana na matokeo ya tafiti hizo pamoja na tafasiri ya taarifa na takwimu za matetemeko ya ardhi zinazonakiliwa na vituo vya kupimia matetemeko ya ardhi nchini hususan kituo cha Geita ambacho ndicho kilicho karibu sana na eneo la tetemeko hili .
 
5 Mambo Muhimu ya Kuzingatia Kuepuka Madhara Yanayoweza Kusababishwa na Tetemeko la Ardhi
i. Kabla ya tukio:
(a) Elimu ya tahadhari inapaswa itolewe ili kila mmoja aelewe nini cha kufanya linapotokea tetemeko la ardhi ikiwa ni pamoja na kupata mafunzo kutoka kwa watu wa msalaba mwekundu kuhusu namna ya kuhudumia majeruhi ama wahanga na pia jeshi la zima moto ili kupata elimu kuhusu namna ya kutumia kizimamoto. Elimu na mafunzo hayo yatasaidia kuwaweka watu katika hali ya tahadhari na hii itasaidia kupunguza taharuki wakati wa tukio kwa vile watakuwa sasa wanajua namna ya kuchukua tahadhari.
(b) Kufanya mazoezi ya kuchukua tahadhari hizo mara kwa mara ili kujizoesha kwani mara nyingi wakati wa matukio ya majanga kama hayo watu huchelewa kuchukua uamuzi wa haraka kujinusuru kwani huwa bado wanajiuliza kwamba wafanye nini. Hivyo mazoezi ya mara kwa mara ya jinsi ya kuchukua tahadhari humfanya mtu kufanya uamuzi wa haraka pindi tukio linapotokea.
(c) Wananchi pia wanashauriwa kujenga nyumba bora na imara kwa kuzingatia viwango halisi vya ujenzi, kuweka misingi imara wakati wa ujenzi, kupata ushauri wa kitaalamu wa aina ya majengo yanayofaa kujengwa katika eneo husika kulingana na ardhi ya mahali hapo, kuepuka ujenzi wa nyumba katika miinuko mikali yenye kuambatana na mawe/ miamba (suspended boulders) na kuepuka ujenzi wa makazi katika maeneo tete yenye mipasuko ya miamba (faults) na uwezekano mkubwa wa kutokea matetemeko.

ii Wakati wa tukio:
(a) Wakati wa tukio la tetemeko la ardhi unashauriwa kukaa mahali salama kama vile sehemu ya wazi isiyo na majengo marefu, miti mirefu na miinuko mikali ya ardhi. Watu wanashauriwa kukaa nje ya nyumba katika sehemu za uwazi.
(b) Endapo tetemeko litakukuta ukiwa ndani ya nyumba unashauriwa ukae chini ya uvungu wa meza imara, ama kusimama kwenye makutano ya kuta na pia ukae mbali na madirisha na makabati ya vitabu, vyombo au fenicha ili kuepuka kuangukiwa na vitu hivyo.
(c) Unashauriwa usitembee umbali mrefu kwa lengo la kutafuta mahali salama kwa sababu tetemeko la ardhi hutokea ghafla na huchukua muda mfupi. Takwimu zinaonesha kwamba watu wanaotaharuki na kukimbia ovyo wakati wa tukio la tetemeko ndio hupata madhara ama kuumia.
(d) Salimisha macho yako kwa kuinamisha kichwa chako wakati wa tukio.
(e) Baki mahali salama hadi hapo mitetemo itakapo malizika na kisha ujikague kuona kama hujaumia na ndipo utoe msaada kwa wengine ambao watakuwa wameumia.
(f) Ondoka mahali ulipo kwa uangalifu kuepuka vitu ambavyo vitakuwa vimedondoka na kuvunjika kwani vinaweza kukudhuru.
(g) Jiandae kwa mitetemo itakayofuata baada ya mtetemo mkuu. Tetemeko kuu huwa mara nyingi linafuatiwa na mitetemo mingi midogo midogo.
(h) Kumbuka kuwa matukio ya matetemeko ya ardhi huweza kuambatana na moto hivyo jihadhari na matukio ya moto kwa vile tetemeko la ardhi linaweza kusababisha kupasuka kwa mabomba ya gesi au kukatika kwa nyaya za umeme ama kuharibika kwa vifaa vinavyotumia umeme na kusababisha hitilafu ya umeme.
(i) Kama uko nje ya jengo wakati tetemeko linatokea unashauriwa kubaki nje, simama mahali pa wazi na uwe mbali na majengo, miti mikubwa, nguzo na nyaya za umeme na ujikinge kichwani kadri inavyowezekana kwani paa za nyumba, miti, nguzo na nyaya za umeme vinaweza kudondoka na kuleta madhara.
(j) Endapo utakuwa unaendesha chombo cha moto wakati wa tukio la tetemeko la ardhi unashauriwa usimame kwa uangalifu sehemu salama na usubiri hadi mitetemo imalizike ndipo uendelee na safari yako kwani tetemeko linaweza kusababisha barabara au madaraja kukatika.
(k) Endapo utakuwa kwenye maeneo ya miinuko au milima uwe mwangalifu ili kuepuka kuporomokewa na mawe au kuangukiwa na miti,
(l) Baada ya mitetemo kumalizika endapo itakulazimu kuondoka mahali ulipo ukiwa katika jengo refu unashauriwa kutumia ngazi badala ya lifti au kipandishi.

iii Baada ya tukio:
(a) Wananchi wanashauriwa baada ya tukio kuzima umeme katika majengo ili kuepuka kutokea kwa hitilafu ya umeme kwani mitetemo huenda ikaendelea tena.
(b) Kukagua majengo kwa uangalifu ili kuhakikisha kama hayakupata madhara kama vile nyufa n.k,na kwamba yanaweza kuendelea kutumika na kama ikibidi basi unashauriwa kuwaita wataalamu wa majengo ili wayafanyie ukaguzi.
(c) Endapo utaangukiwa na vitu vizito usijaribu kutumia nguvu nyingi ili kujinasua kwani hujui vitu hivyo vina uzito kiasi gani, omba msaada kwa kuita kwa sauti lakini usifanye hivyo mara nyingi ili usipoteze nguvu nyingi mwilini maana hujui ni lini utaokolewa,
(d) Toa msaada unaowezekana kwa watu walioathirika na tetemeko na utoe taarifa kwa vyombo vinavyohusika na uokoaji.
 
Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST)
S.L.P. 903
Dodoma
Tanzania
Simu: 0262323020
Tovuti: www.gst.go.tz
Unknown Web Developer

Morbi aliquam fringilla nisl. Pellentesque eleifend condimentum tellus, vel vulputate tortor malesuada sit amet. Aliquam vel vestibulum metus. Aenean ut mi aucto.

Rais Kenyatta, Mbowe watoa msaada kwa waathirika wa Tetemeko la Ardhi Kagera



Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta amezungumza kwa njia ya simu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kumpa pole kufuatia vifo vya watu na madhara mengine yaliyotokana na tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Tetemeko lililotokea mkoani Kagera Septemba 10, limesababisha vifo vya watu 16, kuacha watu 253 wakiwa na majeraha mbalimbali ya mwili na nyumba zaidi ya 1000 zikiwa zimebomolewa.

Taarifa kutoka kwa msemaji wa Rais Kenyatta alisema kuwa Rais Kenyatta ameahidi kutoa msaada wa mabati, blanketi na magodoro ili kuwasaidia watu wasio na makazi mkoani Kagera.

Msaada huo utasafirishwa kwa ndege na Jeshi la Kenya Jumanne  hii Septemba 13  hadi mkoani Kagera ambapo ndipo palipopata madhara.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, jana aliwasili mjini Bukoba kuwatembelea waathirika na kutoa mkono wa pole kwa kaya 16 za waliofikwa na misiba kutokana na tetemeko hilo la ardhi.

Mbowe alitoa shilingi milioni 2.1 kwa ajili ya kaya hizo, mifuko 150 ya sementi kwa familia 15 ambazo zimepoteza makazi ambapo kila kaya ilipata mifuko 10.

Mwenyekiti huyo wa Chadema aliambatana na viongozi wengine wa  Chadema mjini humo pamoja na Mbunge wa Bukoba Mjini, Willfredy Rwakatale na Mbunge wa viti maalum (CUF), Saverina Mwijage, walitoa sukari sukari kilo 25 pamoja na mchele kilo 50.

“Ndugu zangu, tukio hili sio la Serikali au chama chochote, ni jambo la kitaifa. Serikali inapaswa kutenga fungu kubwa kwa ajili ya kuisaidia jamii,” Mbowe anakaririwa.

Akiwa katika shule ya Sekondari ya Ihungo iliyobomolewa na tetemeko la ardhi na kusababisha wanafunzi kukosa madarasa ya kusomea, Mbowe ambaye pia alisoma katika shule hiyo alitoa misaada mbalimbali.

Rais John Magufuli alilazimika kuahirisha safari yake ya kuhudhuria kuapishwa kwa Rais wa Zambia, Edgar Lungu kutokana na janga la tetemeko la ardhi, badala yake alimtuma Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kumuwakilisha.
Unknown Web Developer

Morbi aliquam fringilla nisl. Pellentesque eleifend condimentum tellus, vel vulputate tortor malesuada sit amet. Aliquam vel vestibulum metus. Aenean ut mi aucto.

Vitambulisho vya Taifa Kubadilishwa kuanzia Jumatano Septemba 14, 2016


Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inatarajia kubadilisha vitambulisho vyote vya zamani ambavyo havina saini, huku ikitarajia kutoa vitambulisho vipya vyenye saini kwa wananchi wote, waliokamilisha taratibu za usajili na utambuzi kwa kuchukuliwa alama za kibayolojia, ikiwemo alama za vidole, picha na saini ya kielektroniki.

Aidha, inatarajia kutoa vitambulisho vipya kuanzia Septemba 14, mwaka huu katika ofisi zote za Nida za wilaya. 

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Andrew Massawe, ilisema kwa sasa vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumika sambamba na vipya huku taratibu za kuvibadilisha zikiendelea.

‘’Kutokana na uwepo wa njia nyingi na salama za kusoma taarifa za mwombaji zilizomo ndani ya kifaa maalumi kilichofichwa kwenye kadi ya mtumiaji; ndiyo maana vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumikakatika huduma mbalimbali zinazohitaji kumtambua mtumiaji kabla ya kupata huduma,’’ alisema Massawe.

Alisema kuwa ofisi za wilaya zilizoanza usajili wa vitambulisho hivyo vipya kwa Tanzania Bara na Zanzibar ni mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Ruvuma na Dodoma.

‘’Waombaji wote ambao vitambulisho vyao viko tayari watatumiwa ujumbe mfupi wa maandishi katika simu zao za mkononi kuwafahamisha kufika vituo vya usajili kuchukua vitambulisho vyao,’’alisisitiza Massawe.

Alifafanua kuwa wananchi ambao hawakuwahi kusajiliwa na wana umri wa miaka 18 na kuendelea na kwa mikoa ambayo tayari kuna ofisi za usajili, wajitokeze kwa wingi kusajiliwa ili kupata vitambulisho hivyo.

‘’Kwa wale ambao walisajiliwa kupitia Daftari la Kudumu la Mpiga Kura la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Nida iko mbioni kuanza kutoa nambari za utambulisho wakati taratibu za uzalishaji zikiendelea,’’alisema.

Pia aliwakumbusha wananchi kutunza vitambulisho vyao ili kuepuka gharama kwani kitambulisho cha awali kilitolewa bure na iwapo kitapotea, ili kupata kingine lazima mtumiaji alipie.

Aliongeza kuwa kwa sasa vitambulisho hivyo vimeanza kutumika katika baadhi ya huduma hususani kwenye benki kwa ajili ya kufungua akaunti na kuthibitisha taarifa za mtu kabla ya kupata huduma.
Unknown Web Developer

Morbi aliquam fringilla nisl. Pellentesque eleifend condimentum tellus, vel vulputate tortor malesuada sit amet. Aliquam vel vestibulum metus. Aenean ut mi aucto.

Mrema Awapongeza Wabunge wa UKAWA Kwa Kukubali Kurudi Bungeni


Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Taifa, Augustine Mrema amewapongeza wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kwa kuamua kuacha kususa kuhudhuria vikao vya Bunge kushinikiza Naibu Spika, Tulia Ackson ajiuzulu au aondolewe kwenye wadhifa huo.

Mgomo huo ulisababisha wabunge wa Ukawa kutoshiriki kwenye Bunge la Bajeti, jambo ambalo limesababisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ipitishwe bila wabunge wa upinzani kuijadili na kuchangia mawazo yao bungeni.

Kwa mujibu wa barua yake kwenda kwa Spika wa Bunge Job Ndugai, Mrema ameeleza athari ya mgomo huo wa Ukawa kuwa ni kusababisha bajeti ya serikali ipitishwe kwa mawazo ya upande mmoja wa chama tawala.

Aidha, ilieleza kwamba mawazo ya wananchi kutoka kwenye majimbo yanayoongozwa na wabunge wa Ukawa yalikosekana, hivyo kuwafanya wabunge hao kuwanyima haki wapiga kura wao, kwa kuwakosesha uwakilishi kwenye Bunge la Bajeti.

“Bunge la bajeti ni kikao nyeti kwa vile linajadili na kupitisha mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka husika, ambayo yanamhusu na kumgusa kila mwananchi, hivyo haikuwa busara kwa wabunge wa Ukawa kususa vikao vya Bunge la Bajeti na kuwafanya wapiga kura wao wakose uwakilishi kwenye kikao nyeti kama hicho,” alisema. 

Mrema alisema, kuwepo kwao bungeni kungeweza kusaidia kuboresha bajeti hiyo kutokana na michango yao ya mawazo ambayo wangeyatoa na kupata bajeti bora zaidi kwa manufaa ya taifa.

“Sisemi kwamba bajeti iliyopitishwa ni mbaya, lakini kuwepo kwa wabunge wa upinzani kungesaidia kuboresha ili iwe nzuri zaidi kwa manufaa ya wapigakura wao waliowachagua majimboni mwao,”alisema.

Alisema “Hata kama Naibu Spika alikuwa na kasoro katika utendaji wake wa kazi, lakini Ukawa hawakupaswa kususa vikao vya bunge hilo, badala yake wangetafuta ufumbuzi wa suala kwa kufuata njia za kikatiba na kisheria, ikiwemo kutumia kanuni za Bunge.”

Alisema kwa kususa vikao vya Bunge, Ukawa wamesababisha madhara makubwa kwa wananchi hususani wapigakura wao ambayo hawawezi kulipika na wanaweza wakawaadhibu kwa kosa hilo kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020, kwa sababu wananchi waliwachagua ili kwenda kuwawakilisha bungeni na si kwenda kususia vikao vya Bunge.

“Sisi TLP tunaona kwamba Ukawa wamedhoofisha upinzani badala ya kuimarisha upinzani kama wenyewe wanavyodai, kwani huwezi kuimarisha upinzani kwa kususia vikao vya Bunge hususani Bunge la Bajeti,” alisema.

Alisema Ukawa wanapaswa kujifunza kwamba kususa vikao si mwarobaini wa kutatua mgogoro ya kisiasa, bali migogoro ya kisiasa hutatuliwa kwa kupitia njia za vikao na mazungumzo. 

Hata hivyo, alisema madhara yaliyopatikana kutokana na mgomo huo hayawezi kulipika kwa sababu Bunge la Bajeti limeshapita na haliwezi kurudiwa
Unknown Web Developer

Morbi aliquam fringilla nisl. Pellentesque eleifend condimentum tellus, vel vulputate tortor malesuada sit amet. Aliquam vel vestibulum metus. Aenean ut mi aucto.

Selection Za Vyuo Vikuu Kwa Walioomba Kujiunga na Vyuo Mbalimbali Mwaka Huu Zimetoka



Selection za TCU kwa walioomba kujiunga na vyuo mbalimbali kwa mwaka wa masomo 2016/2017  zimetoka.

==> Bofya hapa  kuangalia   <<Selection Status >> 

NB:  Tumia index number yako na password
Unknown Web Developer

Morbi aliquam fringilla nisl. Pellentesque eleifend condimentum tellus, vel vulputate tortor malesuada sit amet. Aliquam vel vestibulum metus. Aenean ut mi aucto.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumanne ya Septemba 13




Unknown Web Developer

Morbi aliquam fringilla nisl. Pellentesque eleifend condimentum tellus, vel vulputate tortor malesuada sit amet. Aliquam vel vestibulum metus. Aenean ut mi aucto.